habari Mpya


Karibu Uwekeze kwenye Maeneo haya Yaliyotengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Ngara .

Serikali ya Awamu ya tano chini ya Rais  Dk. John Pombe Magufuli ina malengo ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda. 

Rais Magufuli amekuwa akisema Wawekezaji wapewe nafasi na wasicheleweshwe wakati wanapohitaji kuwekeza katika nchi hii.
Katika kutekeleza maagizo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ngara Bw. Aidan J. Bahama kupitia Halmashauri ametenga maeneo maalum kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda, kilimo na sehemu za malisho ya mifugo.

Maeneo yaliyotengwa na Halmashauri ya wilaya ya Ngara mkoani Kagera ni eneo la Lumasi lenye ekari 1133 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda , eneo la Kazingati (Msalasi na Mabonde yanayozunguka) jumla ya ekari 5190 kwa ajili ya kilimo cha kahawa na mpunga na bonde la Bigombo kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. 

 Maeneo mengine ni ya ujenzi wa masoko ya kimkakati katika mipaka ya Kabanga na Rusumo yenye jumla ya ekari 22.83.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa maonesho ya Wiki ya Uwekezaji Kagera,Mkurugenzi Mtendaji wa Ngara, Bw.Bahama alisema kuwa anawakaribisha wawekezaji wa nje na ndani ya nchi kuja kuwekeza wilayani Ngara maana maeneo makubwa yapo,yenye rutuba nzuri kwa ajili ya kilimo,hali ya hewa ya Ngara ni nzuri, miundombinu ya maji,barabara,umeme,usalama na huduma za kiafya zinapatikana kwa urahisi.

Ngara pia imejaliwa kuwa na madini ya Nikeli na Bati ambayo pia wawekezaji wanakaribishwa kubisha hodi ,Halmashauri iko tayari kuwafungulia milango kwa ajili ya uwekezaji.

"Ukiachilia mbali Kilimo na Ufugaji, Ngara tumejaliwa vivutio vingi vya utalii kama Maporomoko Rusumo,Mafiga Matatu(Sehemu ambayo ukisimama utaziona nchi tatu za Tanzania,Burundi na Rwanda kwa pamoja), Makazi ya Chifu Baramba II yenye zana za jadi,sehemu ya hifadhi ya Burigi yenye wanyamapori mbalimbali,Kaburi walipozikwa watu 917 kwa pamoja waliouawa wakati wa vita vya Kimbale nchini Rwanda pamoja na pango lililojengwa na Wajerumani kabla ya vita kuu ya kwanza ya dunia.

Kutoka kwenye 10% ya mapato ya ndani, Halmashauri ya Ngara imewawezesha kikundi cha vijana cha Uzuri ambacho kimeweza kuanzisha kiwanda kidogo cha viatu vya ngozi.

Post a Comment

0 Comments