habari Mpya


Waziri Jafo: "Mganga mkuu wa mkoa wa Kagera hakikisha unatoa kibali, zahanati ya Murulama ianze kufanya kazi".

Na Auleria Gabriel
Waziri wa nchi ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Suleiman Jafo, amemuagiza mganga mkuu wa mkoa wa Kagera Dakt. Marco Mbata kufika katika zahanati ya kijiji cha Murulama kata ya Bukiriro wilayani Ngara na kuifanyia tathmini kisha kutoa kibali cha kuanza kutumika ili wakaazi wa kijiji hicho wanufaike na huduma za afya karibu.

Jafo ametoa maagizo hayo leo Aprili 09, 2019 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Ngara Alex Rafael Gashaza aliyeuliza kama wizara ya Afya inaweza kutoa kibali ili zahanati hiyo ianze kutoa huduma kwa wananchi.


‘Mhe. Mwenyekiti kwanza kwa kauli yako naomba nimuagize mganga mkuu wetu wa mkoa wa Kagera aende akafanye ufuatiliaji wa Zahanati hiyo kama imekamilika kweli lazima ahakikishe nguzu za wananchi ambao lengo lao ni kupata huduma, kwahiyo namuagiza mganga mkuu wa mkoa wa Kagera aende akafanyie kazi ili upate kibali wananchi wapate huduma.’ Alisema Jafo
Mbunge Gashaza alisema zahanati ya Murulama ina takriban miaka miwili imekamilika lakini haijaanza kutoa huduma kutokana na kutokuwepo kwa nyumba ya watumishi pamoja na choo


‘Nashukuru Mhe. Mwenyekiti kunipa nafasi hii kuuliza swali la Nyongeza, kwakuwa ipo zahanati ya Kigarama ambayo jengo la OPD limejengwa kwa nguvu za wananchi mpaka kukamilika lakini zahanati hiyo takriban miaka miwili haijaweza kufanya kazi kwa sababu hakuna nyumba ya watumishi na choo hakijakamilika, lakini upo uwezekano wa kupata nyumba ya kupanga kwenye senta hiyo ambapo ni rahisi mganga kuweza kuhudumia akitokea hapo. Je, wizara iko tayari kutoa kibali ili zahanati hiyo iweze kufunguliwa na kuondoa adha ya akina mama wanaoenda kujifungua kwa kutembea umbali mrefu zaidi ya kilomita 30 wakati tayari wameshatoa mchango kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo?’ Alihoji Mbunge Alex Gashaza

Background

Kutolewa kwa maagizo haya ni mafanikio yaliyopatikana kutokana na Redio Kwizera kupitia kipindi cha ‘Afya yako Haki yako’ kilichorushwa April 03, 2019 kufuatilia uwepo wa zahanati hiyo iliyojengwa tangu mwaka 2013 na kukamilika mwaka 2016 kushindwa kufunguliwa na kutoa huduma kwa wananchi licha ya wananchi kutoa michango kwa ajili ya kupata huduma za matibabu karibu.
Kupitia kipindi hicho wananchi pamoja na viongozi wa kijiji cha Murulama hasa wa kitongoji cha Kigarama ilipojengwa zahanati hiyo, walilalamikia serikali kushindwa kuthamini juhudi walizozionyesha katika kusogeza huduma za afya karibu na maeneo yao kupitia michango waliyoitoa licha ya maisha magumu waliyonayo
 


Awali alipoulizwa juu ya zahanati hiyo, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ngara Aidan John Bahama alieleza kwamba halmashauri haiwezi kutoa hata shilingi kupeleka kijiji cha Murulama ili kusaidia ujenzi wa nyumba ya watumishi mpaka waanzishe wenyewe ujenzi huo licha ya kwamba wameshajitolea kukamilisha jengo la zahanati.


Sera ya afya ya mwaka 2007, Katika ukurasa wake wa 22 tamko la sera linasema, Serikali itaendelea kusogeza huduma za afya karibu na wananchi kwa kuwa na zahanati kwa kila kijiji, kituo cha afya kwa kila kata na hospitali kwa kila wilaya, hospitali ya rufaa kila mkoa na hospitali maalum ngazi ya taifa kwa kushirikiana na wananchi na wadau wote kwa ujumla.
Picha na Maktaba


 

Post a Comment

0 Comments