habari Mpya


Mwenge wa Uhuru 2019 Waanza Mbio Zake Mkoani Kagera Leo April 24.

Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti akizungumza na Wanahabari Ofisini kwake April 23,2019. 

Mkoa wa Kagera leo April 24,2019 unaupokea Mwenge wa Uhuru 2019 katika eneo la Murusagamba wilayani Ngara mpakani mwa Mkoa wa Kigoma na Kagera na baadae Mwenge huo wa Uhuru utaanza mbio zake katika mkoa wa Kagera katika Wilaya ya Ngara.

Mwenge wa Uhuru 2019 ukikimbizwa Mkoani Kagera unatarajiwa kuzindua, kuweka Mawe ya Msingi, na Kukagua miradi ya maendeleo jumla 74 yenye thamani ya shilingi bilioni 18,894,323,585.90.

Katika fedha hizo, Serikali Kuu imechangia shilingi bilioni 10,262,407,160.86 sawa na asilimia 54.31%. Halmashauri za Wilaya na Manispaa ya Bukoba zimechangia shilingi milioni 282,853,162.91 sawa na asilimia 1.5%. Wahisani wamechangia shilingi bilioni 2,472,529,017.96 sawa na asilimia 13.09%. huku Wananchi wakichangia shilingi bilioni 5,876,534,244.17 sawa na asilimia 31.10%.

Miradi 74 ya Maendeleo katika sekta za Afya, Elimu, Maji, Kilimo, Barabara, Ujasiliamali kwa Watu wenye ulemavu Vijana na Wananwake, Viwanda, Mapambano dhidi ya Rushwa na Madawa ya Kulevya itatembelewa, kukaguliwa, kuzinduliwa na Kuwekewa Mawe ya Msingi na Mwenge wa Uhuru Mkoani Kagera.

Aidha, Miradi 21 itazinduliwa, Miradi 12 itawekewa Mawe ya Msingi, na Miradi 38 itatembelewa na kukaguliwa na Mwenge wa Uhuru ikiwemo miradi 3 ambayo ni ya shughuli nyinginezo.

Aidha, Kauli Mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu 2019 ni “Maji ni Haki ya Kila Mtu, Tutunze Vyanzo Vyake na Tukumbuke Kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Marco Gaguti anatoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Kagera kujitokeza kwa wingi wakati wa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru 2019 Kimkoa katika eneo la Murusagamba Wilayani Ngara tarehe 24 Aprili, 2019 na utakimbizwa katika Halmashauri za Wilaya zote za Mkoa wa Kagera ukianzia Ngara, Karagwe, Kyerwa, Missenyi, Bukoba Manispaa, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Muleba na utahitimisha mbio zake katika Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo Mei Mosi, 2019

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti nitaukabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita tarehe 2 Mei, 2019.

Mwenge wa Uhuru karibu Mkoani Kagera ewe mwananchi shiriki katika mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019, “Maji ni Haki ya Kila Mtu, Tutunze Vyanzo Vyake na Tukumbuke Kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”.

Imetolewa na; Sylvester M. Raphael
Afisa Habari wa Mkoa
KAGERA
23 Aprili, 2019

Post a Comment

0 Comments