habari Mpya


Hii Ndiyo Miradi Mikubwa ya Maendeleo Kagera Inayojengwa Sasa.

Katika kuhakikisha kuwa miradi ya kutolea huduma kwa wananchi inasimamiwa na kutekelezwa kwa viwango stahiki ili itoe huduma iliyokusudiwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli imekuwa ikiboresha mazingira ya watendaji wake wanaosimamia miradi hiyo ya maendeleo kwa kuwajengea miundombinu bora inayowawekea mazingira bora pia ya kutekeleza majukumu yao ikiwemo ofisi na makazi yao.

Miradi hiyo ya Serikali yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni mbili (2) katika Mkoa wa Kagera ni pamoja na ujenzi wa Ofisi za Wakuu wa Wilaya mpya tatu za Biaharamulo, Muleba na Kyerwa, ujenzi wa nyumba ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Kyerwa, pia ujenzi wa ofisi tano za Maafisa Tarafa katika Wilaya za Kyerwa, Biharamulo, Karagwe, Muleba na Bukoba vijijini.
Akikagua miradi ya ujenzi wa Ofisi za Wakuu wa Wilaya Biharamulo na Muleba Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti ,Septemba 18, 2019 aliridhishwa na viwango pia ubora wa majengo hayo mawili yanayoendelea kujengwa na kampuni ya SUMA JKT na kusema kuwa majengo hayo yanaonesha thamani halisi ya kiasi cha fedha zilizotumika.

Katika ukaguzi huo , Gaguti alito wito kwa Kampuni ya ujenzi ya SUMA JKT ihakikishe inaendela kutekeleza miradi yake kwa ubora unaotakiwa lakini pia aliishauri Kampuni hiyo ya SUMA JKT kuona namna bora ya kupunguza gharama zake za ujenzi na kutekeleza miradi mingi ya Serikali.
Serikali ya Awamu ya Tano tayari imetoa fedha za ujenzi za ofisi za Wakuu wa Wilaya za Biharamulo shilingi milioni 295, Muleba shilingi milioni 690, Kyerwa shilingi milioni 541.

Ujenzi wa nyumba ya Katibu Tawala Kyerwa shilingi milioni 159, ujenzi wa ofisi za Maafisa Tarafa tano shilingi milioni 326, ujenzi wa miundombinu hiyo upo katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji.

Aidha, katika mkoa wa Kagera Serikali imetoa fedha za kutekeleza pia miradi ya kutolea huduma za jamii na utekelezaji wake unaendelea, Serikali ilitoa shilingi bilioni 4.5 za ujenzi wa Hospitali za Wilaya za Bukoba (vijijni), Karagwe na Kyerwa tayari hospitali zimekamilika.
Serikali ilitoa shilingi milioni 169 za upanuzi wa wodi ya wazazi na kujenga vyumba viwili vya upasuaji katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kagera, ujenzi upo katika hatua za mwisho kukamilika ili kuanza kutoa huduma kwa wananchi akina mama wajawazito.

Vilevile katika kusogeza karibu huduma kwa wananchi Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ilitoa shilingi bilioni 5.9 za ujenzi wa vituo 14 vya afya katika mkoa wa kagera ambavyo vimejengwa na kukamilika na tayari vinatao huduma kwa wananchi wa Kagera.

Wito kwa wananchi ni kuendelea kushirikiana na Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo pia kuitunza miradi hiyo ili idumu na kuendelea kutoa huduma stahiki.

Post a Comment

0 Comments