habari Mpya


TANAPA yawapa Zahanati Wananchi Ikuza wilayani Muleba.

Na: Sylvester Raphael

Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) yaikabidhi Serikali mradi wa ujenzi wa Zahanati uliojengwa kwa ushirikiano kati ya TANAPA, Halmashauri ya Wilaya ya Muleba na Wananchi wa Kijiji cha Ikuza kilichopo Kisiwani Ikuza ambapo mradi huo uligharimu kiasi cha shilingi milioni 280,953,625/= hadi kukamilika kwa hatua ya kwanza ya ujenzi wa vyumba kumi na moja vya vyakutolea huduma.

 Akikabidhi Zahati hiyo Aprili 16, 2019 Naibu Kamishina Mkuu wa TANAPA Bw. Martin Leboki aiyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu TANAPA Taifa Bw. Alani Kijazi alimweleza Mkuu wa Mkoa wa Kagera na wananchi waliohudhuria hafla fupi ya makabidhiano kuwa zahanati hiyo imejengwa na kukamilika kwa ushirikiano mkubwa kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Muleba na wananchi wa kijiji cha Ikuza kutokana na ujirani mwema wa Hifadhi ya Taifa ya Rubondo.

Bw. Leboki alisema kuwa TANAPA ilitoa jumla ya shilingi milioni 144,725,675/= katika ujenzi wa zahanati hiyo yenye vyumba kumi na moja na kununua vifaa tiba kama vitanda vya wagonjwa, vitanda vya akinamama wajawazito kujifungulia pamoja na samani nyingine zitakazotumika katika zahanati hiyo. 

Aidha Halmashauri ya Wilaya ya Muleba ilichangia jumla ya shilingi milioni 124,392,340/= na wananchi walichangia jumla ya shilingi milioni 14,535,000/=

Pamoja na kukamilika kwa zahanati hiyo ya Kijiji Ikuza lakini wananchi walibainisha kuwa bado kuna changamoto ya kutokuwa na shimo la kutupia kondo la nyuma, upatikanaji wa umeme na maji katika zahanati hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti akipokea zahanati ya Kijiji Ikuza kwa niaba ya Serikali aliishukuru TANAPA kwa kushirikiana na wananchi wa Ikuza na kuwajengea Zahanati ya kuwahudumia na kuwaondolea changamoto ya upatikanaji wa huduma ya afya katika kisiwani humo pamoja na visiwa vya jirani.

Aidha, Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano katika mkoa wa Kagera imejenga Vituo vya Afya 14 kwa gharama ya shilingi bilioni 6.9 na tayari imeto shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya . “Pamoja na juhudi hizo zote kufanyika lakini uhuhitaji katika vijiji ni mkubwa na kama hatutajenga zahanati kama hizi mlundikano katika Vituo vya Afya utakuwa mkubwa mno.” Alisisitiza Mhe. Gaguti.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa Gaguti alitoa maagizo kuwa zahanati hiyo inatakiwa kuanza kutoa huduma mara moja isikae tena mwaka bila kutoa huduma kwa wananchi. 

Kuhusu changamoto za wananchi juu ya shimo la kondo la nyuma alitoa mifuko 50 ya saruji ili shimo hilo lianze kujengwa kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji cha Ikuza.
Kuhusu umeme, Mkuu wa Mkoa Gaguti alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Bw. Emannuel Shelembi kufunga mara moja solar ambayo tayari ipo katika ofisi za Halmashauri pia kuhakikisha Mkurugenzi huyo anaandaa watumishi wa kwenda kutoa huduma katika zahanati hiyo. Na kuhusu suala la maji aliwahakikishia wananchi kuwa atatoa Sim tank ya lita 5000 na wao wachimbe mtaro kutokea ziwani ili maji yapatikane kwa haraka.
 
Mwisho, Mkuu wa Mkoa Gaguti aliwashukuru TANAPA kwa kuendelea kudumisha ujirani mwema na wananchi wanaopakana na Hifadhi za Taifa ambapo alimshukuru tena Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Taifa kwa kumkubalia kushirikiana naye kujenga Zahanati katika vijiji vinavyopakana na Mapori yaliypandishwa hadhi na kuwa hifadhi za Taifa za Biharamulo Burigi na Kimisi, Ibanda na Rumanyika.
Naye diwani wa Kata ya Ikuza Mhe. Fortunatus Wazia Matta aliishukuru TANAPA na Serikali kwa kuwasogezea karibu wananchi huduma ya afya kwani alisema kuwa tangu alipochaguliwa kuwa diwani wa kata ya Ikuza mwaka 2010 hadi sasa wakina mama wajawazito wanne tayari wamepoteza maisha yao kutokana na changamoto ya afya katika kata hiyo iliyopo visiwani.

Post a Comment

0 Comments