habari Mpya


Picha 7 za Ukarabati wa Meli ya Mv Victoria Ulipo Sasa.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti  akitizama Ukarabati wa meli ya Mv Victoria ulipo sasa na unatarajiwa  kukamilika ukarabati wake ifikapo March  2020.

  Picha Na: Sylvester Raphael.
Ni Meli kongwe na maarufu kwa wakazi wa Mkoa wa Kagera na inatarajiwa  kukamilika ukarabati wake ifikapo March  2020 na kurejea safari zake katika Ziwa Victoria kwa kufanya kazi kati ya bandari za Mwanza, Bukoba na Kemondo ikisafirisha abiria zaidi 1000 pamoja na mizigo tani 200  na inaelezwa italeta nafuu kubwa ya bidhaa za viwandani pamoja na usafiri wa wananchi kati ya Bukoba na Mwanza.
 
Uhakika wa meli ya MV Victoria kukamilika ukarabati wake mwakani March 2020 pia na ujenzi wa meli mpya ulishuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti pamoja na Kamati ya Amani ya Mkoa wa Kagera iliyowajumuisha Viongozi wa dini watatu Askofu Methodius Kilaini, Askofu msaidizi Jimbo Katoliki la Bukoba, Askofu Dk. Abednego Keshomshahara Askofu wa (KKKT) Jimbo la Kasikazini Magharibi na Sheikh Haruna Kichwabuta Sheikh wa Mkoa wa Kagera.
 
Bw. Eric B. Hamissi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za meli nchini alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Gaguti kutembelea miradi hiyo ya ujenzi na ukarabati wa meli na kutoa wito kwa wananchi na viongozi wengine nchini kwenda kutembelea miradi hiyo kujionea maendeleo ya ujenzi wa meli mpya na cherezo pia na ukarabati wa meli za zamani. 
Bw. Eric amesema kuwa mradi unatekelezwa na Kampuni ya JV of Gas Entec CO. Ltd Kang Nam Corporation na SUMA JKT ambapo kwa ujumla utagharimu jumla ya shilingi bilioni 152 na tayari Serikali imetoa shilingi bilioni 60 wakandarasi wanadaiwa kazi hawaidai Serikali aidha, mradi umegawanyika katika sehemu kuu nne.

Kwanza ni ujenzi wa meli mpya ambayo itakuwa na uwezo wa kubeba tani 400 Abiria 1200 ikiwa na urefu wa meta 92.6, urefu kwenda juu meta 11.2 (sawa na ghorofa nne) na upana wa meta 17 na gharama yake ni shilingi bilioni 90.

Mradi wa pili ni ujenzi wa cherezo ambacho kitakuwa na uwezo wa kubeba meli zenye uzito wa tani 4000 ambapo meli mpya itakuwa na uzito wa tani 3500 tu aidha, cherezo kama hicho hakuna katika nchi za Afrika Mashariki na Kati na kikikamilika kitaiingizia Serikali Mapato kama kitatumika kwa kujenga meli zenye uzito mkubwa hasa kutoka nje ya Tanzania. 

Mradi wa cherezo utagharimu shilingi bilioni 36 na ujenzi wake umefikia asilimia 52.

Mradi wa tatu ni ukarabati wa Meli ya Mv Victoria ambao utagharimu shilingi bilioni 22.8 na ukarabati wa meli hiyo umefikia asilimia 50 ambapo inakarabatiwa ikiwa ni pamoja na kubadilishwa mfumo wake wa zamani na kuwekewa mfumo wa kidigitali.

Mradi wa wa nne ni ukarabati wa meli ya Butihama ambapo mradi huo nao utagharimu shilingi bilioni 4.9 na ukarabati wake umefikia asilimia 40. 
Aidha Viongozi hao wa Dini Askofu Msaidizi Methodius Kilaini ,Askofu Dk. Keshomshahara na Sheikh Haruna Kichwabuta  kwa pamoja  wamesema kuwa Rais Magufuli alihaidi wakati wa kampeini sasa ametekeleza bila ahadi hewa hasa kwa Wananachi wa Mkoa wa Kagera na kumshukuru Rais John Pombe Magufuli kwa kutekeleza maajabu katika miradi ya ujenzi na ukarabati wa meli. 

Post a Comment

0 Comments