JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI
MAPENDEKEZOYA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2019/2020.
13 Juni, 2019 Dodoma
HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. PHILIP I.
MPANGO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI
MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2019/2020.
I.
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kukubali
kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2019/20. Hii ni
bajeti ya nne ya Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bajeti hii
inawasilishwa kwa kuzingatia matakwa ya Ibara ya 137 ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na kifungu cha 26 cha Sheria
ya Bajeti namba 11 ya mwaka 2015.
2.
Mheshimiwa Spika, hotuba hii inaambatana na vitabu vinne vya bajeti. Kitabu cha Kwanza ni
Makadirio ya Mapato; Kitabu cha Pili ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Wizara,
Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali; Kitabu cha Tatu ni
Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni Makadirio ya Matumizi ya Maendeleo kwa Wizara,
Idara Zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2019 pamoja
na Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Serikali wa mwaka 2019 ambavyo ni sehemu ya
bajeti hii.
3.
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumuinulia Mungu moyo wangu wote kwa shukrani, kwa kuwa
amenijalia mema mengi katika maisha yangu na katika utumishi wangu kwa Taifa.
Ninamshukuru kwa kuendelea kuijalia nchi yetu amani na umoja na kutupatia safu
ya juu ya uongozi wa Taifa hili unaomtanguliza Mungu katika kuwatumikia
Watanzania wote na kujielekeza kutatua kero za wanyonge.
4.
Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo kwa Mwenyezi Mungu, naomba nimpongeze kwa dhati Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu na Mwenyekiti
wa CCM Taifa, kwa uongozi wake shupavu na wa mfano katika bara la Afrika hususan
katika kufanya maamuzi magumu yenye maslahi mapana kwa Taifa. Katika kipindi
cha uongozi wake: amesimamia kwa ujasiri uvunaji adili wa rasilimali za Taifa; ameongoza
mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi bila kigugumizi; amedhibiti biashara
haramu ya madawa ya kulevya; ameimarisha nidhamu na uwajibikaji katika utumishi
wa umma; na ameendelea kusikiliza na kushughulikia malalamiko na kero za
makundi mbalimbali katika jamii, wakiwemo wajasiriamali wadogo (wamachinga na
mama/baba lishe), wafanyabiashara wadogo wa madini, wakulima na wafugaji, na wafanyabiashara
wa kati na wakubwa kutoka katika wilaya zote nchini. Vile vile, ameendelea
kudumisha amani na usalama katika nchi. Aidha, amethubutu kutekeleza miradi
mikubwa ya kielelezo ili kujenga Tanzania mpya. Nitaeleza hapo baadaye mafanikio
makubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuleta mabadiliko chanya ya
kiuchumi na kijamii nchini. Kwa sasa itoshe tu niseme kuwa yalihitajika maamuzi
magumu kutoka kwa kiongozi jasiri kuelekeza utekelezaji wa mageuzi makubwa na miradi
ya kielelezo ambayo yameleta maendeleo makubwa na ya kuvutia katika miaka hii
mitatu na nusu tu! Watanzania tunayo kila sababu ya kujivunia kumpata kiongozi
shupavu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mwenye uthubutu na uzalendo
wa hali ya juu.
5.
Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo, ninapenda kumshukuru
kipekee Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini katika dhamana hii kubwa ya
Waziri wa Fedha na Mipango na hivyo kuniwezesha kuandaa na kusoma hotuba ya
bajeti kuu ya Serikali hivi sasa kwa mara ya nne mfululizo. Kwa unyenyekevu,
ninasema asante sana Mheshimiwa Rais kwa heshima hii kubwa uliyonipatia mimi na
wananchi wenzangu wa wilaya ya Buhigwe na mkoa wa Kigoma kwa ujumla. Ninayasema
haya nikitambua kwamba wapo Watanzania wengi wenye sifa za kuwa Waziri wa Fedha
na Mipango. Mimi ni nani basi hata nikateuliwa na kukabidhiwa majukumu haya
makubwa? Kama alivyonijibu yeye mwenyewe siku aliponiteua, kazi hii nimepewa
kwa neema tu kutoka kwa Mungu. Hivyo, napenda niwaahidi tena Watanzania kuwa
nitaendelea kuifanya kazi hii ya Mungu kwa uadilifu.
6.
Mheshimiwa Spika, naamini Watanzania watakubaliana nami kuwa nguzo ya uongozi thabiti ni wasaidizi imara na wanaojituma. Hivyo, kwa
namna ya pekee, napenda nimpongeze Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa busara na bidii katika kazi
zake za kumsaidia Rais kuongoza Taifa letu. Nimpongeze pia Mheshimiwa Dkt. Ali
Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi kwa kuendelea kuiongoza Zanzibar kwa hekima, hali ambayo
imewaletea wananchi wa Zanzibar maendeleo yanayoonekana katika kipindi cha
uongozi wake. Kadhalika, napenda kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Kassim
Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mbunge wa jimbo la
Ruangwa, kwa uongozi hodari ndani ya Serikali na hapa Bungeni pamoja na kumsaidia Rais kufuatilia kwa karibu utekelezaji
wa ahadi zilizomo katika Ilani ya CCM kwa Ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.
Vile vile kwa namna ya pekee sana nimpongeze Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, Katibu
Mkuu wa CCM kwa utendaji wake uliotukuka na kusimamia misingi ya Chama Cha
Mapinduzi ya kupigania usawa wa binadamu na haki za wanyonge.
7.
Mheshimiwa Spika, niwapongeze pia wakuu wa mihimili mingine ya dola kwa usimamizi na uongozi
shupavu, hususan wewe Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Kongwa kwa kuongoza vema mhimili
wa Bunge. Hakuna shaka hata kidogo na kila mtu sasa anajua kwamba Bunge hili ni
chombo chenye nguvu sana chini ya Mheshimiwa Spika, Job Ndugai na Naibu Spika Mheshimiwa
Dkt. Tulia Ackson (Mb). Aidha, ninampongeza sana Mheshimiwa Profesa Ibrahim
Hamisi Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania kwa uongozi makini wa mhimili wa Mahakama.
8.
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Balozi John Kijazi, Katibu Mkuu
Kiongozi ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Mawaziri na Mkuu wa Utumishi wa Umma,
kwa kutekeleza kazi zake kwa weledi mkubwa.
9.
Mheshimiwa Spika, napenda niwapongeze na kuwashukuru kwa dhati wakuu wote wa vyombo vya
ulinzi na usalama, makamanda na askari wote (wanaovaa na wasiovaa sare za
majeshi) kwa utumishi wao makini na uzalendo wa hali ya juu. Kipekee naomba niwatambue
Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo; Inspekta Jenerali wa
Polisi, Simon Nyakoro Sirro; Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Faustine
Martin Kasike; Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Peter Makakala;
Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Dkt. Modestus Francis Kipilimba; Mkurugenzi
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Kamishna wa Polisi, Diwani
Athuman Msuya; Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Madawa ya
Kulevya, Rogers William Siang’a; na Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji, Thobias
Andengenye. Hakika, Watanzania tunatembea kifua mbele na kutekeleza shughuli
mbalimbali za kijamii na kiuchumi bila wasiwasi kwa sababu vyombo vyetu vya
ulinzi na usalama viko macho na imara kuliko chuma! Tunawaomba muendelee
kutimiza wajibu wenu wa kulinda mipaka na amani ya nchi yetu kwa wivu na moyo
wa kizalendo na hivyo kuzidi kuimarisha mazingira ya kuwasha moto wa maendeleo
na ustawi wa Taifa letu na wananchi wake.
10.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee ninamshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Profesa Adelardus Lubango Kilangi kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2019 na
Muswada wa Sheria ya Matumizi wa mwaka 2019. Napenda pia nitumie fursa hii kumpongeza kwa dhati
mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti
Mheshimiwa George Boniface Simbachawene, Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, na Makamu
wake Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi,
kwa umakini wao katika kuongoza shughuli za Kamati hii muhimu sana. Chini ya
uongozi wao, Kamati ya Bajeti imetupatia maoni mengi na ushauri wa kujenga
ambao umeisadia sana Serikali katika kuboresha mapendekezo ya bajeti hii.
11.
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi chote
ambacho nimekuwa kwenye nafasi hii, napenda nishuhudie kwa Bunge hili na Taifa kwa
ujumla kwamba, Kamati hii ya Bajeti imetoa mchango mkubwa sana katika kuboresha
sera za uchumi na bajeti kuliko Watanzania wengi wanavyofahamu. Kusema kweli
wanastahili kutambulika kipekee. Kama kuna nishani au tuzo ya Spika kwa Kamati
ya Bunge inayojitanabaisha kwa utumishi uliotukuka, basi kama itakupendeza
Mheshimiwa Spika, napendekeza iwe Kamati ya kwanza kutunukiwa heshima hiyo. Aidha,
ninawapongeza Wenyeviti, Makamu wenyeviti na wajumbe wa Kamati zote za Kudumu
za Bunge kwa michango yao waliyoitoa kupitia vikao vya kamati za kisekta katika
kuboresha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara mbalimbali na Serikali kwa
ujumla kwa mwaka 2019/20. Maboresho hayo yalilenga kuwapatia Watanzania
maendeleo hususan uboreshaji wa huduma za kijamii na miundombinu.
12.
Mheshimiwa Spika, bajeti ya mwaka
2019/20 imeandaliwa kwa kuzingatia dhamira
ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwainua wananchi wanyonge kiuchumi na
kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuwekeza hapa nchini. Dhima kuu kama
ilivyokubaliwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki bado itaendelea
kuwa “kujenga
uchumi wa viwanda utakaochochea ajira na ustawi endelevu wa jamii”.
Bajeti hii inaendelea kufungamanisha juhudi za kuimarisha sekta ya viwanda na uendelezaji
wa sekta ya kilimo inayoajiri wananchi wengi na hasa waishio vijijini huku
msisitizo ukiwa katika kuhamasisha tija na uzalishaji, kujenga miundombinu ya
kiuchumi, kutafuta masoko, kupunguza kero kwa wakulima, wafugaji, wavuvi,
wafanyabiashara na wawekezaji na kuimarisha huduma za jamii.
13.
Mheshimiwa Spika, leo asubuhi niliwasilisha Hotuba
ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa
mwaka 2019/20 ambapo nilieleza kwa kina mwenendo wa
viashiria mbalimbali vya uchumi katika mwaka 2018. Aidha, katika hotuba hiyo,
nilifafanua juu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2018/19
na kuainisha maeneo ya vipaumbele kwa mwaka 2019/20. Hivyo, katika hotuba hii,
nitajielekeza kutoa tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2018/19 na ahadi
zilizomo katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, kuwasilisha maboresho
ya mfumo na viwango vya kodi na tozo mbalimbali, pamoja na mapendekezo ya
makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2019/20, ambayo yanatoa picha ya
namna gani Serikali inakusudia kuendelea kukuza uchumi, kuboresha kilimo,
miundombinu, huduma na kujenga uchumi wa viwanda ili kuongeza ajira na
kuboresha ustawi wa Watanzania.
II.
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2018/19
Mwenendo wa Mapato
14.
Mheshimiwa Spika, Katika bajeti ya mwaka
2018/19, Serikali ilitarajia kupata jumla ya shilingi trilioni 32.48 kutoka
katika vyanzo vyote vya ndani na nje. Mchanganuo wa mapato yaliyopatikana hadi
Aprili 2019 ikilinganishwa na lengo la kipindi hicho ni kama ifuatavyo:
(i)
Mapato ya kodi yalifikia shilingi trilioni 12.9, sawa
na asilimia 87.4 ya lengo;
(ii)
Mapato yasiyo ya kodi yalifikia shilingi trilioni
2.04, sawa na asilimia 122 ya lengo. Mapato yasiyo ya kodi yalivuka lengo
kutokana na kuimarika kwa matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji wa maduhuli
kwenye taasisi za Serikali kupitia Mfumo
wa Kielektroniki wa Serikali wa
Ukusanyaji wa Mapato (Government electronic Payment Gateway –GePG);
(iii)
Mapato ya Halmashauri yalifikia shilingi bilioni
529.25, sawa na asilimia 72 ya lengo;
(iv) Misaada na Mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ilifikia
shilingi trilioni 1.70 sawa na asilimia 86 ya lengo;
(v)
Mikopo ya ndani ikijumuisha mikopo ya kulipia dhamana
za Serikali zilizoiva ilifikia shilingi trilioni 3.3, sawa na asilimia 57.4 ya
lengo; na
(vi) Mikopo ya masharti ya kibiashara ya nje ilifikia shilingi bilioni 692.3.
15.
Mheshimiwa Spika, kutofikiwa kwa malengo ya
mapato ya kodi kulitokana na sababu mbalimbali, zikiwemo; ugumu wa
kutoza kodi sekta isiyo rasmi; kuendelea kuwepo kwa upotevu wa mapato kunakosababishwa
na tatizo la magendo hususan kupitia bandari bubu kwenye mwambao mrefu wa
Bahari ya Hindi; na mwamko mdogo wa wananchi kudai risiti za kielektroniki
wanapofanya manunuzi au baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kutotoa
risiti wanapofanya mauzo.
16.
Mheshimiwa
Spika, kutopatikana kwa mikopo ya
ndani kama ilivyotarajiwa kumetokana na kupungua kwa washiriki katika soko la
fedha la ndani hususan mifuko ya hifadhi ya jamii iliyokuwa kwenye zoezi la
kuunganishwa. Kwa upande wa mikopo ya nje ya kibiashara, upungufu uliojitokeza
ulitokana na hali ya masoko ya fedha kimataifa kubana zaidi (tighter global
financial conditions) hususan kuimarika kwa dola ya Marekani, na riba kubwa za
mikopo. Hali hii pia ilipelekea majadiliano na taasisi za fedha za Kimataifa
kuchukua muda mrefu ili kuhakikisha kuwa Serikali inapata mikopo hiyo kwa
gharama zinazohimilika.
17.
Mheshimiwa Spika, mwenendo wa
upokeaji wa misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo
ulikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya Washirika wa Maendeleo
kutotimiza ahadi zao kama walivyoahidi kwenye bajeti kinyume na misingi ya
makubaliano kama ilivyoainishwa kwenye Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo
Tanzania (Development Coperation Framework – DCF).
Mwenendo wa Matumizi
18.
Mheshimiwa Spika, bajeti ya mwaka 2018/19
iliyoidhinishwa na Bunge ilikuwa shilingi trilioni 32.48 ambapo shilingi
trilioni 20.47 ni matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 12.01 ni matumizi ya
maendeleo. Katika kipindi cha Julai, 2018 hadi Aprili 2019, Serikali imetoa
jumla ya shilingi trilioni 22.19 zikijumuisha shilingi bilioni 529.25 kutoka
kwenye makusanyo ya Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kati ya kiasi hicho, shilingi
trilioni 16.75 zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambazo zinajumuisha
shilingi trilioni 6.28 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa umma, shilingi
trilioni 2.49 kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi trilioni 7.98 kwa
ajili ya kugharamia deni la Serikali na mahitaji mengine ya Mfuko Mkuu.
19.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Aprili 2019
Serikali imetoa jumla ya shilingi trilioni 5.44 kwa ajili ya utekelezaji wa
miradi ya maendeleo ambapo shilingi trilioni 4.89 ni fedha za ndani na shilingi
bilioni 547.38 ni fedha za nje. Hata hivyo, kiasi hiki hakijumuishi baadhi ya
fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo zilizopelekwa moja kwa moja kwenye
utekelezaji wa miradi (D-Funds) ambazo hazikupita kwenye mfumo wa malipo wa
Serikali. Fedha hizi zitajumuishwa pindi taratibu za kiuhasibu zitakapokamilika
mwishoni mwa mwaka wa fedha.
20.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mamlaka za
Serikali za Mtaa hadi kufikia Aprili 2019 jumla ya shilingi bilioni 529.25
ambazo zinatokana na makusanyo yao ya ndani zimetumika. Kati ya kiasi hicho,
shilingi bilioni 211.7 zimetumika kugharamia miradi ya maendeleo na shilingi
bilioni 317.55 zimetumika kugharamia matumizi ya kawaida.
21.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa maeneo ya
kimkakati ambayo yamepatiwa fedha katika kipindi cha Julai 2018 hadi Aprili
2019 ni pamoja na:
(i)
Kulipa mishahara ya watumishi
kila mwezi kwa wakati ambapo hadi Aprili 2019 jumla ya shilingi trilioni 6.3
zimelipwa;
(ii)
Kuendelea kulipa madeni ya
Serikali kwa mujibu wa mikataba ambapo jumla ya shilingi trilioni 5.7 zilitumika,
ikijumuisha shilingi trilioni 2.8 kwa ajili ya kulipa mtaji wa deni la ndani
kwa utaratibu wa “rollover”.
(iii)
Kugharamia uendeshaji wa ofisi
ambapo jumla ya shilingi trilioni 2.2 zimelipwa;
(iv)
Mradi wa kufua umeme utokanao
na nguvu za maji katika Mto Rufiji ambapo kiasi cha shilingi bilioni 723.6 kimetolewa;
(v)
Kugharamia elimu msingi bila
ada na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, ambapo zimetolewa shilingi bilioni 616.9;
(vi)
Awamu ya Tatu ya Mradi wa
Kupeleka Umeme Vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) jumla ya
shilingi bilioni 269.3 zimetolewa;
(vii)
Ununuzi na uendeshaji wa ndege
mpya ambapo zimetolewa shilingi bilioni 238.8;na
(viii) Kuendeleza
ujenzi wa meli mpya katika maziwa makuu, zimetolewa shilingi bilioni 27.6.
Ulipaji wa Malimbikizo
ya Madai
22.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhakiki na
kulipa madeni ya wazabuni, makandarasi na watumishi ambapo hadi Mei 2019 kiasi
cha shilingi bilioni 598.4 kimelipwa kati ya
bajeti iliyotengwa ya shilingi bilioni 600.0 kwa mwaka 2018/19. Kati ya kiasi
kilicholipwa shilingi bilioni 300.5 ni kwa ajili ya wakandarasi, shilingi
bilioni 232.9 ni kwa ajili ya watoa huduma, na shilingi bilioni 65.0 ni kwa ajili ya watumishi. Aidha, Serikali imelipa
malimbikizo ya kimshahara ya watumishi 790 waliostaafu kabla hawajalipwa,
ambapo hadi Aprili, 2019 jumla shilingi bilioni 3.10 zililipwa.
23.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga
fedha kwa ajili ya kulipa madai yaliyohakikiwa na kuchukua hatua mbalimbali kwa
lengo la kupunguza ulimbikizaji wa madai ikiwa ni pamoja na kuhimiza
uzingatiaji wa Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015; Sheria ya Ununuzi wa Umma
SURA 410; Sheria ya Fedha za Umma SURA 348 na miongozo na maelekezo mbalimbali
yanayotolewa na Serikali.
24.
Mheshimiwa Spika, napenda nisisitize kuwa
japokuwa rasilimali fedha zinazopatikana hazitoshi kugharamia mahitaji yote ya
kawaida na miradi ya maendeleo, hakuna shaka kwamba kupitia jitihada
tunazofanya hivi sasa, tunapanda mbegu leo ambazo zimeanza na zitaendelea kuzaa
matokeo mazuri ya Tanzania ya uchumi wa kati.
Mafanikio ya
Serikali ya Awamu ya Tano katika Kutekeleza Ilani ya CCM 2015
25.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano
inatekeleza kwa dhati ahadi zake kama zilivyobainishwa katika Ilani ya Uchaguzi
ya CCM ya mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano
2016/17-2020/21 na vipaumbele vilivyobainishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania wakati wa ufunguzi rasmi wa Bunge la 11 mnamo tarehe 20/11/2015.
26.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa bajeti hii ni ya nne,
niruhusu tujikumbushe kwa uchache maeneo ambayo Mheshimiwa Rais aliyawekea
mkazo mkubwa mwanzoni mwa utawala wake. Maeneo hayo ni pamoja na: kuendeleza ukuaji wa uchumi na kujenga uchumi
wa kipato cha kati; kuongeza mapato na kuimarisha usimamizi wa matumizi ya
Serikali; kuendeleza na kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya barabara na
madaraja, viwanja vya ndege, reli mpya, bandari na umeme; ujenzi wa viwanda;
kuongeza kasi ya kuzalisha ajira na kupunguza umaskini; kuhakikisha kwamba
madini na maliasili zetu zinatumika kwa manufaa ya Taifa letu; kuboresha sekta
ya kilimo, mifugo na uvuvi; kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma za maji, afya
na elimu (ikiwa ni pamoja na kuweka mkazo katika viwango vya ubora wa elimu na
stadi za kazi); mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi; kuboresha mazingira ya
uwekezaji; Kuendeleza utalii; kushughulikia migogoro ya ardhi; kurejesha
nidhamu katika utumishi wa umma; na kuhakikisha kila mmoja wetu anafanya kazi.
.
27.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka mitatu
na nusu ya uongozi wa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, mafanikio mengi
yamepatikana katika maeneo niliyoyataja hapo juu, ikiashiria kwamba Ilani ya CCM
ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 inatekelezwa ipasavyo.
28.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mafanikio ya
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika kipindi cha miaka mitatu na nusu
ya Serikali ya Awamu ya Tano ni pamoja
na:
(i)
Ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard
gauge, ambapo hadi Aprili 2019 ujenzi wa
kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) umefikia asilimia 48.9 na
kipande cha Morogoro – Makutupora (km 422), ujenzi umefikia asilimia 7.12.
Mradi huu utakapokamilika utaboresha usafiri nchini na kuwezesha usafirishaji
wa mizigo (mazao, mifugo, madini, mazao ya misitu) na abiria kwenda na kutoka
nchi jirani zisizo na bahari (Uganda, Rwanda, Burundi, DRC) na kuiwezesha
Tanzania kuwa kitovu cha biashara na huduma (trade and logistics hub) katika
nchi za maziwa makuu. Aidha, mradi huu utapunguza uharibifu wa barabara
unaotokana na usafirishaji wa mizigo mizito kwa malori, utapunguza msongamano
wa shehena ya mizigo katika bandari ya Dar es Salaam na kutoa fursa za ajira;
(ii)
Ufufuaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ambapo
hadi Aprili 2019 jumla ya ndege sita mpya zimenunuliwa na kuanza kutoa huduma
za usafiri wa anga nchini (Dar es Salaam, Mwanza, Bukoba, Kigoma, Tabora,
Dodoma, Iringa, Mbeya, Songea, Mtwara, Arusha, Mpanda) na kimataifa (Hahaya –
Comoro, Lusaka, Harare, Entebbe, Bujumbura). Aidha, ndege nyingine mpya aina ya
Boeing 787-8 Dreamliner na Bombadier Q400 zinatarajiwa kuwasili nchini mwishoni
mwa mwaka 2019. Hivi karibuni, ATCL inatarajiwa kuanza safari kwenda Mumbai
(India), Johannesburg (Afrika Kusini) na Guangzhou (China). Kuimarishwa kwa
usafiri wa anga kutasaidia sana kukuza biashara na sekta ya utalii nchini;
(iii)
Ujenzi wa jengo la tatu la abiria (Terminal III) na
miundombinu yake katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere
lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka umekamilika;
(iv) Ujenzi wa barabara kuu na za mikoa kwa kiwango cha lami, ikiwemo daraja
la juu la Mfugale katika makutano ya TAZARA; ujenzi wa barabara ya juu yenye
ngazi tatu (ubungo interchange) katika makutano ya Ubungo; barabara ya njia
nane kutoka Kimara Dar es Salaam hadi Kibaha (km 19); daraja la Magufuli katika
mto Kilombero; na kuanza ujenzi wa daraja jipya la Selander jijini Dar es
Salaam ikijumuisha barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 5.2;
(v)
Ujenzi wa meli mpya za kubeba mizigo na abiria kwenye Ziwa
Victoria, Tanganyika na Nyasa;
(vi) Kukamilika kwa upanuzi wa gati namba moja, kuanza ujenzi wa gati namba
mbili, na kuendelea na ujenzi wa sakafu ngumu katika gati la kupakua na kupakia
magari katika bandari ya Dar es Salaam. Upanuzi huu utawezesha meli kubwa
kuingia na kutoka bandarini kwa ajili ya kushusha na kupakia mizigo;
(vii) Ujenzi wa mradi wa kihistoria wa kufua umeme utokanao na nguvu ya maji
katika Mto Rufiji wenye uwezo wa kuzalisha MW 2,115 ambapo ujenzi wa
miundombinu wezeshi imekamilika na mkandarasi wa kutekeleza ujenzi huo
ameshapatikana. Mradi huu utaiwezesha nchi yetu kuwa na umeme wa uhakika na wa
gharama nafuu ambao ni wa lazima katika jitihada na dhamira yetu kama Taifa ya
kujenga uchumi wa viwanda. Mradi huu pia utafungua fursa za utalii, uvuvi na
kilimo cha umwagiliaji; na
(viii) Kuendelea na utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Kupeleka Umeme Vijijini
(REA) ambapo hadi Mei 2019, jumla ya vijiji 7,127 vimeunganishiwa umeme.
29.
Mheshimiwa Spika, yapo pia mafaniko makubwa yaliyopatikana
katika kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma za jamii kwa kipindi cha Awamu
ya Tano ambayo ni pamoja na;
(i)
Kuendelea na utekelezaji wa ahadi ya kugharamia elimu
msingi (kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne) bila ada na kuongezeka kwa
utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu;
(ii)
Ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vyuo vikuu
ikiwemo kukamilika na kuzinduliwa kwa maktaba ya kimataifa yenye uwezo wa
kuhudumia wanafunzi 2,100 kwa wakati mmoja katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;
(iii)
Kuboreshwa kwa huduma za afya katika hospitali za
rufaa, mikoa, wilaya, vituo vya afya na zahanati nchini. Aidha, upatikanaji wa
dawa, vifaa tiba, vitendanishi na huduma za kibingwa umeimarika. Vile vile,
idadi ya wagonjwa waliokuwa wanapelekwa kutibiwa nje imepungua na hivyo kuokoa
fedha ambazo zingetumika kwa ajili ya matibabu nje ya nchi; na
(iv) Kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za maji safi mijini na vijijini
ambapo katika Jiji la Dar es Salaam
umefikia asilimia 85, katika mikoa mingine asilimia 80, miji midogo asilimia 64
na vijijini asilimia 64.8.
30.
Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine
yaliyopatikana katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano ni:
(i)
Kutengamaa kwa viashiria vya uchumi jumla ikiwemo
ukuaji wa Pato la Taifa kwa wastani wa asilimia 6.9 katika kipindi cha miaka
mitatu iliyopita (2016 – 2018), kukua kwa sekta ya kilimo kwa wastani wa
asilimia 5.3, mfumuko wa bei wa tarakimu moja ya kiwango cha wastani wa
asilimia 4.7 katika kipindi hicho, utulivu wa thamani ya shilingi, na kupungua
kwa kiwango cha umaskini kutoka asilimia 28.2 hadi asilimia 26.4.
(ii)
Serikali kuhamia makao makuu ya nchi, Dodoma na
kuendeleza eneo la Mji wa Serikali kwa kujenga majengo 23 ya ofisi za wizara
zote na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na miundombinu yake (umeme, maji,
barabara).
(iii)
Kudhibiti utoroshaji na uuzaji wa madini nje ili
kuwezesha Taifa kunufaika na rasilimali zake ikiwa ni pamoja na kufanya
marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, kutunga Sheria ya Mamlaka ya
Nchi Kuhusiana na Umiliki wa Maliasili ya Mwaka 2017, ujenzi wa uzio kuzunguka
eneo la migodi ya Tanzanite Mirerani na kuanzisha masoko ya madini;
(iv) Kuanza utekelezaji wa Mkakati wa Kuharakisha Maendeleo ya viwanda Nchini
(Fast Tracking Industrialization Strategy). Aidha, sekta binafsi pamoja na
mifuko ya hifadhi ya jamii zimewekeza kwenye miradi ya viwanda ambapo mifuko
hiyo inaendeleza miradi 7 kati ya miradi 25;
(v)
Mifumo ya kielektroniki ya usimamizi na ukusanyaji wa
mapato imeimarishwa;
(vi) Usimamizi wa fedha za Serikali umeimarishwa, ikiwa ni pamoja na
kuanzisha Akaunti Jumuifu ya Hazina;
(vii) Kuimarishwa kwa taasisi za umma na zile ambazo Serikali ina hisa. Serikali
imeendelea kufuatilia na kusimamia kwa karibu zaidi utendaji katika mashirika
ya umma ili kuhakikisha kuwa michango na gawio stahiki inatolewa kwa Serikali. Katika
kuimarisha mashirika ya umma na taasisi ambazo Serikali ina hisa, Serikali
imepata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na mashirika mengi ambayo yalikuwa
hayatoi gawio na michango stahiki kwa Serikali kuanza kufanya hivyo. Mwaka
2015/16 kulikuwa na mashirika 13 tu yaliyotoa gawio kwa Serikali kiasi cha
shilingi bilioni 119.2 na sasa yameongezeka kufikia mashirika 28 ambayo hadi
Mei 2019 yalikuwa yametoa gawio la jumla ya shilingi bilioni 497.5.
(viii) Serikali imefanya majadiliano yenye maslahi kwa Taifa na baadhi ya makampuni
ikiwemo kampuni ya “Airtel Tanzania” ambayo yameleta mafanikio yafuatayo: Umiliki
wa hisa za Serikali kuongezeka kutoka asilimia 40 hadi asilimia 49 bila
kuzilipia, Mwenyekiti wa Bodi na Afisa Mkuu wa Ufundi (Chief Technical Officer)
kuteuliwa na Serikali, Kampuni kuilipa Serikali shilingi bilioni moja kila
mwezi kwa kipindi cha miaka mitano ambapo kiasi cha shilingi bilioni 3
kimeshalipwa kwa kipindi cha mwezi Aprili, Mei na Juni 2019, Kupatikana kwa
kiasi cha dola za Marekani milioni moja kutoka kwa Mwenyekiti wa “Bharti Airtel”
kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii (Corporate Social Responsibility) ambazo
zimeelekezwa kujenga hospitali mpya ya kisasa Dodoma, Kufutwa kwa madeni na
madai ya “Bharti Airtel” kwa Airtel (T) kiasi cha shilingi bilioni 937 (Dola
milioni 407.38), na Serikali kupata gawio maalum kutoka mapato ghafi ya Airtel
Tanzania kwa mwaka 2019; na
(ix) Mafanikio katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ambapo ripoti ya
uwazi ya kimataifa (Transparency International) ya mwaka 2018 imeonesha
Tanzania imeshika nafasi ya 16 kwa nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara
ikilinganishwa na nafasi ya 27 mwaka 2015.
31.
Mheshimiwa Spika, kwa matokeo haya
niliyoeleza, ni wazi kabisa kuwa Taifa letu linakwenda mbele chini ya Serikali
hii ya tano ya CCM na liko katika mwelekeo sahihi (moving forward in the right
direction). Serikali ya CCM chini ya Jemadari Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
inawashukuru sana wananchi wote wa Tanzania waliotimiza wajibu wao wa msingi
kwa kulipa kodi ipasavyo na hivyo kuwezesha Taifa kupata mafanikio hayo makubwa
sana katika kipindi kifupi. Wananchi wamejitoa na kuonesha uzalendo wa hali ya
juu kwa kushiriki kwenye ujenzi wa Tanzania mpya. Mafanikio haya pia ni matunda
mazuri ya kutunza nidhamu katika usimamizi wa uchumi, udhibiti wa mianya ya
upotevu wa mapato na matumizi yasiyo na tija ya fedha za umma. Bajeti hii
ninayowasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu itaendelea kutekeleza malengo ya
Serikali kama yalivyoanishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 na
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17-2020/21.
III.
SERA ZA BAJETI
KWA MWAKA 2019/20
Shabaha za Uchumi Jumla
32.
Mheshimiwa Spika, Shabaha za uchumi jumla katika
kipindi cha mwaka 2019/20 ni kama ifuatavyo:-
(i)
Pato la Taifa kukua kwa
asilimia 7.1 mwaka 2019 kutoka ukuaji halisi wa asilimia 7.0 mwaka 2018;
(ii)
Mfumuko wa bei kuendelea
kubaki katika wigo wa tarakimu moja kati ya asilimia 3.0 hadi 4.5 katika
kipindi cha muda wa kati;
(iii)
Mapato ya ndani kufikia asilimia
15.8 ya Pato la Taifa mwaka 2019/20 kutoka matarajio ya asilimia 14.3 mwaka 2018/19;
(iv)
Mapato ya kodi kufikia
asilimia 13.1 ya Pato la Taifa mwaka 2019/20 kutoka matarajio ya asilimia 12.1
mwaka 2018/19;
(v)
Matumizi ya Serikali kufikia
asilimia 22.7 ya Pato la Taifa mwaka 2019/20
kutoka matarajio ya asilimia 21.6 mwaka 2018/19; na
(vi)
Nakisi ya bajeti inakadiriwa kufikia
asilimia 2.3 ya Pato la Taifa mwaka 2019/20 kutoka matarajio ya asilimia 2.0
mwaka 2018/19.
Sera na Mikakati ya Kuongeza Mapato
33.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20, Serikali
imekusudia kuongeza na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa lengo la
kuiwezesha kugharamia shughuli za Serikali ikiwemo miradi mikubwa ya
miundombinu na huduma za jamii. Katika kufanikisha azma hii, Serikali itatekeleza
sera zifuatazo:
(i)
Kuboresha mazingira ya kufanya
biashara ili kuvutia uwekezaji, ukuaji wa biashara ndogo na za kati ili kupanua
wigo wa kodi na mapato mengine ya Serikali;
(ii)
Kurekebisha viwango vya kodi
kwa lengo la kuhamasisha uzalishaji na kulinda viwanda vya ndani dhidi ya
ushindani kutoka nje;
(iii)
Kuboresha mazingira ya ulipaji
kodi kwa hiari, upanuzi wa wigo wa kodi na matumizi ya TEHAMA katika usimamizi
wa kodi;
(iv)
Kuimarisha usimamizi wa sheria
za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato,
pamoja na kuweka mkazo zaidi katika kutoa elimu kwa mlipakodi;
(v)
Kuimarisha makusanyo yasiyo ya
kodi kwa kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA;
(vi)
Kuendelea kuwianisha na
kupunguza tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na wakala, taasisi na Mamlaka za
Serikali za Mitaa; na
(vii)
Kuiongezea Mamlaka ya Mapato
ya Tanzania uwezo hususan watumishi, vitendea kazi bora na mafunzo ili kutambua
na kudhibiti mbinu za ukwepaji kodi.
34.
Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo ya
makadirio ya mapato ya ndani, Serikali imeandaa mikakati mahsusi ya kiutawala
itakayotekelezwa katika kipindi cha muda wa kati. Mikakati hiyo inajumuisha:
(i)
Kuongeza ufanisi katika
usimamizi na ukusanyaji wa kodi za ndani kwa kutekeleza Mfumo Jumuishi wa
Usimamizi wa Mapato ya Ndani (Integrated Domestic Revenue Admistrative System-IDRAS);
(ii)
Kupanua wigo wa kodi kupitia
utambuzi na usajili wa walipakodi wapya pamoja na kuendelea na zoezi la
urasimishaji wa sekta isiyo rasmi;
(iii)
Kuwekeza kwenye maeneo ambayo
Serikali inaweza kupata mapato zaidi hususan katika uvuvi wa bahari kuu kwa
kujenga bandari ya uvuvi na ununuzi wa meli za uvuvi;
(iv)
Kuimarisha uwezo wa
ufuatiliaji na udhibiti wa uhamishaji wa faida unaofanywa na kampuni za kimataifa;
(v)
Kuimarisha usimamizi wa
misamaha ya kodi kwa kuhakikisha inaelekezwa kwenye miradi inayokusudiwa;
(vi)
Kuhakikisha kuwa maduhuli yote
yanapitia katika Mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato
(GePG) ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato; na
(vii)
Kuimarisha mifumo ya
ufuatiliaji katika taasisi za Serikali ili kuhakikisha kuwa michango stahiki ya
taasisi za umma kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali inawasilishwa kwa wakati.
35.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa misaada na mikopo
nafuu kutoka nje, Serikali itaendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Washirika
wa Maendeleo. Aidha, Serikali itaendeleza mazungumzo na Washirika wa Maendeleo ili kila upande uzingatie
misingi na kanuni za ushirikiano wa maendeleo pamoja na kuendeleza majadiliano ya
kimkakati (Strategic Dialogue) na kumaliza tofauti za kisera au kimtazamo pindi
inapojitokeza, pasipo kuathiri utoaji wa fedha za utekelezaji wa Bajeti ya
Serikali.
36.
Mheshimiwa Spika, kuhusu mikopo ya kibiashara ya
ndani na nje, Serikali itaimarisha uhamasishaji wa wadau katika soko la ndani
kwa lengo la kuimarisha ushiriki wao katika minada ya dhamana za Serikali.
Aidha, jitihada zinafanyika ili kuvutia wawekezaji mbalimbali kutoka nje ya
nchi wenye nia ya kuikopesha Serikali ili kuwezesha utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya maendeleo yenye tija kwa uchumi wa Taifa letu.
Sera za Matumizi
37.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20, Serikali
itaendelea kusimamia nidhamu katika matumizi ya fedha za umma na kufanya
ufuatiliaji na tathmini ya matumizi hususan katika miradi ya maendeleo. Lengo kuu ni kuwa na matumizi bora ya fedha katika
utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha upatikanaji wa thamani ya
fedha. Aidha, Serikali itaendelea kuhakiki, kulipa na kuzuia kuongezeka kwa
malimbikizo ya madai kwa Serikali. Pia, Serikali itaendelea kuelekeza
fedha kwenye maeneo ya kipaumbele yenye kuchochea ukuaji wa uchumi.
Maeneo ya vipaumbele kwa mwaka
2019/20
38.
Mheshimiwa Spika, katika Hotuba niliyoiwasilisha
asubuhi kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa mwaka 2019/20, niliainisha vipaumbele kwa mwaka 2019/20 ambavyo
vitatekelezwa kwa kuzingatia umuhimu wa pekee wa kulinda mazingira nchini
(environmental sustainability). Bajeti hii inalenga kutekeleza vipaumbele hivyo
kama ifuatavyo:
(i)
Viwanda na kilimo: Katika kuendeleza azma ya kujenga
uchumi wa viwanda, katika mwaka 2019/20 Serikali itajikita kuvutia uwekezaji zaidi
kwenye viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini kama vile mazao ya
kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini; kuzalisha bidhaa
kwa ajili ya soko la ndani na ziada kwa ajili ya kuuza nje, pamoja na kuongeza
fursa za ajira. Vile vile kama wote tunavyofahamu, sekta ya kilimo (mazao,
uvuvi, mifugo na misitu) ni muhimu sana kwa uendelezaji wa viwanda Tanzania kwa
kuwa sehemu kubwa ya malighafi za viwanda zinatokana na kilimo. Katika
kuimarisha sekta hii, Serikali itaendelea kutekeleza Programu ya Kuendeleza
Sekta ya Kilimo awamu ya pili (ASDP II) hususan kuhakikisha upatikanaji wa mbegu
bora, pembejeo, huduma za ugani, masoko, miundombinu wezeshi na tafiti, ikiwa ni
pamoja na kupeleka fedha zaidi kwenye maeneo wezeshi kwa kilimo na kutoa nafuu
za kikodi. Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha bodi za mazao,
kuboresha na kuhamasisha uanzishwaji wa vyama vya ushirika vya mazao ili
kuviwezesha kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha kwa ajili ya kuwekeza
kwenye shughuli mbalimbali za kilimo na uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo
vya kuongeza thamani ya mazao.
(ii)
Ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu: Licha ya
kutilia mkazo kuongeza ukuaji wa sekta kuu za uchumi zinazotegemewa na kuajiri
Watanzania wengi, bajeti ya 2019/20 itaelekezwa kuimarisha upatikanaji wa
huduma bora za afya, elimu na ujuzi, chakula na lishe bora na huduma za maji
safi na salama. Aidha, kupitia bajeti hii, msukumo utawekwa katika kuongeza
ubora wa nguvukazi ili iendane na mahitaji ya soko la ajira.
(iii) Uboreshaji wa mazingira wezeshi
kwa uendeshaji biashara na uwekezaji: Bajeti hii imeweka
msisitizo mkubwa katika kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu hususan reli,
bandari, nishati, barabara, madaraja, na viwanja vya ndege. Aidha, Serikali
itaendelea kupitia na kuimarisha mifumo
ya kisera, kisheria na kitaasisi, sambamba na kuimarisha ulinzi na usalama ili
kushawishi na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje. Napenda niwahakikishie wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi kwa ujumla kuwa kuanzia mwaka
ujao wa fedha, Serikali itaanza kutekeleza kwa nguvu zaidi mpangokazi wa
kuboresha mazingira ya biashara (Blueprint
for the Regulatory Reforms to improve the Business Environment) ili
mazingira ya biashara nchini yawe rafiki zaidi na yenye gharama nafuu.
(iv) Ufuatiliaji na tathmini Bajeti hii pia inakusudia kuimarisha zaidi ufuatiliaji na tathmini ya
utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika ngazi zote. Aidha, Serikali itaimarisha
usimamizi wa ukusanyaji mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ili kuongeza ufanisi
katika utekelezaji wa bajeti lakini wakati huo huo kuhakikisha kuwa ukusanyaji
wa kodi unafanyika bila kuathiri biashara. Napenda kuwasisitiza tena watumishi
wa TRA kwamba hairuhusiwi kufunga biashara ili kushinikiza mfanyabiashara alipe
kodi au malimbikizo ya kodi isipokuwa kwa kibali cha Kamishna Mkuu wa TRA.
IV.
MABORESHO YA MFUMO WA KODI, ADA NA TOZO MBALIMBALI
39.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho
ya mfumo wa kodi ikiwemo baadhi ya viwango vya kodi, tozo na ada zinazotozwa
chini ya Sheria mbalimbali na pia taratibu za ukusanyaji na usimamiaji wa
mapato ya Serikali. Marekebisho haya yamezingatia dhamira ya Serikali ya
kuendelea kuwa na mfumo wa kodi ambao ni tulivu na wa kutabirika (stable and
predictable). Vilevile yanalenga pamoja na mambo mengine, kuchochea kasi ya
ukuaji wa uchumi hususan katika sekta ya kilimo, viwanda, kukuza ajira, na
kuongeza mapato ya Serikali. Aidha, Serikali
imeanza kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara
(BluePrint) ulioidhinishwa mwaka 2017/18 kwa kuanza kupitia mfumo wa tozo
na ada mbalimbali zinazotozwa na Mamlaka za Udhibiti kwa lengo la kupunguza au
kuzifuta baadhi ya tozo na ada, kupunguza na kuondoa muingiliano katika kutoza
tozo hizo. Marekebisho yanayopendekezwa yanahusu Sheria zifuatazo:-
(a)
Sheria
ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148;
(b)
Sheria
ya Kodi ya Mapato, SURA 332;
(c)
Sheria
ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
(d)
Sheria
ya Usimamizi wa Kodi, SURA 438;
(e)
Sheria
ya Usalama Barabarani, SURA 168;
(f)
Sheria
ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004;
(g)
Sheria
ya Bajeti, SURA 439;
(h)
Marekebisho
madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali;
(i)
Kuanza
utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara (Blueprint)
kwa kurekebisha Ada na Tozo mbalimbali;na
(j)
Hatua
za Kisera na Kiutawala katika Kuboresha ukusanyaji wa mapato.
(a)
Sheria ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani, SURA 148
40.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho
kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura 148 kama ifuatavyo:-
(i)
Kusamehe Kodi ya
Ongezeko la Thamani kwenye makasha yenye majokofu (HS Code 8418.69.90)
yanayotumika kwenye Kilimo cha Kisasa cha mboga mboga (horticulture) kwa
wakulima watakaoingiza makasha hayo kutoka nje ya nchi kwa matumizi ya kilimo.
Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama na kutoa unafuu katika uzalishaji
na kuhamasisha kilimo cha kisasa
cha mboga mboga nchini;
(ii)
Kufanya marekebisho
kwenye Kifungu cha 68(3)(d) ili kisihusishe uuzaji wa mazao ghafi ya kilimo nje
ya nchi. Lengo la hatua hii ni
kuwawezesha wauzaji wa mazao ghafi ya kilimo nje ya nchi kuendelea kufanya
biashara hiyo kwa kadri ya kibali kitakavyotolewa na Serikali;
(iii)
Kusamehe Kodi ya
Ongezeko la Thamani kwenye vifaa vya kukaushia nafaka (Grain Drying Equipment
HS Code 8419.31.00). Msamaha huu unatarajiwa kutoa unafuu kwenye gharama za
kukausha nafaka kwa ajili ya kuzihifadhi. Aidha hatua hii itachochea ukuaji wa
kilimo cha mazao ya nafaka;
(iv) Kupunguza kiwango cha Kodi ya Ongezeko la Thamani kutoka asilimia kumi na
nane (18) hadi asilimia sifuri (0) kwenye huduma ya umeme unaouzwa kutoka
Tanzania Bara kwenda Tanzania Zanzibar ili kuwapunguzia gharama za maisha
wananchi wa Tanzania Zanzibar. Serikali iliridhia na kuelekeza kuwa umeme
unaouzwa kutoka Tanzania Bara kwenda Tanzania Visiwani utozwe Kodi ya Ongezeko
la Thamani kwa kiwango cha asilimia sifuri;
(v)
Kutoa msamaha wa Kodi
ya Ongezeko la Thamani kwa vilainishi vya ndege vinavyoingizwa nchini na
waendeshaji wa ndani, Shirika la ndege la Taifa, au mashirika ya ndege
yanayotambulika katika Mikataba ya Kimataifa ya Huduma za Anga (Bilateral Air
Services Agreements) kwa Kufanya marekebisho ya Sehemu ya Pili ya Jedwali la
Misamaha la Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani katika kipengele cha 11.
Hatua hii itawezesha nchi yetu kusaini Mikataba ya Kimataifa ya Huduma za Anga
ambayo ilishindikana kusainiwa hapo awali kutokana na kutokuwepo kwa msamaha
huo;
(vi) Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye tiketi za ndege, vipeperushi,
kalenda, shajara, karatasi zenye nembo na sare za wafanyakazi zilizowekwa nembo
ya Shirika husika la ndege, kwa kufanya marekebisho ya Sehemu ya Pili ya
Jedwali la Misamaha la Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kuongeza
kipengele kipya kinachotoa msamaha pale vinapoingizwa nchini na mashirika ya
ndege yanayotambulika katika Mikataba ya Kimataifa ya Huduma za Anga. Hatua hii
itawezesha nchi yetu kusaini Mikataba ya Kimataifa ya Huduma za Anga ambayo
ilishindikana kusainiwa hapo awali kutokana na kutokuwepo kwa msamaha huo; na
(vii) Kufuta msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani uliokuwa unatolewa kwenye
taulo za Kike (HS Code 9619.00.10) kwa kuwa haujawezesha kupatikana kwa bidhaa
hiyo muhimu kwa bei nafuu kwa walengwa na badala yake unawanufaisha
wafanyabiashara. Aidha, wakati Serikali ilipoweka msamaha huu ilitarajia kwamba
wazalishaji wa taulo za kike wataziuza kwa bei nafuu baada ya kusamehewa kodi.
Hatua zote za Kodi ya Ongezeko la Thamani
kwa ujumla wake zinatarajiwa kupunguza
mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi
milioni 1,646.7
(b)
Sheria ya Kodi ya
Mapato, SURA 332
41.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho
kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 kama ifuatavyo:-
(i)
Kupunguza kiwango cha
Kodi ya Mapato ya Makampuni (Corporate Income Tax) kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato kutoka asilimia 30
hadi asilimia 25 kwa kipindi cha miaka miwili (2) kuanzia mwaka 2019/20 hadi
mwaka 2020/21 kwa wawekezaji wapya wa viwanda vya kuzalisha taulo za kike.
Aidha, Serikali itaingia mkataba wa makubaliano (Performance Agreement) na kila
mwekezaji ambao utaainisha wajibu wa kila upande. Lengo la hatua hii ni kuvutia
uwekezaji katika uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu, kuongeza ajira na mapato ya
Serikali. Vile vile hatua hii itapunguza matumizi ya fedha za kigeni
zinazotumika kuagiza bidhaa hiyo kutoka nje na kuhamasisha uzalishaji wake
ndani ya nchi;
(ii)
Kusamehe Kodi ya Zuio
inayotozwa kwenye gharama zinazoambatana na mikopo (mfano ada za bima, gharama
ya usimamizi, na uandaaji wa mkopo, na ada nyingine zinazoendana na gharama za
mkopo) kwa mikopo inayotolewa na Benki, Taasisi za Fedha za nje na wahisani
mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Serikali. Lengo la hatua hii
ni kuiwezesha Serikali kupata mikopo kwa gharama nafuu na kwa muda mfupi.
Aidha, msamaha huu utaiwezesha Serikali kutekeleza miradi yake kwa wakati;
(iii)
Kutoa msamaha wa
kutengeneza hesabu ambazo zinatakiwa kuwasilishwa Mamlaka ya Mapato Tanzania
kwa ajili ya ukokotoaji wa Kodi ya Mapato kutoka kiwango cha sasa cha shilingi
milioni ishirini (20,000,000/=) hadi shilingi milioni mia moja (100,000,000/=).
Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama kwa mlipa kodi ya kutafuta mtaalam
(Certified Public Acountant) kwa ajili ya kutengeneza hesabu. Aidha, hatua hii
inalenga pia kuchochea ulipaji kodi wa hiari na kuongeza mapato ya Serikali; na
(iv) Kusamehe kodi kwenye mauzo ghafi yasiyozidi shilingi milioni nne
(4,000,000/=) kwa wenye vitambulisho vya wajasiriamali na kupunguza kiwango cha
chini cha kodi kutoka shilingi laki moja na nusu (150,000/=) kwa mwaka hadi
shilingi laki moja (100,000/=) kwa mwaka kama ilivyofafanuliwa kwenye Jedwali
Na. 1 na Na. 2. Lengo la hatua hii ni kupunguza mzigo wa kodi kwa walipakodi
wadogo pamoja na kuoanisha viwango vya kodi na kiwango cha chini kinachotakiwa
kwa mfanyabiashara kutumia mashine ya kodi ya kielektroniki (EFD) ambacho kwa
sasa ni shilingi milioni kumi na nne (14,000,000/=). Aidha, hatua hii inalenga
pia katika kusisitiza matumizi ya mashine za kielektroniki (Electronic Fiscal
Device- EFD) ili kuwezesha ukokotoaji wa kodi ulio sahihi na kuongeza ulipaji
kodi wa hiari.
Jedwali Na.1: Viwango vya sasa vinavyotozwa kodi kwa
Wafanyabiashara wasiotengeneza Vitabu vya Hesabu
Mauzo
(Shilingi)
|
Kodi ya kulipa kwa
Mfanyabiashara asiye na Kumbukumbu kamili kwa mujibu wa kifungu cha 35 cha
Sheria ya Usimamizi wa Kodi
|
Kodi ya kulipa kwa
Mfanyabiashara mwenye kumbukumbu kamili kwa mujibu wa kifungu cha 35 cha
Sheria ya Usimamizi wa Kodi
|
Mauzo yasiyozidi Shilingi
4,000,000
|
Hamna
|
Hamna
|
Mauzo yanayozidi shilingi
4,000,000 lakini hayazidi shilingi 7,500,000
|
Shilingi
150,000
|
Asilimia 3 ya kiasi cha
mauzo kinachozidi shilingi 4,000,000
|
Mauzo yanayozidi shilingi
7,500,000 lakini hayazidi shilingi 11,500,000
|
Shilingi
318,000
|
Shilingi 135,000 jumlisha
asilimia 3.8 ya kiasi cha mauzo kinachozidi Shilingi 7,500,000
|
Mauzo yanayozidi shilingi
11,500,000 lakini hayazidi shilingi 16,000,000
|
Shilingi
546,000
|
Shilingi
285,000 jumlisha asilimia 4.5 ya kiasi cha mauzo
kinachozidi Shilingi 11,500,000
|
Mauzo yanayozidi shilingi
16,000,000 lakini hayazidi shilingi 20,000,000
|
Shilingi
862,500
|
Shilingi
487,000 jumlisha asilimia 5.3 ya kiasi cha mauzo kinachozidi shilingi
16,000,000
|
Jedwali Na. 2: Viwango Vipya
vinavyopendekezwa kutozwa kodi kwa Wafanyabiashara wasiotengeneza Vitabu vya
Hesabu
Mauzo (Shilingi)
|
Kodi ya
kulipa kwa Mfanyabiashara asiye na Kumbukumbu kamili kwa mujibu wa kifungu
cha 35 cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi
|
Kodi ya
kulipa kwa Mfanyabiashara mwenye kumbukumbu kamili kwa mujibu wa kifungu cha
35 cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi
|
Mauzo yasiyozidi Shilingi 4,000,000
|
Hamna
|
Hamna
|
Mauzo yanayozidi shilingi 4,000,000 lakini hayazidi shilingi 7,000,000
|
Shilingi 100,000
|
Asilimia 3 kiasi cha mauzo kinachozidi shilingi 4,000,000.
|
Mauzo yanayozidi shilingi 7,000,000 lakini hayazidi shilingi 11,000,000
|
Shilingi 250,000
|
Shilingi 90,000 jumlisha asilimia 3 kiasi cha mauzo kinachozidi
Shilingi 7,000,000.
|
Mauzo yanayozidi shilingi 11,000,000 lakini hayazidi shilingi
14,000,000
|
Shilingi 450,000
|
Shilingi 230,000 jumlisha asilimia 3 ya kiasi cha mauzo kinachozidi
Shilingi 11,000,000
|
Mauzo yanayozidi shilingi
14,000,000 lakini hayazidi shilingi 100,000,000
|
Shilingi 450,000 jumlisha asilimia 3.5 ya
kiasi cha mauzo kinachozidi shilingi 14,000,000
|
|
|
|
|
Hatua hizi za Kodi ya Mapato kwa ujumla wake
zinatarajiwa kuongeza mapato ya
Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni
35,192.5
(c)
Sheria ya Ushuru wa
Bidhaa, SURA 147
42.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru
wa Bidhaa Kifungu cha 124(2), marekebisho ya viwango maalum vya Ushuru wa
Bidhaa (specific duty rates) kwa bidhaa zote zisizo za petroli yanaweza
kufanyika kila mwaka ili kuviwianisha na mfumuko wa bei na viashiria vingine
vya uchumi jumla. Kwa msingi huo wa sheria, napendekeza kutokufanya mabadiliko ya viwango maalum vya Ushuru wa
Bidhaa kwa bidhaa zote zisizo za petroli. Aidha, hatua hii inazingatia
kiwango kidogo cha mfumuko wa bei nchini na azma ya Serikali ya kujenga Uchumi
wa Viwanda, na hivyo kuhamasisha uwekezaji kwenye Sekta ya Viwanda, kuvilinda
na hatimaye kukuza ajira na mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa. Hata
hivyo, napendekeza kurekebisha Sheria ya Ushuru wa Bidhaa kwa bidhaa chache tu
kama ifuatavyo:-
(i)
Kupunguza Ushuru wa Bidhaa kwenye mvinyo uliotengenezwa kutokana
na usindikaji wa matunda (kama ndizi, mabibo, rozela/choya, nyanya, nk)
yanayozalishwa hapa nchini tofauti na zabibu kwa kiwango kinachozidi asilimia
75 kutoka shilingi 200 kwa lita hadi
shilingi 61 kwa lita ikiwa ni
punguzo la shilingi 139 kwa lita.
Lengo la hatua hii ni kuhamasisha ulipaji wa kodi wa hiari na pia kuvutia
uwekezaji kwenye viwanda vidogo vidogo vya aina hii. Aidha, bei ya mvinyo huu
kwa lita inafanana na bei ya vinywaji baridi;
(ii)
Kutoza Ushuru wa Bidhaa
wa asilimia 10 kwenye nywele za
bandia zinazotengenezwa ndani ya nchi na asilimia 25 kwenye nywele bandia zinazoagizwa kutoka nje ya nchi zinazotambuliwa
kwa HS Code 67.03; 67.04 na 05.01. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato ya
Serikali;
(iii)
Kusamehe Ushuru wa
Bidhaa kwenye vilainishi vya ndege (lubricants) vinavyoingizwa nchini na
Shirika la ndege la Taifa au mashirika ya ndege yanayotambulika katika mikataba
ya Kimataifa ya huduma za anga. Lengo la hatua hii ni kuiwezesha nchi yetu
kusaini mikataba ya Kimataifa ya Huduma za Anga ambayo ilishindikana kusainiwa
hapo awali kutokana na kutokuwepo kwa msamaha huo; na
(iv) Kutoza Ushuru wa Bidhaa wa asilimia 10
kwenye bidhaa za mabomba na vifaa vya plastiki vinavyotumika kwenye ujenzi wa
miradi ya ujenzi wa miundo mbinu ya maji kwa kuwa hivi sasa kuna viwanda vingi
vyenye uwezo wa kuzalisha bidhaa hizo na kutosheleza mahitaji hapa nchini.
Hatua hii inahusisha bidhaa za mabomba na plastiki zinazotambuliwa katika HS
Code 39.17. Lengo la kuanzisha Ushuru wa Bidhaa kwenye bidhaa hizo ni kulinda
viwanda na kuongeza fursa za kazi, ajira na mapato ya Serikali.
Hatua za Ushuru wa Bidhaa kwenye bidhaa
zisizo za petroli kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 2,955.50.
(d)
Sheria ya Usimamizi
wa Kodi, SURA 438
43.
Mheshimiwa Spika; napendekeza
kuongeza muda wa ziada wa miezi sita (6) hadi Disemba 2019 kwa walipa Kodi
waliokubaliwa kulipa kodi wanazodaiwa kwa utaratibu maalum wa kusamehe
malimbikizo ya nyuma ya riba na adhabu (Tax Amnesty on Interest and Penalties)
kwa asilimia 100 kwa kufanya marekebisho ya Kifungu cha 70 (2) cha Sheria ya
Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015 . Hatua hii inapendekezwa kutokana na muitikio
mzuri wa walipakodi wakati msamaha huo ulipotolewa mwezi Julai 2018 ambapo
dhamira ya Serikali ilikuwa ni kutoa ahueni kwa walipakodi waliokuwa na
malimbikizo makubwa yanayoathiri biashara zao.
Hatua
hiyo ya marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi inatarajiwa
kuongeza mapato ya Serikali kwa
kiasi cha shilingi milioni 367,000.
(e)
Sheria ya Usalama
Barabarani, SURA 168
44.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho kwenye Sheria ya Usalama Barabarani, Sura 168 kama ifuatavyo:-
(i)
Kuongeza muda wa Leseni
za udereva kutoka miaka mitatu (3) ya sasa hadi miaka mitano (5);
(ii)
Kuongeza tozo ya Leseni
ya udereva kutoka shilingi elfu arobaini (40,000) kwenda shilingi elfu sabini
(70,000); na
(iii)
Kuongeza ada ya kadi ya
usajili wa magari kutoka shilingi elfu kumi (10,000/=) hadi shilingi elfu
hamsini (50,000/=); pikipiki za matairi matatu kutoka shilingi elfu kumi (10,000/=) hadi shilingi
elfu thelathini (30,000/=) na pikipiki
kutoka shilingi elfu kumi (10,000/=) hadi shilingi elfu ishirini
(20,000/=).
Lengo la mapendekezo
haya ni kupunguza gharama za kuchapisha leseni kwa kipindi cha miaka mitatu
kwani leseni hizo zinaweza kudumu zaidi ya miaka mitano. Aidha, marekebisho
haya pia yanalenga katika kuoanisha gharama za uchapishaji wa leseni na kipindi
cha leseni husika.
Hatua hizi kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi
cha shilingi milioni 18,147.0
(f)
Sheria ya Forodha ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004
45.
Mheshimiwa Spika, kikao cha Mawaziri
wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki cha Maandalizi ya Bajeti (Pre-Budget
consultations of Ministers of Finance) kilichofanyika tarehe 3 Mei, 2019 mjini
Arusha, kilipendekeza kufanya marekebisho ya Viwango vya Ushuru wa Pamoja wa
Forodha (EAC – Common External Tariff “CET”) na Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC Customs Management Act, 2004) kwa Mwaka wa Fedha 2019/20.
Mapendekezo hayo yanalenga katika kuendeleza viwanda, kukuza ajira na kuboresha
maisha ya wananchi katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
46.
Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya
Mawaziri wa Fedha ya kufanya marekebisho kwenye Viwango vya Pamoja vya Ushuru
wa Forodha yanahusisha hatua mpya na zinazoendelea ambazo zimekuwa
zikitekelezwa katika mwaka 2018/19.
(i)
Mapendekezo ya hatua
mpya za viwango vya Ushuru wa Forodha ni kama ifuatavyo:-
(a)
Kupunguza
Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10
hadi asilimia 0 kwenye malighafi ya
kutengeneza taulo za watoto (Baby Diapers) zinazotengenezwa hapa nchini kwa
mwaka mmoja. Aidha, Watakaonufaika na punguzo hili ni viwanda vinavyozalisha
bidhaa hiyo hapa Tanzania na utaratibu utakaotumika katika kuagiza malighafi
hizo ni ule wa kuwapa unafuu wa Ushuru wa Forodha “Duty Remission”. Aidha, Serikali itaendelea kutoza ushuru wa
Forodha wa asilimia 25 kwa taulo za watoto (Baby Diapers) za kutoka nje ya
nchi. Hatua hii inatarajiwa kutoa unafuu wa gharama za uzalishaji, ajira na
mapato ya Serikali. Aidha ni matarajio ya Serikali kuwa viwanda vinavyonufaika
na msamaha huu wa Ushuru wa Forodha vitazalisha bidhaa hizi muhimu kwa afya ya
watoto na kuziuza kwa bei nafuu ili watanzania wengi waweze kuzinunua.
Malighafi zitakazohusika katika msamaha huu ni zile zinazotumbulika katika HS
Code 3506.91.00; PE Film HS Code 3926.90.90; Super Aborbent Polymer HS Code 3906.90.00;
Wet Strength Paper HS Code 4803.00.00; Non Wovens HS Code 5603.11.00;
Polyethylene Laminated Non Wovens HS Code 5903.90.00; Spandex HS Code
5402.44.00; na Dust Free Paper Hs Code 4803.00.00;
(b)
Kupunguza
Ushuru wa Forodha kutoka kiwango cha asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa
mwaka mmoja kwenye vifaa vinavyotumika katika kukata, kung’arisha na kuongeza
thamani ya madini ya vito. Hatua hii itawanufaisha wanaofanya shughuli hizo na
utaratibu wa “Duty Remission” ndio
utatumika katika kuagiza vifaa hivyo. Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu wa
gharama na kuhamasisha ukataji na usafishaji wa madini hayo hapa nchini na
hivyo kuongeza thamani yake kabla ya kuuzwa. Aidha, hatua hii itaongeza mapato
ya Serikali na ajira. Vifaa vitakavyohusika ni vile vinavyotambulika katika HS
Codes 3606.90.00; 6804.10.00; 6813.20.00; 7018.90.00; 7020.00.99; 8202.20.00;
8202.99.00; 8203.20.00; 8205.10.00; 8423.89.90;
8513.10.90; na 9002.19.00;
(c)
Kupunguza
Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10
hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja
kwenye makaratasi (HS Code 4805.11.00 na 4805.19.00) yanayotumika kama
malighafi ya kutengeneza vifungashio vya mboga mboga kwa ajili ya kuuza nje ya
nchi. Utaratibu wa “Duty Remission”
utatumika ambapo viwanda vinavyotengeneza vifungashio hivyo tu ndivyo
vitakavyonufaika. Lengo la kuondoa Ushuru wa Forodha kwenye malighafi hizo ni
kupunguza gharama ya utengenezaji wa vifungashio ili kulinda viwanda vya ndani
dhidi ya ushindani wa nje, kuvutia
uwekezaji katika uzalishaji wa vifungashio vya aina hii na hatimaye kuhamasisha
uuzaji nje wa mboga mboga kwa ajili ya kupata fedha za kigeni;
(d)
Kupunguza
Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25
hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja
kwenye vifungashio vya mbegu vinavyotumiwa na wazalishaji wa mbegu hapa nchini.
vifungashio vitakavyohusika ni vile vinavyotambulika katika HS codes
3923.29.00; 6305.10.00; 4819.40.00; 7310.29.90; 6305.33.00; 6305.20.00;
6304.91.90; 7607.19.90. Lengo la hatua hii ni kuongeza ubora wa mbegu na pia
kuzipa unafuu wa gharama Taasisi zinazozalisha mbegu hapa nchini. Aidha
utaratibu wa “Duty Remission”
utatumika katika kuagiza vifungashio hivyo;
(e)
Kupunguza
ushuru wa forodha kutoka asilimia 25
hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwa
utaratibu wa “Duty Remmission” kwenye
malighafi (Alluminium Alloys) zenye HS Code 7606.92.00 zinazotumika katika
kutengeneza sufuria (Alluminium pots). Hatua hii inalenga katika kupunguza
gharama za uzalishaji, kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu hapa
nchini, kulinda viwanda vya ndani ili viweze kuongeza uzalishaji wa kutosheleza
mahitaji na kuongeza ajira;
(f)
Ili
kulinda na kuhamasisha uzalishaji wa kahawa hapa nchini pamoja na kuongeza
mapato ya Serikali napendekeza kuongeza Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa
mwaka mmoja kwenye kahawa inayoagizwa nje ya nchi (HS Code 09.01);
(g)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 au
dola za kimarekani 125 kwa kila tani
moja ya ujazo (Metric ton) kwenye bidhaa za chuma kwa mwaka mmoja kutegemea
kiwango kipi ni kikubwa badala ya asilimia 10
pekee. Bidhaa hizo ni “Flat -rolled products
of iron or Non-alloy steel na Flat –rolled products of other alloy steel.” Bidhaa hizi hutambulika katika HS Codes
7209.16.00; 7209.17.00; 7209.18.00; 7209.26.00; 7209.27.00; 7209.28.00;
7209.90.00; 7211.23.00; 7211.90.00; 7225.50.0 na 7226.92.00. Lengo la kuweka
viwango hivyo vya Ushuru wa Forodha ni kudhibiti udanganyifu wa thamani halisi
ya bidhaa hizo na kulinda viwanda vya
hapa nchini na ajira;
(h)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au
dola za kimarekani 200 kwa kila tani
moja ya ujazo (Metric ton) kwenye bidhaa za mabati kwa mwaka mmoja kutegemea
kiwango kipi ni kikubwa badala ya asilimia 25
pekee. Ushuru huo unahusu bidhaa zinazotambulika katika HS Code 7212.30.00;
7212.40.00 na 7212.50,00. Hatua hii ina lengo la kulinda viwanda vya ndani kutokana
na udanganyifu wa thamani halisi ya bidhaa hizo zinapoingizwa kutoka nje
(under-invoicing and under valuation), na kulinda ajira na mapato ya Serikali;
(i)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 au
dola za kimarekani 250 kwa kila tani
moja ya ujazo (Metric ton) kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa
kwenye bidhaa za mabati zinazotambulika katika HS Code 7212.60.00 badala ya kutoza
ushuru wa asilimia 10 pekee. Lengo
la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani kutokana na udanganyifu wa thamani halisi
ya bidhaa hizo zinapoingizwa kutoka nje (under-invoicing and under valuation),
na kulinda ajira na mapato ya Serikali;
(j)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au
dola za kimarekani 250 kwa kila tani
moja ya ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za mabati kwa mwaka mmoja kutegemea
kiwango kipi ni kikubwa badala ya ushuru wa asilimia 25 pekee. Hatua hii inahusu bidhaa zinazotambulika katika HS codes
7210.41.00; 7210.49.00; 7210.61.00; 7210.69.00; 7210.70.00 na 7210.90.00. Lengo
la hatua hiyo ni kuwalinda wazalishaji wa bidhaa hizo hapa nchini kutokana na
ushindani wa nje;
(k)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au
dola za kimarekani 250 badala ya
kiwango cha asilimia 25 au dola za
kimarekani 200 kwa kila tani moja ya
ujazo (metric ton) kwenye bidhaa za chuma kwa mwaka mmoja kutegemea kiwango
kipi ni kikubwa kwenye nondo kwa mwaka mmoja. (Reinforment bars and hallow
profile). Hatua hii inahusu bidhaa zinazotambulika katika Hs codes 7213.10.00;
7213.20.00; 7213.99.00; 7214.10.00; 7214.20.00; 7214.30.00; 7214.90.00;
7214.99.00; 7215.10.00; 7215.50.00; 7215.90.00; 7225.90.00; 7225.92.00;
7225.99.00; 7306.30.00; 7306.50.00; 7306.61.00; 7306.69.00; na 7306.90.00.
Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vinavyozalisha nondo hapa nchini na
kuongeza ajira;
(l)
Kwa
kuwa mbogamboga zinalimwa kwa wingi hapa nchini, napendekeza kuongeza Ushuru wa
Forodha kutoka asilimia 25 hadi
asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye
bidhaa za mboga mboga (horticultural products) zinazotambulika kwenye HS codes
0603.11.00; 0603.12.00; 0603.13.00; 0603.14.00; 0603.19.00; 0604.20.00;
0604.90.00; 0701.90.00; 0702.00.00; 0703.10.00; 0703.20.00; 0706.10.00;
0710.10.00; 0710.21.00; 0710.22.00; 0710.30.00; 0714.10.00; 0714.20.00;
0804.30.00; 0804.40.00; 0804.50.00; 0805.10.00; 0805.40.00; 0805.50.00; 0806.10.00;
0807.11.00; 0807.20.00; 0808.10.00; 0808.20.00. Aidha, hatua hii itaongeza
mapato ya serikali; na
(m)
Kutoza
ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia 10
badala ya asilimia 0 kwa mwaka mmoja
kwenye bidhaa za fito za plastiki zijulikanazo kama PVC Profiles HS Code 3916.10.00; 3916.20.00; 3916.90.00 ambazo
hutumika kwa ajili ya kutengenezea fremu za milango, madirisha n.k. Lengo la
hatua hii ni kuongeza mapato ya Serikali.
(ii)
Mapendekezo ya
kuendelea na utekelezaji wa viwango vya Ushuru wa Forodha vya mwaka 2018/19 ni
kama ifuatavyo;-
(a)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 25
badala ya asilimia 0 kwa mwaka mmoja
kwenye karatasi zinazotambulika kwenye HS codes 4804.11.00; 4804.21.00;
4804.29.00; 4804.31.00 na 4804.41.00. Karatasi hizi ni zile zinazozalishwa na
kiwanda cha Mufindi;
(b)
Kupunguza
Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 35
hadi asilimia 10 kwa mwaka mmoja
kwenye ngano inayotambulika kwa HS Code 1001.99.00 na HS Code 1001.99.90. Hatua
hii imezingatia kwamba uzalishaji wa ngano katika Nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki hautoshelezi mahitaji, na bidhaa hii ni muhimu katika kutengeneza
vyakula mbalimbali. Lengo la Serikali ni kuwezesha Viwanda na walaji wa vyakula
vilivyotengenezwa kwa ngano waweze kupata vyakula husika kwa bei nafuu na
tulivu. Aidha utaratibu wa “Duty
Remission” utaendelea kutumika katika kuagiza ngano hiyo ambapo Viwanda
vinavyotumia ngano ya aina hii katika uzalishaji ndivyo vinavyohusika katika
kutumia kiwango hicho nafuu cha Ushuru wa Forodha. Kutokana na mahitaji makubwa
ya ngano katika Jumuia ya Afrika Mashariki na SADC, wakati umefika sasa kwa
wananchi kuchangamkia fursa ya Kulima ngano katika maeneo mbalimbali nchini
yanayofaa kwa kilimo cha ngano ikiwemo eneo la shamba la Basuto;
(c)
Kupunguza
Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye mashine za kielektroniki zinazotumika
kukusanya mapato ya Serikali (Electronic Fiscal Device) zinazotambulika katika
HS Code 8470.50.00;
(d)
Kupunguza
Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0
kwa mwaka mmoja kwenye bidhaa ijulikanayo kama “Printed Alluminium Barrier Laminates” (ABL) HS Code 3920.10.90
ambayo hutumika kama malighafi ya kutengeneza dawa ya meno kwenye viwanda vya
ndani;
(e)
Kupunguza
Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 10
hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwa
utaratibu wa “Duty Remission” kwenye
bidhaa ya kutengeneza sabuni ijulikanayo kama RBD Palm Stearin (HS Code
1511.90.40);
(f)
Kutoza
kwa mwaka mmoja Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 au dola za kimarekani 1.35
kwa kilo moja ya viberiti (safety matches) vnavyotambuliwa kwenye HS code
3605.00.00 kutegemea kiwango kipi ni kikubwa;
(g)
Kutoza
kwa mwaka mmoja Ushuru wa Forodha wa
asilimia 25 au dola za
kimarekani 350 kwa kila tani moja ya
ujazo (Metric ton) kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kwenye bidhaa za chuma za
misumari zinazotambulika katika HS code 7317.00.00 (nails, tacks, drawing pins,
corrugated nails, staples other than those of heading 83.05);
(h)
Kutoza
ushuru wa Forodha wa asilimia 35
badala ya asilimia 25 kwa mwaka
mmoja kwenye soseji (sausages) na bidhaa za aina hiyo (HS code 1601.00.00);
(i)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 35
badala ya asilimia 25 kwa mwaka
mmoja kwenye chingamu (chewing gum) zinazotambulika katika HS code 1704.10.00;
(j)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 35
badala ya asilimia 25 kwa mwaka
mmoja kwenye peremende (HS code 1704.90.00);
(k)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 35
badala ya asilimia 25 kwenye
chokoleti (chocolates) HS code 18.06 kwa mwaka mmoja;
(l)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 35
badala ya asilimia 25 kwenye biskuti
(HS code 1905) kwa mwaka mmoja;
(m)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 35
badala ya asilimia 25 kwa mwaka
mmoja kwenye nyanya zilizosindikwa (tomato sauces) zinazotambulika katika HS
code 2103.20.00;
(n)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 60
badala ya asilimia 25 kwa mwaka
mmoja kwenye maji (mineral water) yanayotambulika katika HS code 2201.10.00;
(o)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 35
badala ya asilimia 25 kwenye nyama
(meat and edible meat offal in chapter 2) kwa mwaka mmoja;
(p)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 25
kwenye mafuta Ghafi ya kula (mfano alizeti, mawese, soya, mizeituni, nazi,
karanga, mahindi n.k) kwa mwaka mmoja. Hatua hii inalenga katika kulinda na
kuhamasisha uzalishaji wa mbegu za mafuta na mafuta ya kula hapa nchini. Nchi
yetu ina fursa kubwa ya kukuza uzalishaji wa bidhaa hiyo. Hivyo, kuna umuhimu
wa kuchochea na kuhamashisha uzalishaji wa mbegu za mafuta na uchakataji wa
mafuta ghafi kwa kutumia mbegu zinazozalishwa hapa nchini. Lengo la hatua hii
ni kuongeza ajira mashambani, viwandani na pia kulinda fedha za kigeni
zinazotumika kuagiza mafuta hayo nje ya nchi. Mafuta ghafi hayo yanatambulika
kwenye HS code 1507.10.00; 1508.10.00; 1511.10.00; 1512.11.00; 1513.11.00;
1514.11.00; 1514.91.00; 1515.11.00; 1515.21.00; 1515.30.00;
(q)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 35
badala ya asilimia 25 kwa mwaka
mmoja kwenye mafuta ya kula yaliyochakatwa kwa kiwango cha mwisho
(semi-refined, refined/double refined oil) mfano alizeti, mawese, soya,
mizeituni, karanga, nazi, mahindi n.k. Ongezeko la Ushuru wa Forodha
linatarajiwa kuhamasisha uchakataji wa mbegu za mafuta hapa nchini na kuongeza
ajira viwandani na mashambani. Aidha ongezeko la Ushuru wa Forodha linahusu
mafuta yote ya kula yaliyochakatwa yanayoingizwa nchini na yanayotambulika
kwenye HS codes 1507.90.00; 1508.90.00; 1509.90.00; 1510.00.00; 1511.90.10;
1511.90.30; 1511.90.90; 1512.19.00; 1512.29.00; 1513.19.00; 1513.29.00;
1514.19.00; 1514.99.00; 1515.19.00; 1515.20.00; 1515.50.00; 1515.90.00;
(r)
Kutoza
Ushuru wa Forodha wa asilimia 10
badala ya asilimia 0 kwenye “Gypsum
Powder” HS code 2520.20.00 kwa mwaka mmoja;
(s)
Kupunguza
ushuru wa forodha kutoka asilimia 100
hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja
kwenye sukari ya matumizi ya kawaida (consumption sugar) inayoagizwa kutoka nje
ya nchi kwa vibali maalum kwa lengo la kuziba pengo (gap sugar) la uzalishaji
hapa nchini. Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani vinavyozalisha
sukari, ajira na mapato ya Serikali;
(t)
Kutoza
kwa mwaka mmoja Ushuru wa Forodha wa asilimia 35 kwenye mitumba inayoingia kutoka nje (badala ya asilimia 35 au dola za marekani 0.40 kwa kilo moja kutegemea kiwango
kipi kikubwa);
(u)
Kusamehe
Ushuru wa Forodha kwenye malighafi, vipuri na mashine vinavyotumika katika
kutengeneza nguo na viatu vya ngozi. Aidha, Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki wameridhia orodha iliyooanishwa (harmonized list) ya malighafi
na vipuri ili kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha na kuziwezesha nchi za Jumuiya
ya Afrika Mashariki ziweze kufanya biashara kwa bidhaa za nguo na viatu vya
ngozi vitakavyozalishwa ndani ya Jumuiya; na
(v)
Nchi
za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekubaliana kutoza Ushuru wa Mauzo nje (Export
Levy) wa asilimia 10 kwenye ngozi
iliyosindikwa kwa kiwango cha kati (wet blue). Lengo la hatua hii ni
kuhamasisha usindikaji wa ngozi, kuongeza thamani, na kuongeza ajira katika
nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
47.
Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha
wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya pia marekebisho
kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Management Act, 2004) kama ifuatavyo:-
(i)
Kufanya marekebisho
katika kipengele cha 1 (a) Sehemu B ya Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-CMA, 2004) ili kuingiza vilainishi kwa ajili
matengenezo ya ndege (Lubricants for Aircraft), sare (uniforms), kalenda,
shajara na peni kwenye orodha inayopata msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye
huduma za ndege. Lengo la kutoa msamaha huo ni kuiwezesha nchi yetu kusaini
mikataba ya Kimataifa ya Huduma za Anga ambayo haikuweza kusainiwa hapo awali
kutokana na kutokuwepo kwa msamaha huo.
Hatua hizi za Ushuru wa Forodha kwa pamoja
zinatarajiwa kuongeza mapato ya
Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni
31,074.0
(g)
Sheria ya Bajeti,
SURA 339
48.
Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha
utekelezaji wa Miradi Mikubwa yenye manufaa kwa Taifa kama vile Ujenzi wa
Miundombinu, Ununuzi wa Ndege, Mabehewa au Vichwa vya Treni, Miradi ya Umeme
n.k, inapendekezwa kurekebisha Kanuni ya 23 ya Kanuni za Sheria ya Bajeti za
mwaka 2015, ili kumpa Mamlaka Mlipaji Mkuu wa Serikali kuongeza muda wa
matumizi ya fedha za mwaka wa fedha uliomalizika hususan zinazohusu Miradi ya
Maendeleo. Hivi sasa Kanuni hii imeweka ukomo wa miezi mitatu (3) wa kutumia
fedha za mwaka wa fedha uliomalizika, ambapo baada ya muda huu wa miezi mitatu
(3) kuisha, fedha hizo hupaswa kurejeshwa Mfuko Mkuu wa Serikali. Utaratibu huu wa sasa wa kurejesha fedha za
miradi, Mfuko Mkuu wa Serikali baada ya kumalizika kwa muda wa miezi mitatu (3)
unaathiri utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kutokana na kutokuwepo kwa fedha
za kulipia Hati za Madai hadi hapo mgao mpya wa fedha utakapotolewa kwenye
bajeti ya mwaka mpya wa fedha.
(h)
Marekebisho madogo
madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi na Sheria nyingine mbalimbali.
49.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera katika sheria mbalimbali za
kodi pamoja na sheria nyingine ili ziwe sanjari na azma ya kurahisisha
utekelezaji wake. Marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa Sheria ya
Fedha ya mwaka 2019 na Matangazo ya Serikali (Government Notices).
(i)
Kuanza utekelezaji
wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa biashara (Blueprint) kwa
kurekebisha Ada na Tozo mbalimbali.
50.
Mheshimiwa Spika, kufuatia matokeo ya
mkutano wa Mh. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na wafanyabiashara kutoka
wilaya zote nchini uliofanyika ikulu, Dar es salaam, tarehe 7 Juni, 2019,
Serikali inapendekeza kufuta au kupunguza ada na tozo hamsini na nne (54) zinazotozwa na Wizara, Idara na taasisi
zinazojitegemea ili Kuondoa kero na urasimu kwa wafanyabiashara na kuboresha
mazingira ya biashara na uwekezaji. Hatua hizi ni sehemu ya kwanza ya
utekelezaji wa Mpango wa kuboresha Mfumo
wa udhibiti wa Biashara (Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the
Business Environment). Aidha, hatua
hii imelenga kuondoa muingiliano wa majukumu ya kiutendaji baina ya Wizara,
Taasisi na Mamlaka za Udhibiti. Marekebisho hayo yataainishwa katika Muswada wa
Sheria ya Fedha ya mwaka 2019 na Matangazo ya Serikali (Government Notices).
Marekebisho hayo yatajumuisha:-
I.
Mamlaka ya Dawa (TFDA)
(a)
Kufuta
tozo za Kushikilia usajili wa dawa za chanjo (Vaccines and Biologicals)
inayotozwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani mia hamsini (150); dawa za
mitishamba (Herbal medicines) inayotozwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani mia
hamsini (150); vifaa tiba (medical devices) inayotozwa kwa kiasi cha Dola za
Kimarekani mia moja (100); vitendanishi (diagnostics) inayotozwa kwa kiasi cha
Dola za Kimarekani mia mbili hamsini (250); chakula kinachotozwa kwa kiasi cha
Dola za Kimarekani mia moja (100); vipukusi (antiseptics and diagnostics) vinavyotozwa
kwa kiasi cha shilingi laki moja (100,000/=); na tozo za bidhaa
zinazotengenezwa ndani ya nchi (retention fees for domestic products);
(b)
Kufuta
tozo za Kudurufu cheti cha usajili wa vitendanishi inayotozwa kwa kiasi cha
Dola za Kimarekani mia moja (100);
(c)
Kufuta
tozo za ukaguzi wa maduka mapya ya kuuzia vyakula inayotozwa kwa kiasi cha
shilingi elfu hamsini (50,000);
(d)
Kufuta
tozo za usajili wa maduka ya reja reja ya dawa za mifugo kati ya shilingi elfu
hamsini (50,000/=) hadi shilingi laki moja (100,000/=);
(e)
kufuta
tozo ya ukaguzi wa viwanda vya samaki nchini iliyokuwa inatozwa kwa kiwango cha
kati ya shilingi laki mbili (200,000/=) hadi shilingi laki mbili na elfu
hamsini (250,000/=);
(f)
Kufuta
tozo ya ukaguzi wa maduka mapya ya samaki ya shilingi elfu hamsini (50,000/=);
na
(g)
Kufuta
tozo ya leseni ya mwaka ya biashara ya samaki kati ya shilingi elfu hamsini
(50,000/=) hadi shilingi laki tatu (300,000/=).
Lengo la hatua hizi ni kuweka mazingira
rafiki ya kibiashara na uwekezaji ili kuchochea uzingatiaji wa sheria kwa hiari
na kuongeza wigo wa wadau wanautumia huduma za TFDA (customer base).
Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 2,500.0
II.
Shirika la Viwango Tanzania
Napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya
Shirika la Viwango Tanzania kwa:-
(a)
Kufuta
tozo ya shilingi elfu hamsini (50,000/=) ya maombi ya alama ya ubora (TBS
mark);
(b)
Kufuta
tozo ya nembo ya ubora (TBS mark guarantee) ya asilimia kumi na tano (15) ya
tozo ya gharama za mwanzo za ukaguzi wa ubora (transport costs and overhead
fees);
(c)
Kufuta tozo ya dhamana ya cheti cha kutumia
nembo ya ubora (TBS mark licence). Tozo hii hutozwa kwa kiwango cha asilimia
hamsini (50) ya gharama za usafirishaji na upimaji wa Sampuli kutoka sokoni na
viwandani;
(d)
Kufuta
tozo ya shilingi elfu hamsini (50,000/=) ya ununuzi wa fomu ya maombi ya bidhaa
zinazotoka nje kwa bidhaa zote;
(e)
Kufuta
tozo ya gharama za ugenzi (calibration of equipment based on industrial metrology).
Tozo hii hutozwa kulingana na umbali wa sehemu (Kwa mfano Dar es salaam - chini
ya umbali wa kilometa 5 kutoka TBS ni
shilling elfu kumi (10,000/=); umbali wa kati ya kilometa 5 hadi 7 kutoka TBS
ni shilingi elfu hamsini (50,000/=); na umbali wa zaidi ya kilometa 7 kutoka
TBS ni shilingi laki moja (100,000/=); na
(f)
Kufuta
tozo ya asilimia 0.2 ya gharama ya mzigo na usafirishaji ya udhibiti wa
vipodozi, vifaa tiba ikiwa ni pamoja na kondomu, mabomba ya sindano (syringes),
glavu (gloves), pamba (cotton wool) na bendeji (bandage).
Lengo la hatua hii ni kupunguza mzigo kwa
wafanyabiashara na wazalishaji, kupunguza gharama katika uendeshaji wa vifaa
vya viwandani na kupunguza tozo za kero.
Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 2,687.4
Aidha, napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)
kwenye eneo la usimamizi wa viwango ambao unajumuisha ubora na usalama wa
chakula na vipondozi ili Shirika la Viwango Tanzania (TBS) liendelee kusimamia
eneo la chakula na vipodozi kwa ujumla kama ilivyo kuwa tangu mwaka 1975. Hivyo
basi, Shirika la Viwango litachukua jukumu la kuunganisha utaratibu wa usajili
wa majengo (premises registration), Usajili wa bidhaa (product registration),
udhibiti wa bidhaa (certification) na udhibiti wa bidhaa kutoka nje (import
inspection) kwa ujumla. Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) itaendelea kusimamia
madawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi ili kuongeza ufanisi katika eneo hili.
III.
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali
Napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya
Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Majumbani na Viwandani, Sura 182 kwa
kufuta tozo zifuatazo:-
(a)
Kufuta
tozo ya huduma ya kusitisha kibali cha awali na kutoa kibali kipya inayotozwa
kwa kiwango cha Dola za Kimarekani hamsini (50);
(b)
Kufuta
tozo ya huduma ya kubadilisha taarifa za kibali inayotozwa kwa kiwango cha Dola
za Kimarekani hamsini (50);
(c)
Kufuta
tozo ya usajili wa kampuni ya Wakala wa Forodha (Clearing Agent) inayotozwa kwa
kiwango cha Dola za Kimarekani mia tano (500) kila kipindi cha usajili;
(d)
Kufuta
tozo ya huduma ya kubadilisha taarifa za usajili inayotozwa kwa kiwango cha
Dola za Kimarekani mia moja (100) kila kipindi cha usajili;
(e)
Kufuta
tozo ya huduma ya ukaguzi wa dharura inayotozwa kwa kiwango cha Dola za
Kimarekani mia tatu (300) kwa kila ukaguzi;
(f)
Kufuta
ada ya kulinda cheti cha usajili
(maintenance fee) kwa viwanda vya magodoro inayotozwa kwa kiwango cha
Dola za Kimarekani elfu moja (1,000) kila mwaka;
(g)
Kufuta
ada ya kulinda cheti cha usajili kwa
viwanda vya rangi inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani elfu moja
(1,000) kwa mwaka;
(h)
Kufuta
ada ya kulinda cheti cha usajili kwa
viwanda vya nguo inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani elfu moja
(1,000) kwa mwaka;
(i)
Kufuta
ada ya kulinda cheti cha usajili kwa
viwanda vya ngozi inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani elfu moja
(1,000) kwa mwaka;
(j)
Kufuta
ada ya kulinda cheti cha usajili kwa
viwanda vya plastiki inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani elfu moja
(1,000) kwa mwaka;
(k)
Kufuta
ada ya kulinda cheti cha usajili kwa
viwanda vinginevyo vikubwa inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani elfu
moja (1,000) kwa mwaka;
(l)
Kufuta
ada ya kulinda cheti cha usajili kwa
viwanda vidogo vidogo inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani mia mbili
hamsini (250) kwa mwaka;
(m)
Kufuta
ada ya kulinda cheti cha usajili kwa
wasambazaji wakubwa inayotozwa kwa kiwango cha Dola za Kimarekani elfu moja
(1,000) kwa mwaka; na
(n)
Kufuta
ada ya kulinda cheti cha usajili kwa wasambazaji wa kati inayotozwa kwa kiwango
cha Dola za Kimarekani mia tano (500) kwa mwaka.
Aidha, napendekeza pia kufanya marekebisho ya Sheria ya Usimamizi na
udhibiti wa Kemikali za Majumbani na Viwandani Sura 182, ili kurekebisha
viwango vya tozo kama ifuatavyo:-
(a)
Kutoza
tozo ya shilingi elfu arobaini (40,000/=) ya usajili wa kemikali kwa kila
kemikali kwa kipindi cha usajili badala ya Dola za Kimarekani ishirini (20);
(b)
Kutoza
tozo ya shilingi laki mbili (200,000/=) kwa wafanyabiashara wakubwa na shilingi
elfu hamsini (50,000/=) kwa wajasiriamali wadogo kwa kila cheti cha usajili
(Certificate holder registration);
(c)
Kutoza
tozo ya shilingi laki mbili (200,000/=) badala ya Dola za Kimarekani mia moja
(100) kwa wafanya biashara wakubwa na shilingi elfu hamsini (50,000/=) kwa
wafanyabiashara wadogo kwa Usajili wa eneo la kuhifadhia kemikali (Premises
registration);
(d)
Kutoza
tozo ya shilingi laki tatu (300,000/=)
kwa siku kwa kila mtu ya kuchambua kemikali chakavu badala ya Dola za
Kimarekani mia tatu (300);
(e)
Kutoza
tozo ya shilingi laki mbili (200,000/=) ya kuainisha na kuidhinisha njia ya
kuteketeza kemikali badala ya Dola za Kimarekani mia tano (500);
(f)
Kutoza
tozo ya shilingi laki tatu (300,000/=) kwa kila siku kwa kila mtu ya kusimamia kupakia, kusafirisha, kushusha na
kuteketeza kemikali chakavu badala ya Dola za Kimarekani mia tatu (300);
(g)
Kutoza
tozo ya shilingi laki tatu (300,000/=) ya ukaguzi wa maghala na sehemu za
kuhifadhia kemikali badala ya Dola za Kimarekani mia mbili (200);
(h)
Kutoza
tozo ya shilingi laki moja na elfu hamsini (150,000/=) kwa kila siku kwa kila
mtu kwa tathmini ya njia za Usafirishaji
na ukaguzi wa dharura (Transportation Routes assessment and emergency
inspection) badala ya Dola za Kimarekani mia moja (100);
(i)
Kutoza
tozo ya shilingi laki moja na elfu hamsini (150,000/=) kwa siku kwa kila mtu
kwa kusindikiza kemikali hatarishi badala ya Dola za Kimarekani mia moja (100);
na
(j)
Usafirishaji
wa kemikali hatarishi na kemikali zingine ndani na nje ya nchi utatozwa tozo
kama zilivyoainishwa kwenye Jedwali Na. 3 hapa chini:-
Jedwali Na 3.
Kiasi cha kemikali kinachosafirishwa kwa MT
|
Ada
ya sasa
(USD)
|
Ada
inayopendekezwa
(USD)
|
Kati
ya 0.1 - 10
|
1-2 kila MT
|
10
|
10.1
- 200
|
1
kila MT
|
201
- 1000
|
400
|
1001
- 5000
|
600
|
5001
- 10,000
|
800
|
10,001-
20,000
|
1,200
|
20,001-
40,000
|
1,500
|
40,001+
|
2,000
|
Aidha, ili kutimiza matakwa ya sheria ya
kutumia fedha za kitanzania, tozo zote zilizokuwa zinatozwa kwa dola za
kimarekani zitatozwa kwa fedha za Kitanzania isipokuwa kwa shehena za kemikali
zinazoenda nje ya nchi (On-transit). Lengo la hatua hizi ni kupunguza wingi na
ukubwa wa tozo ili kuweka mazingira bora ya biashara nchini. Aidha, mizigo ya
kemikali inayopitishwa katika bandari ya Dar es salaam itaongezeka na hivyo
kuongeza mapato ya Serikali.
Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 450.0
IV.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi- Sekta ya Mifugo
Napendekeza kufuta tozo mbalimbali kwenye
Sekta ya mifugo kama ifuatavyo:-
(a)
Kufuta
tozo ya shilingi 5,000 ya vibali vya vyombo vya kusafirisha maziwa chini ya
lita 51;
(b)
Kufuta
tozo ya shilingi 50,000 ya usajili wa vituo vya kukusanyia maziwa lita 201 kwa
siku;
(c)
Kufuta
tozo ya shilingi 5,000 ya usajili wa wazalishaji wa maziwa chini ya lita 51 kwa
siku;
(d)
Kufuta
tozo ya shilingi 500,000 ya usajili wa wasambazaji wa pembejeo za maziwa;
(e)
Kufuta
tozo ya shilingi 15,000 ya usajili wa wafugaji wadogo wa mifugo ya nyama;
(f)
Kufuta
tozo ya shilingi 50,000 ya usajili wa wafugaji wa kati wa mifugo ya nyama;
(g)
Kufuta
tozo ya shilingi 75,000 ya usajili wa wafugaji wakubwa wa mifugo ya nyama;
(h)
Kufuta
tozo ya shilingi 20,000 ya usajili wa wasimamizi wa minada ya awali;
(i)
Kufuta
tozo ya shilingi 30,000 ya usajili wa wasimamizi wa minada ya upili na
mipakani;
(j)
Kufuta
tozo ya shilingi 50,000 ya usajili wa minada ya upili na mipakani;
(k)
Kufuta
tozo ya shilingi 30,000 ya usajili wa wafanyabiashara wa minada ya awali;
(l)
Kufuta
tozo ya shilingi 60,000 ya usajili wa
wafanyabiashara wa minada ya upili na mipakani;
(m)
Kufuta
tozo ya shilingi 100,000 ya usajili wa wafanyabiashara wa nyama na bidhaa zake
nje ya nchi;
(n)
Kufuta
tozo ya shilingi 1,000 ya kibali cha kusafirisha kuku nchini (vifaranga 100 kwa
siku moja); na
(o)
Kufuta
tozo ya shilingi 200 ya kibali cha kusafirisha kuku mkubwa nchini.
Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha takribani shilingi milioni 16,689.8
V.
Wizara ya Maliasili na Utalii
Napendekeza kufuta ada ya Leseni ya kufanya
biashara ya Utalii inayohusisha uwindaji wa kitaalamu (professional hunting)
iliyokuwa inatozwa kwa dola za kimarekani mia mbili (USD 200) kwa raia wa
Tanzania na dola za kimarekani elfu moja (USD 1000) kwa raia wa kigeni. Lengo
la hatua hii ni kupunguza tozo zinazotozwa katika sekta ya utalii, na kuvutia
watalii. Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha
takribani Dola za Kimarekani elfu themanini (USD 80,000).
VI.
Wizara ya Maji
Napendekeza kufuta ada ya matumizi ya maji
kwa watumiaji wenye visima nyumbani ambayo ilikuwa inatozwa kuanzia shilingi
laki moja (100,000/=) na kuendelea kulingana na matumizi ya maji. Lengo la
kufuta tozo hiyo ni kupunguza gharama kwa wananchi wanaochimba visima vya maji
kwa matumizi binafsi nyumbani na kuwezesha upatikanaji wa maji hayo kwa gharama
nafuu. Hata hivyo, ili kudhibiti uchimbaji holela wa visima, itabidi visima
hivyo viendelee kusajiliwa na Bodi za Maji za Mabonde.
Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 1,961
Aidha, Serikali itaendelea kufanya tathmini
ya utekelezaji wa mpango kazi wa Mpango
wa kuboresha Mfumo wa udhibiti wa Biashara (BLUEPRINT). Lengo ni kuendelea kuweka mazingira bora ya kuvutia
uwekezaji, katika kipindi cha muda wa kati na muda mrefu. Hatua hii inatoa
fursa kwa wajasiriamali kuanzisha biashara mpya zitakazo ongeza ajira na kukuza
uchumi. Kwa kuzingatia kuwa, Serikali imewekeza katika kuboresha mazingira ya
udhibiti wa mazingira ya biashara, kupitia mpango wa BLUEPRINT, hivyo basi, ni
matarajio na wito wa Serikali kwamba wawekezaji wa ndani na nje, watachangamkia
fursa hii kwa kuanzisha na kuendeleza uwekezaji mpya ili kukuza faida za
biashara na kuweza kulipa kodi stahiki kwa hiari na kuongeza mapato ya
Serikali.
(j)
Hatua za Kisera na
Kiutawala katika Kuboresha ukusanyaji wa mapato
51.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kuweka
utaratibu mpya wa kuondoa mizigo bandarini ambapo wananchi wa kawaida
wataruhusiwa kutoa mizigo yao bila ya kuwa na ulazima wa kutumia Wakala wa
Forodha (Clearing and Forwarding Agents). Hata hivyo, utaratibu huu
hautahusisha mizigo inayopitishwa hapa nchini kwenda nje ya nchi (Transit
Cargo). Aidha, Mamlaka ya Mapato Tanzania itaandaa utaratibu wenye kueleweka
kwa urahisi ili kuwawezesha Wananchi kugomboa mizigo yao kwa gharama nafuu
zaidi na bila kuchelewa.
52.
Mheshimiwa Spika, Serikali inapendekeza
kuchukua hatua mbalimbali za Kisera na Utawala kwa lengo la kuimarisha na
kurahisisha ukusanyaji mapato. Hatua hizo ni pamoja na:-
(i)
Ili kuondoa malalamiko
ya wafanyabiashara dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Serikali kupitia Wizara
ya Fedha na Mipango, imeamua kuanzisha kitengo huru cha kupokea malalamiko na
taarifa za kodi (Office of Tax Ombudsman) ambacho kitaratibiwa na Wizara ya
Fedha na Mipango. Aidha, kitengo hiki kitahusisha kupokea na kupitia malalamiko
ya taarifa za Kodi zitakazotolewa na walipakodi au watu wenye nia njema. Baadhi
ya majukumu ya Kitengo hiki ni kama yafuatayo:-
(a)
Kupokea
malalamiko ya rushwa dhidi ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania;
(b)
Kupokea
malalamiko ya ukadiriaji wa Kodi na uthamanishaji wa bidhaa usio wa haki wala
uhalisia dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania;
(c)
Kupokea
malalamiko ya matumizi ya nguvu katika ukusanyaji kodi dhidi ya Mamlaka ya
Mapato Tanzania;
(d)
Kupokea
malalamiko ya ufungaji wa biashara bila kufuata sheria na taratibu dhidi ya
Mamlaka ya Mapato Tanzania; na
(e)
Kupokea
malalamiko pamoja na kero nyingine zinazofanana na hayo dhidi ya Mamlaka ya
Mapato Tanzania.
(ii)
Ili kuongeza ukusanyaji
wa mapato ya kodi za ndani, serikali inakamilisha manunuzi ya mfumo unganishi
wa kielektroniki (Intergrated Domestic Revenue Adminstration System- IDRAS)
katika kukusanya kodi na mapato yasiyo ya kodi ili kuleta uwazi na ufanisi
katika ukusanyaji wa mapato. Pia mfumo huu utarahisisha ulipaji wa kodi na
kupunguza rushwa miongoni mwa watumishi wasio waaminifu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania;
(iii)
Kuendelea kusimamia
matumizi ya mfumo wa kukusanyia kodi wa
kielektroniki (Electronic Fiscal Device Management System) ambao umefanyiwa
maboresho makubwa na kuanza kazi tangu tarehe 1 June, 2019, ili kudhibiti na kubaini
udanganyifu unaofanywa katika matumizi ya mfumo huo. Aidha, hatua hii
itadhibiti uvujaji wa mapato katika urejeshaji wa kodi ( Tax refund), utoaji wa
risiti bandia, n.k;
(iv) Kutokana na wimbi la vijana wengi kujihusisha na michezo ya kubahatisha na
kusahau majukumu ya ujenzi wa taifa, Serikali ikishirikiana na Bodi ya Michezo
ya Kubahatisha imebuni na kutengeneza mfumo maalum ambao utatumika kudhibiti
uchezaji wa michezo hii (Responsible Gaming). Pia, Mfumo huu utatumika kudhibiti udanganyifu ambao
unafanywa na waendeshaji wa michezo ya kubahatisha ili Serikali ipate mapato
yake halali;
(v)
Kutokana na malalamiko
ya walipa kodi kuhusu ukadiriaji wa kodi na uthaminishaji wa bidhaa usio na
haki wala uhalisia, Serikali imeiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania kuanzisha
dawati la kushughulikia mapingamizi ya makadirio ya kodi ambapo pingamizi za
uthamanishaji na utambuzi litashughulikiwa ndani ya masaa ishirini na nne (24);
na
(vi) Kutoa unafuu wa kutolipa kodi kwa kipindi cha miezi sita (6) kuanzia wakati
mfanyabiashara au mwekezaji anapopewa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).
Hatua hii inatofautiana na hali ilivyo sasa ambapo mfanyabiashara anapopewa TIN
anaanza kufanyiwa tathmini (tax assessment) ya mapato yake ya biashara na
kutakiwa kulipa kodi. Hatua hii itawezesha wafanyabiashara na wawekezaji wapya
kupata muda wa kujiandaa na mahitaji yanayotakiwa katika shughuli wanazofanya
na kuondoa usumbufu au dhana ya woga wakati wa kuanzisha biashara. Mfano kuna
mahitaji ya Leseni ya biashara na vibali vingine muhimu.
(k)
Tarehe ya Kuanza
Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi.
53.
Mheshimiwa Spika, hatua hizi za kodi
zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2019, isipokuwa pale
ilipoelezwa vinginevyo.
V.
SURA YA BAJETI
KWA MWAKA 2019/20
54.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia shabaha, malengo pamoja na sera za
bajeti kwa mwaka 2019/20, Sura ya Bajeti inaonesha kuwa jumla ya shilingi
trilioni 33.11 zinatarajiwa
kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho. Jumla ya mapato ya ndani
(ikijumuisha mapato ya Halmashauri) yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 23.05,
sawa na asilimia 69.6 ya bajeti yote. Kati ya mapato hayo, Serikali inalenga
kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya shilingi trilioni 19.10 sawa na asilimia
12.9 ya Pato la Taifa. Mapato yasiyo ya kodi kwa mwaka 2019/20 yanatarajiwa
kuwa shilingi trilioni 3.18 na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri ni Shilingi
bilioni 765.5.
55.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 4.96 kutoka soko la ndani.
Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni
3.46 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na
kiasi cha Shilingi bilioni 1.50 sawa na asilimia 1.0 ya Pato la Taifa ni mikopo
mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Kwa lengo la kuongeza kasi
katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu, Serikali inatarajia kukopa shilingi
trilioni 2.32 kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara.
56.
Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia shilingi trilioni 2.78
ambayo ni asilimia 8 ya bajeti. Misaada na mikopo hii inajumuisha miradi ya
maendeleo shilingi trilioni 2.31; Mifuko ya Pamoja ya Kisekta shilingi bilioni
199.5; na Misaada na Mikopo nafuu ya Kibajeti (General Budget Support-GBS) shilingi
bilioni 272.8.
57.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20, Serikali inapanga kutumia
jumla ya shilingi trilioni 33.11 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha
hizo, shilingi trilioni 20.86 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwa
ni asilimia 63.0 ya bajeti, ikijumuisha Shilingi trilioni 9.72 kwa ajili ya
ulipaji wa deni la Serikali na shilingi trilioni 7.56 kwa ajili ya mishahara.
Aidha, shilingi trilioni 3.58 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (Other
Charges-OC) ikijumuisha shilingi bilioni 460.5 kwa ajili ya matumizi yatokanayo
na vyanzo vya ndani vya Halmashauri. Aidha, kwa mwaka 2019/20, Serikali imetenga
fedha kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 na maandalizi ya
uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
58.
Mheshimiwa Spika, matumizi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa shilingi
trilioni 12.25, sawa na asilimia 37.0 ya bajeti yote, ambapo kiasi cha Shilingi
trilioni 9.74 ni fedha za ndani na shilingi trilioni 2.51 ni fedha za nje. Kati
ya fedha za maendeleo zilizotengwa, shilingi trilioni 2.48 ni kwa ajili ya
mradi wa ujenzi wa reli kwa kiwango cha Standard
Gauge; shilingi trilioni 1.44 ni kwa ajili ya mradi wa kufua umeme Mto
Rufiji; shilingi bilioni 788.8 ni kwa ajili ya mifuko ya Reli, Maji na REA;
shilingi bilioni 450 ni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; na
shilingi bilioni 288.5 kwa ajili ya elimu msingi bila ada. Aidha, Serikali imetenga
jumla ya shilingi bilioni 600.0 kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya
watumishi, watoa huduma na makandarasi wa barabara, maji na umeme.
59.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mfumo wa bajeti
kama nilivyoeleza, sura ya bajeti kwa mwaka 2019/20 ni kama inavyooneshwa
katika Jedwali A.
Jedwali A: Mfumo wa Bajeti ya Mwaka 2019/20
Chanzo: Wizara ya Fedha na Mipango
VI.
HITIMISHO
60.
Mheshimiwa Spika, bajeti ni nyenzo ya
kufikia matarajio ya wananchi wetu. Hivyo, katika kuandaa bajeti hii, Serikali
iliwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo, Kamati ya Bunge ya Bajeti,
wafanyabiashara, taasisi za umma na binafsi, wananchi wa kawaida, na wataalam
wa kodi hususan wale walioshiriki vikao vya kazi vya kikosi kazi cha maboresho
ya kodi (Task Force and Think Tank)
kujadili na kushauri juu ya mapendekezo ya maboresho ya kodi na tozo
mbalimbali. Baadhi ya wadau walituletea maoni na ushauri kwa maandishi au barua
pepe. Nakiri kuwa walitupatia mrejesho ambao umesaidia kuboresha será na
vipaumbele vya nchi yetu kwa mwaka
2019/20 na siku zijazo. Napenda kwa niaba ya Serikali kuwashukuru sana kwa
michango hiyo mizuri ambayo tumejitahidi kuizingatia. Ni matarajio ya Serikali
kwamba wadau hao wataendelea kufanya hivyo katika mchakato wa bajeti
zitakazofuata.
61.
Mheshimiwa Spika, bajeti ya 2019/20 inahusu
kuendeleza juhudi za kujenga msingi wa uchumi wa viwanda ili kupanua fursa za
ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa na ustawi endelevu wa jamii na hatimaye kuondokana na umaskini, ujinga na
maradhi. Hususan, bajeti hii imelenga:
(i)
Kuimarisha na kujenga
miundombinu ya kisasa ili kuongeza uwezo wa Taifa katika uzalishaji viwandani
hasa vile vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi hapa nchini na kutoa
huduma bora (afya, elimu na maji) kwa wananchi. Aidha, miundombinu hiyo itasaidia
kuongeza biashara nchini, kikanda na kimataifa;
(ii)
Kujenga mazingira
mazuri ya kufanya biashara na uwekezaji kwa kushughulikia changamoto
zilizobainishwa katika mpango wa kuboresha mazingira ya biashara (Blueprint);
(iii)
Kuimarisha kilimo (uzalishaji
wenye tija na masoko ya mazao, ufugaji, uvuvi, na misitu) kwa kuzingatia
umuhimu mkubwa wa sekta hii katika uchumi wa Taifa (chakula, ajira, kipato cha
mwananchi, mchango katika fedha za kigeni na muunganiko wa sekta hii na
maendeleo ya viwanda);
(iv) Kudumisha amani na usalama katika Taifa; na Kujenga misingi ya Taifa
kujitegemea kiuchumi
62.
Mheshimiwa Spika, safari ya kuijenga
Tanzania mpya imeiva lakini haitakuwa rahisi hasa tukizingatia mabadiliko
yanayoendelea katika uchumi wa dunia, ushindani mkali wa kibiashara, mabadiliko
ya haraka ya teknolojia na demografÃa na changamoto zinazotokana na mabadiliko
ya tabianchi. Hata hivyo, bahati nzuri ni kuwa, katika historia ya nchi yetu,
Watanzania ni watu jasiri katika mapambano dhidi ya changamoto zinazojitokeza
na kila wakati zilipojitokeza tulizishinda
kwa kutumia ubunifu na nguvu ya umoja wa Watanzania.
63.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa tuko imara zaidi
chini ya uongozi shupavu wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Uchumi
wetu unaendelea kukua kwa kasi kubwa, ambapo mwaka 2018 ulikua kwa asilimia 7.0
na kiwango cha umaskini wa mahitaji ya
msingi kinazidi kupungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011/12 hadi asilimia 26.4
mwaka 2017/18. Naamini pasipo shaka yoyote kwamba kwa umoja wetu, uongozi
makini, kufanya kazi kwa bidii na kwa kutumia rasilimali za nchi yetu vizuri,
tutaijenga Tanzania mpya, ambayo itakuwa kitovu kikuu cha uchumi (Economic hub)
katika ukanda wa Afrika Mashariki katika muda usiozidi miongo miwili ijayo.
64.
Mheshimiwa Spika, ninapoelekea mwisho wa
hotuba hii, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru Washirika wetu wa Maendeleo
kwa misaada na mikopo nafuu wanayoendelea kutupatia katika kutekeleza miradi na
programu mbalimbali za maendeleo nchini. Katika bajeti ya mwaka 2019/20,
Washirika wa Maendeleo kwa pamoja wanatarajia kuchangia jumla ya shilingi
trilioni 2.78. Naomba niwatambue kwa kuwataja mmoja mmoja: Nikianza na nchi za Canada,
China, Denmark, Finland, India, Ireland, Italia, Japan, Korea ya Kusini,
Marekani, Norway, Poland, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, Ujerumani,
Uingereza, na Uswisi. Aidha, zipo taasisi za kimataifa ambazo ni: Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB), Benki ya Dunia, Arab Bank for Economic Development
in Afrika (BADEA), Global Fund, Kuwait Fund, Abu Dhabi Fund, Jumuiya ya Umoja
wa Ulaya (EU), Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB), OPEC Fund, Global
Environmental Facility (GEF), Shirika la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA),
Mfuko wa kukinga Hatari ya Kimazingira (GRMF), Climate Development Special
Fund, African Legal Support Facility (ALSF), Dignity, Global Agriculture and
Food Security Program (GAFSP),na Mashirika ya Umoja wa Mataifa yakiwemo UNICEF,
IFAD, UNDP, UNFPA, Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), na United Nations
Environment Programme (UNEP). Napenda pia kutambua uhusiano mzuri tulionao na
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Ni matarajio yetu kuwa misaada ya kiufundi
na fedha zilizoahidiwa na marafiki zetu hawa zitatolewa kwa wakati na kwa kiasi
kilichoahidiwa. Nasi kwa upande wa Serikali tunaahidi kutumia misaada hiyo kama
ilivyokusudiwa.
65.
Mheshimiwa Spika, napenda nitumie nafasi
hii kuwahimiza Waheshimiwa Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao na taasisi za kimataifa hapa nchini
Tanzania waongeze nguvu kukuza biashara kati ya nchi zao na nchi yetu na
kuhamasisha wenye mitaji toka nchi zao kuja kuwekeza hapa Tanzania. Tanzania ni
salama kwa uwekezaji wenye faida kwao na kwetu. Aidha, wafanye jitihada zaidi
kuhamasisha watalii kuja kujionea vivutio vya utalii, ambavyo ni fahari ya
Tanzania.
66.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya
Tano inatambua na kuthamini michango yao katika maendeleo ya Taifa letu ili
mradi isiambatane na masharti yanayohatarisha uhuru wa Tanzania (national
sovereignity), au kwenda kinyume na mila na desturi zetu. Hata pale ambapo
Serikali au mihimili mingine imefanya maamuzi ambayo hawakubaliani nayo, ni
vema na haki washirika wetu wa maendeleo watupe muda wa kuyatafakari na
kujadiliana nao kwa staha badala ya kuishinikiza Serikali ibadili uamuzi wake
ndipo watoe fedha, jambo ambalo halikubaliki hata kidogo.
67.
Mheshimiwa Spika, kwa Watanzania
wenzangu, napenda kuwasisitiza tuendelee kushikamana katika kuijenga Tanzania
mpya. Tuwe wazalendo na tena tukae macho daima kulinda na kutetea maslahi ya
Taifa letu. Tuongeze bidii kufanya kazi. Enzi za kutegemea wajomba hazipo tena
na habari njema ni kuwa: “Tukiamua Tunaweza” na Serikali ya CCM inayoongozwa na
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imethibitisha ukweli huo.
68.
Mheshimiwa Spika, naomba kwa niaba ya
Serikali kupongeza mchango mkubwa wa wafanyabiashara na wananchi wote ambao
wamelipa kodi kwa mujibu wa sheria. Aidha, napenda kutambua mchango adhimu wa mashirika
na taasisi ambazo Serikali ina hisa yaliyotoa gawio au asilimia 15 ya mapato
ghafi kuingia katika Mfuko Mkuu wa Hazina. Katika mwaka ujao wa fedha, Serikali
inayataka mashirika yote ya umma na taasisi ambazo Serikali ina hisa
kuhakikisha kuwa wanatoa gawio au mchango wa asilimia 15 ya mapato ghafi na
Msajili wa Hazina asimamie kikamilifu utekelezaji wa maagizo haya ya Serikali.
69.
Mheshimiwa Spika, kama mnavyofahamu,
mwezi Oktoba mwaka huu wa 2019 tutafanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Serikali kwa upande wake imejipanga kikamilifu katika maandalizi ikijumuisha
mahitaji ya kibajeti kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi huo. Ninawasihi wananchi
wote wenye sifa wajitokeze kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura. Aidha,
katika kuchagua viongozi wa ngazi hiyo, tafuteni Watanzania wenye sifa
zifuatazo:
(i)
Awe mchapakazi mwenye kujitoa
sadaka kuwatumikia watu, hasa wananchi wa kawaida;
(ii)
Awe mwepesi kuona, kusikiliza
na kuguswa na shida za wananchi wake. Tena awe jasiri katika kupigania haki za
wanyonge na awe na uwezo na ubunifu katika kutatua kero za wananchi hao;
(iii)
Awe mwadilifu, anayechukia na
kupiga vita rushwa na ufisadi kwa matendo;
(iv)
Anayetambua fursa zilizopo
katika eneo lake, kubuni mikakati ya kuwaendeleza wananchi anaowaongoza na
kuwatia watu wake hamasa ya kuthubutu kutumia fursa hizo;
(v)
Awe mtetezi hodari wa kulinda
mazingira na mpambanaji dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi;
(vi)
Mwenye kutoabudu nyadhifa;
anayetambua kuwa nafasi na vyeo tulivyopewa ni vya muda tu. Ni vya kupita!
Thamani halisi ya kiongozi ni kufanya kazi kwa bidii na kuacha kumbukumbu nzuri
kwa ustawi wa eneo analoliongoza na Taifa kwa ujumla;
(vii)
Awe kama mchezaji mzuri wa
kiungo katika timu ya ushindi, anayetambua kwamba mkono mmoja hauwezi kupiga
makofi ya shangwe;
(viii) Awe mwenye
kutambua kwamba kazi za kiongozi zina maana sana kwa kuwa zinamwezesha kubadilisha
maisha ya maelfu ya Watanzania, hasa wanyonge, kuwa bora zaidi;
(ix)
Awe na uwezo wa kuwaeleza
wananchi kinaganaga kuhusu Serikali yao inawapeleka wapi na wajibu wa kila
mmoja ili waendelee kuiunga mkono; na
(x)
Awe anatoka ndani ya chama cha
siasa kinachotetea maslahi na haki za wanyonge na chama hicho ni CCM!
Naomba nikiri kuwa, sifa hizi nilizozitaja nimeziazima kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila ridhaa
yake!
70.
Mheshimiwa Spika, nawaomba viongozi wote
wa dini pamoja na waumini wote kila mmoja kwa imani yake, tuendelee kumwombea
Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ili Mwenyezi Mungu
aendelee kumjalia afya njema, hekima, busara na kumwongoza kwa kila jambo
alifanyalo kuliletea Taifa letu maendeleo.
71.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuwashukuru viongozi
wenzangu wa Wizara ya Fedha na Mipango, ambao wamekuwa msaada mkubwa katika
utekelezaji wa majukumu ya Wizara na maandalizi na uratibu wa bajeti hii ya Watanzania.
Kipekee ninawashukuru Mheshimiwa Dkt. Ashatu K. Kijaji, Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango ambaye ni Mbunge mahiri wa Jimbo la Kondoa; Katibu Mkuu HAZINA na
Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bwana Doto M. James, pamoja na Naibu Makatibu Wakuu,
Bi. Amina Kh. Shaaban, Dkt. Khatibu M.
Kazungu na Bwana Adolf H. Ndunguru pamoja na watumishi wa ngazi zote wa Wizara
ya Fedha na Mipango. Vile vile, ninamshukuru Profesa Florens D. Luoga, Gavana
wa Benki Kuu ya Tanzania pamoja na Naibu Gavana Dkt. Yamungu Kayandabila, Dkt.
Bernard Kibesse na Bwana Julian Raphael Banzi kwa kusimamia vema sekta nyeti ya
fedha. Kwa nafasi ya kipekee, napenda nimpongeze Dkt. Edwin Mhede kwa kuteuliwa
na Rais kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Ni matumaini
yangu na ya Watanzania kuwa atakuwa chachu ya kujenga taswira mpya ya TRA
itakayoongeza mapato ya Serikali bila manyanyaso kwa wafanya biashara.
72.
Mheshimiwa Spika, ninawashukuru viongozi na watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ofisi ya Msajili wa Hazina na Ofisi ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yao.
Nawashukuru Wakuu wote wa Idara na Vitengo, Taasisi na Wakala za Serikali
zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na wafanyakazi wake wote kwa
kazi nzuri wanazofanya na kuendelea kunipa ushirikiano wa dhati katika kutekeleza majukumu ya Wizara kwa
ufanisi wa hali ya juu.
73.
Mheshimiwa Spika, niwashukuru pia
wananchi wenzangu wa Wilaya ya Buhigwe na
mkoa wetu wa Kigoma ambao
walinilea na kunifundisha kufanya kazi. Mwisho kabisa naishukuru familia yangu,
hususan mke wangu mpenzi na rafiki yangu Mbonimpaye, watoto, wajukuu, ndugu,
jamaa na marafiki zetu wote tuliopewa na Mungu. Asanteni kwa kuniombea msaada
wa Mungu katika kazi hii, usiku na mchana. Nami ninasema kwa kila mmoja wao:
“Bwana akubarikie na kukulinda,
Bwana akuangazie nuru za uso wake, na
kukufadhili,
Bwana akuinulie uso wake, na kukupa amani”
Hesabu 6: 24-26.
Nimalizie kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa baraka
zake na kuniwezesha kuwasilisha hotuba hii. Aidha, apende kuendelea kunijalia
uwezo na unyenyekevu wa kulitumikia Taifa letu na wananchi wake kwa uadilifu. Asanteni
sana Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa kunisikiliza.
MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA
74.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
|
0 Comments