habari Mpya


Boti Yawaka Moto Kagera Abiria Watatu Wakijeruhiwa na Wengine 56 Wakinusurika Kifo.

Na: Sylvester Raphael.

Abiria 56 wanusurika kifo baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kutoka Kemondo Wilayani Bukoba kuelekea Rushonga Bumbire Wilayani Muleba mkoani Kagera,kuwaka moto na kubadili uelekeo na kusababisha tafrani kubwa kwa abiria waliokuwemo katika boti hiyo.

Akitoa taarifa ya ajali hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera REVOCATUS MALIMI amesema kuwa boti ijulikanayo kwa jina la Lulimbe ikiwa imebeba abiria 56 na mizigo yao ilianza safari majira ya saa 8:00 mchana Septemba 16, 2019 muda mchache baada ya kuanza safari ilishika moto gafla na kubadili elekeo kurudi bandarini ilikotoka.
Kamanda MALIMI amesema kuwa katika boti hiyo yenye uwezo wa kubeba abira 84 abiria waliokuwemo 56 waliokolewa na wananchi waliokuwa nchi kavu pia abiria wengine waliweza kujiokoa kwa kougelea majini. 

Aidha, majeruhi watatu walikimbizwa katika Hospitali ya Mtakatifu Joseph Kagondo na kupatiwa matibabu ambapo hali zao zinaendelea vizuri.
Shuhuda wa tukio hilo aliyekuwa katika boti hiyo BW. MICHAEL DOMINICK mkazi wa Isamilo Mwanza amesema kuwa mara baada ya kuanza safari umbali kidogo kutoka mwaloni gafla ulitokea mlipuko mkubwa eneo la nyuma ya boti kwenye injini na kusababisha moto mkubwa uliogeuza mwelekeo wa boti kwasababu ya upepo na kurudi bandarini ilikotoka abiria wakipiga kelele kuomba msaada na wengine kurukia majini kuogelea ili kujiokoa. 
 
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali MARCO E. GAGUTI akiwapa pole manusura wa ajali hiyo na kuzungumza na wananchi katika eneo hilo la tukio aliwasisitiza wananchi kuhakikisha wanazingatia usalama wao wakatia wa kusafiri kwa kuvaa life jacket na kwataka wakaguzi wa vyombo vya usafiri majini kuhakikisha wanavikagua kikamilifu kabla ya kuanza safari.

Pia na nyinyi wananchi mtusaidie sisi Serikali kwa kuhakikisha mnavikagua vyombo hivi kabla ya safari mkivitilia mashaka toeni taarifa kwa mamlaka husika ili tuweze kudhibiti ajali hizi kabla ya kutokea.” Amesitiza Mkuu wa Mkoa GAGUTI. 
Mkuu wa Mkoa GAGUTI pamoja na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama ya mkoa waliwatembelea majeruhi watatu katika Hospitali ya Mtakatifu Joseph Kagondo kuwajaulia hali ambapo majeruhi hao walikuwa wakiendelea kupatiwa matibabu na hali zao zikiwa zinaendelea vizuri. 

Majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo ni ELIZABETH MSIWA (28), AGNES WILIAM (42) Mkazi wa Kataoro Buseresere Na MARIAM DEUS (30). 
 

Post a Comment

0 Comments