habari Mpya


‘’Halmashauri Nchini Zaagizwa Kutenga Maeneo ya Michezo’’ –Waziri Mkuu Majaliwa.

Wanamichezo kutoka Mkoa wa Simuyu wakiingia kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona kushiriki katika Ufunguzi wa Michezo ya UMISETA uliofanywa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Juni 10, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wachezaji wa timu ya soka  mkoa wa Tanga wakati alipofungua mashindano ya UMISETA kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara Juni 10, 2019. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa timu ya soka ya mkoa wa Mtwara wakati alipofungua mshindano ya UMISETA  kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara Juni 10, 2019 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameagiza halmashauri zote za majiji na miji zihakikishe kuwa kuanzia sasa zinatenga maeneo ya michezo na burudani kila zinapopima viwanja.

Naagiza kuanzia sasa, maeneo yote yanayopimwa na halmashauri na miji yote nchini, lazima yazingatie uwepo wa maeneo ya michezo na burudani,” amesisitiza Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo (Jumatatu, Juni 10, 2019) wakati akifungua mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa shule za msingi na sekondari Tanzania UMISETA, katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

 Zaidi ya wanafunzi 5,400 wanashiriki mashindano hayo.

Pia, amezitaka Halmashauri ziweke mpango madhubuti wa kuyaendeleza maeneo ya michezo na burudani sambamba na miundombinu inayozingatia mahitaji ya wote bila kubagua.

Hivyo, Waziri Mkuu ameagiza yafanyike marekebisho na hatua za haraka ili kutoa fursa ya ukuaji wa michezo na kusaidia wananchi kushiriki michezo, mazoezi na kupata burudani.

Amesema ifikapo Septemba 30, 2019, kila halmashauri iwe imefanya mapitio ya maeneo yote yaliyokuwa yamepimwa kwa matumizi ya huduma maalum ikiwemo michezo, burudani, shule na ibada na kutoa taarifa kama yanatumika kwa ajili hiyo au vinginevyo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia irudishe na iimarishe mchepuo wa Elimu kwa Michezo Chuo cha Ualimu Butimba ili kupata wataalam zaidi.

Halmashauri ziendelee kuwaruhusu walimu mbalimbali nchini kuhudhuria mafunzo ya michezo katika chuo cha Mendeleo ya Michezo Malya ili kupunguza uhaba wa watalaam wa michezo katika shule mbalimbali na nchini kwa ujumla.”

Waziri Mkuu amesema michezo ni muhimu kwa wanafunzi kwa kuwa itawaepusha vijana na makundi yasiyofaa yakiwemo matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vingine visivyoendana na maadili ya Kitanzania,kuwa na afya bora na kufanya vema katika masomo yao kwa kuwa ili waweze kusoma vema ni sharti afya zao ziwe njema. Pia sanaa itasaidia katika kuutambulisha utamaduni wetu ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu.

“Tangu tumerejesha shughuli za michezo katika shule zetu tumekuwa na mafanikio makubwa sana ikiwemo kupata wachezaji wanaofuzu kucheza soka la kulipwa kwenye viwango vya kimataifa kama Mbwana Samatta (Genk –Belgium), Simon Msuva (Difaa El Jadid – Morocco), “

Wengine ni Shiza Kichuya (Enppi –Misri), Thomas Ulimwengu (JS Saoura – Algeria), Hamid Mao (Petrojet – Misri), Adi Yusuph (Blackpool –England), Hassan Kessy (Nkana – Zambia), Yahya Zaydi (Ismaily –Misri), Shabani Chilunda, (Tenerife – Hispania) Rashid Mandawa (BDF- Botswana), Farid Mussa ( Tenerife– Hispania).

Waziri Mkuu amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, jitihada zaidi zinahitajika ili kuwa na maendeleo ya kutosha katika shughuli za michezo nchini.

Hivyo, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais TAMISEMI wakamilishe tathmini ya shule 56 za Serikali zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza vipaji vya michezo.

Ufunguzi huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Selemani Jafo, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, Maafisa Elimu kutoka mikoa yote nchini, walimu wa michezo pamoja na Maofisa wengine wa Serika

Post a Comment

0 Comments