habari Mpya


Serikali Yatumia Zaidi ya Bilioni 19 Kukarabati Shule Kongwe 17 Nchini.

Serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 19 kukarabati Shule kongwe 17 nchini lengo likiwa ni kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule hizo za kitaifa ambapo jukumu la uratibu wa ukarabati wa shule hizo 17 ilipewa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako anabainisha hayo wakati wa makabidhiano ya Miradi ya ukarabati wa shule hizo 17 yaliyofanyika katika shule ya sekondari ya Wavulana Sengerema, wilayani Sengerema Mkoani Mwanza ambapo amesema ukarabati huo umefanywa kwa kutumia fedha za Serikali.

 Prof. Ndalichako amesema ukarabati wa shule hizo 17 zilizosimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania ni utekelezaji wa mpango kabambe wa serikali wa kukarabati shule zote 89 kongwe za serikali ambapo amesema mpaka sasa tayari shule kongwe 46 zimeshakamilika. 

Amesema Serikali inaendelea na utekelezaj awamu ya tatu ya mpango huu ambapo shule nyingine 17 zitakarabatiwa mwaka huu wa fedha.

Akizungumzia ukarabati wa huo Waziri Ndalichako amesema kama uamuzi wa uboreshaji wa mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule kongwe usingefanyika mapema kungeweza kutokea majanga kwani hali ya miundombinu ilikuwa katika hali mbaya kwenye hasa katika mifumo ya umeme, maji safi na taka na mapaa mengi yalikuwa yameoza kabisa.

Prof. Ndalichako amesema serikali inaendelea kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji ambapo alitolea mfano katika mwaka wa fedha ulioisha wa 2018/19 serikali kupitia Mradi wa Lipa kulingana na Matokeo EP4R ilitenga na kutoa fedha ambazo ziliwezesha kujengwa kwa madarasa 1,208, mabweni 222, matundu ya vyuo 2,141 na nyumba za walimu 99 pamoja na kutatua changamoto ya huduma ya maji safi ambapo katika baadhi ya shule visima vilichimbwa.

Shule 17 zilizokarabatiwa kwa uratibu wa TEA ni pamoja na Shule ya sekondari ya Dodoma, Mwenge Sekondari Singida, Sekondari ya Wasichana Ruvu, Kilakala Sekondari na Shule ya Sekondari Ilboru.

Post a Comment

0 Comments