habari Mpya


Wafanya biashara Kagera tumieni fursa ya kuwa mipakani kujiinua kiuchumi

Wafanyabiashara mkoani Kagera wametakiwa kutumia fursa ya mpaka wa Rusumo kuingia nchini Rwanda kufanya biashara zenye kukuza uchumi wa Nchi na kipato cha Watanzania

Hayo yamesemwa na balozi wa Tanzania Nchini Rwanda Ernest Mangu wakati wa kikao cha kujadili namna ya kuboresha biashara za watanzania kuingia nchini Rwanda kilichofanyika wilayani Ngara kikiwahusisha viongozi wa mkoa wa Kagera na baadhi ya wawakilishi wa wafanyabisahara.
Balozi Mangu amesema wafanyabishara wanapaswa kuwa wabunifu hasa kutumia jiografia ya mipaka ya nchi yetu kwa kuangalia zaidi kuuza bidhaa zao katika nchi za Congo na Rwanda kwakuwa mazingira ya biashara ni mazuri na kwamba Shughuli hiyo ikifanyika kwa kuzingatia sheria itaongeza kipato na kodi ya nchi.


Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jeneral Marco Elisha Gaguti  amesema nia ya serikali ni kuona wafanyabishara wananufaika kupitia biashara zao na kwamba maafisa biashara katika halmashauri zote nane za mkoa  wanapaswa kuorodhesha majina ya wafanyabishara wenye uwezo wa kufanya biashara za kuvuka mipaka ya nchi ili wajengewe uwezo wa kuingia katika soko la ushindani.
Awali baadhi ya wafanyabiashara waliohudhiria kikao hicho wamesema ili kuwe na uwanja sawa katika biashara serikali inapaswa kuziangalia upya baadhi ya mamlaka zake zilizo mipakani na vituo vya ukaguzi ili kuepuka kuwakatisha tamaa wafanyabisahara.
Post a Comment

0 Comments