habari Mpya


Habari Kubwa za Saa 24 Radio Kwizera October 8,2019.

Source; RK: SD (mahakamani)
ED: AG
Date: Tuesday, October 08, 2019
NGARA

Mkazi wa kijiji cha Kigina kata ya Ntobeye wilayani Ngara Mkoani Kagera   amefikishwa katika Mahakama ya wilaya hiyo akikabiliwa na tuhuma ya kukutwa na gunia 70 za bangi ambazo alikuwa amezihifadhi nyumbani kwake

Akisoma mashitaka dhidi ya Mtuhumiwa, mwendesha mashitaka wa polisi Bw. Jumanne Maatu mbele ya hakimu Mfawidhi Frendinard Kiwonde amemtaja mtuhumiwa kuwa ni Ramadhani Abdul ambaye alikamatwa Octoba 05 mwaka huu majira ya  usiku.

Kutokana na kesi hiyo kutokuwa na mdhamana, hakimu mfawidhi  wa wilaya ya Ngara  Bw. Frendinard Kiwonde amesema kuwa  mtuhumiwa  hapaswi kuzungumza lolote na amepelekwa rumande hadi Octoba 22,2019 kesi yake itakapotajwa tena kwa mara ya pili huku jalada lake likipelekwa kwa mwanasheria mkuu wa Serikali.


Source; RK: Gmika (AJARI)
ED: AG
Date: Tuesday, October 08, 2019
GEITA

Mtoto mwenye umri wa miaka mitatu katika kitongoji cha Izenga wilayani Chato Mkoani Geita amefariki papo hapo baada ya kuangukiwa na ukuta wa kanisa ulioporomoka siku ya Jumapili wakati ibada ikiendelea.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Geita Mponjori Mwabulambo amesema katika tukio hilo pia watu watano wamejeruhiwa.

Hata hivyo, chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo la kanisa ni kutokana na ujenzi usiokuwa na viwango na kwamba mpaka sasa majeruhi waliokuwa wakitibiwa katika zahanati ya Buseresere wameruhusiwa huku mmoja aliyepewa rufaa ya kutibiwa katika kituo cha afya Bwanga akiendelea na matibabu.

Kufuatia tukio hilo baadhi ya wananchi mkoani Geita wameiomba serikali kuchunguza upya majengo ya makanisa yanayojengwa ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika kwa waumini wanapokuwa kwenye ibada.

Source; RK: AE (Ujenzi wa machinjio)
ED: AG
Date: Tuesday, October 08, 2019
KIGOMA

Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma imeonyesha kutoridhishwa na kiwango cha ujenzi wa machinjio katika eneo la Kibirizi ikilinganishwa na fedha iliyotolewa na serikali kukamilisha mradi huo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Huduma za Jamii Manispaa ya Kigoma Ujiji Bw.Hussein Kalyango, mradi huo ulioanza tangu Januari 2018 hadi sasa umeshindwa kukamilika kwa wakati na kwamba licha ya changamoto hiyo kiasi cha shilingi milioni 40 kimeshatumika.

Aidha ameongeza kuwa kutokamilika kwa mradi huo kunaikosesha mapato halmashauri ya Kigoma Ujiji na kwamba kamati ya Uchumi, Elimu na afya haikubaliana na hatua zinazoendelea na hivyo wahusika wa mradi huo wanatakiwa kuwajibika.
 Kwa upande wao baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wamesema ni vema serikali ikapitia majumuisho ya mradi huo sambamba na kuchukua hatua kwa wahusika kwakuwa gharama zilizotumika hadi sasa haziendani na kiwango cha ujenzi unaoendelea.


Source; RK: AG (Ziara)
ED: AG
Date: Tuesday, October 08, 2019
RUKWA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakt. John Magufuli amelipongeza jeshi la polisi nchini kwa kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha usalama wa raia na mali zake.

Rais Magufuli ametoa pongezi hizo hii leo akiwa wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa wakati akiwahutubia wakaazi wa mkoa huo.

Amesema vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi kubwa hasa ya kusuruhisha matatizo ya watu huku akiwataka kutomuonea mtu wanapokuwa wanatimiza majukumu yao.


Rais Dakt. John Magufuli yupo mkoani Rukwa kwa ziara ya kikazi ambapo amefungua na kukagua miradi ya Maendeleo pamoja na kuzungumza na Wananchi wa Maeneo mbalimbali ya Rukwa na Wilaya zake.

Source; RK: AS (majanga)
ED: AG
Date: Tuesday, October 08, 2019
PWANI

Kutokana na kuwa na uelewa mdogo kwa baadhi ya waandishi wa habari juu ya majanga yanayotokea katika jamii, imeasababisha baadhi yao kuandika habari zilizoegemea upande mmoja.

Hayo yameelezwa na mtaalam wa majanga kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Bw. Celvin Robert wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari  juu ya kuandika na kuandaa vipindi vinavyohusiana na majanga mbalimbali yanayotokea katika jamii.

Bw. Robert amesema ili kujenga taifa stahimilivu waandishi wa habari wanalo jukumu la kuleta mabadiliko katika jamii kwa kuandika habari zenye ukweli na uhakika wa tukio husika.
 Kwa upande wake Mtaalam wa Maafa, Majanga na Uchumi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Charles Msangi amesema waandishi wa habari wanatakiwa kuzingatia utu pindi wanapoandika na kuandaa vipindi vinavyohusu majanga yanayosababisha kukatisha uhai wa watu na viumbe hai.

Jumla ya waandishi wa habari 25 kutoka radio za kijamii Tanzania bara na visiwani Zanzibar ikiwemo Radio Kwizera wanashiriki mafunzo ya siku tano ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari juu ya kuandika na kuandaa vipindi vya kukabiliana na majanga yanayofanyika wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

Post a Comment

0 Comments