habari Mpya


Kigoma Kunufaika na Ujenzi wa Madaraja ya Mawe.

Na- Geofrey A.Kazaula na Bebi Kapenya - Kigoma.

 Wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wanatarajia kunufaika na  Ujenzi wa Madaraja ya mawe unaofadhiliwa na Serikali ya Ubelgiji chini ya mradi wa Kilimo endelevu katika Mkoa wa Kigoma  (Sakirp – Enabel)  na kusimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kigoma Bi. Pendo E. Mangali ameeleza kuwa mradi huo uliibuliwa na wananchi baada ya kueleza changamoto wanayokutana nayo katika kusafirisha mazao yao kutoka mashambani hadi majumbani na kwenye masoko.

Kiongozi huyo amebainisha kuwa mradi huo wa Ujenzi wa madaraja ya mawe unalenga kutatua kero ya usafiri na usafirishaji wa mazao na kwamba wananchi walihamasishwa na wakakubali kujitokeza katika kusomba mawe na kushiriki kujenga madaraja hayo.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Mhandisi Pharles E. Ngeleja  ameeleza kuwa Ujenzi wa madaraja kwa teknolojia ya kutumia mawe ni wa gharama  nafuu na kwamba una washirikisha wananchi moja kwa moja kwa kukusanya vifaa vinavyopatikana katika mazingira yao hususani mawe na wafadhili wanatoa vifaa vya viwandani visivyopatikana kwenye mazingira mfano simenti huku TARURA wakisimamia shughuli za ujenzi .
Akiongea kwa niaba ya wananchi wanaoshiriki katika ujenzi wa madaraja hayo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyabigufa  Ndg. Johnphace Kabora Tunzwe  amesema kuwa changamoto ya usafiri ni kubwa hasa kipindi cha masika na hivyo tayari wameamua kujitolea kwa kukusanya mawe ili kujenga madaraja .

Aidha ameongeza kuwa baada ya kukamilisha ujenzi wa daraja, kazi itakayokuwa imebaki ni Kufungua barabara za kufika mashambani ili kuwasaidia wananchi kusafirisha mazao yao na kwamba anaimani kuwa  Serikali kupitia TARURA watafungua barabara .

Naye Meneja mshauri wa mradi huo chini ya Serikali ya Ubelgiji Ndg. Steven Hollevoet ameeleza kuwa Teknolojia ya ujenzi wa madaraja ya mawe ni ya muda mrefu hasa katika nchi za Ulaya na Asia na sasa wameileta Tanzania ili kuwafundisha wananchi kujenga madaraja kwa gharama nafuu kwasababu vifaa vinavyotakiwa kama mawe na mchanga vinapatikana kwa urahisi.
Hadi sasa madaraja sita yamekamilika na madaraja tisa yapo katika hatua mbalimbali huku lengo likiwa ni kukamilisha madaraja kumi na tano ifikapo mwezi Desemba, 2019.

Post a Comment

0 Comments