
Na Mwandishi Wetu, MAELEZO.
RAIS
Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali haina mpango wa kuongeza
maeneo ya utawala ikiwemo kuanzisha mikoa mipya na badala yake
imejipanga kuimarisha huduma na mahitaji ya miundombinu iliyopo ili
kuwaletea maendeleo wananchi.
Akizungumza
katika hafla ya uzinduzi wa barabara ya
Namtumbo-Kilimasera-Matemanga-Tunduru yenye urefu wa kilometa 193
(Ijumaa April 5, 2019), Rais Magufuli alisema Serikali imekusudia
kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi ikiwemo ujenzi wa
miundombinu ya barabara, afya, maji, elimu n.k katika maeneo waliopo.
Aliongeza
kuwa katika awamu yake yake ya Uongozi, suala la kuongeza maeneo ya
utawala halipo na badala yake kuwataka Viongozi wa maeneo hayo wajipange
katika kuwaletea maendeleo wananchi badala ya fedha zilizopo kwenda
katika kujenga ofisi mpya za Wakuu wa Mikoa mipya na kuwalipa mishahara
viongozi hao.
“Tumepanga
kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wetu, tumechelewa kuleta
Maendeleo hususani kwa wananchi wetu wa mikoa ya kusini, Serikali
ninayoiongoza haina mpango wa kuanzisha mikoa mipya , badala yake pesa
hizo tutazielekeza katika ununuzi wa madawa na kuboresha miundombinu ya
barabara, elimu na nishati’ alisema Rais Magufuli.
Aidha
Rais Magufuli alisema bado yapo baadhi ya maeneo mengi nchini
yanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo barabara za lami, hivyo
Serikali haitoweza kuleta Maendeleo katika sehemu moja kwa kuwa fedha
hizo hazipo kwa kuwa ina na mahitaji makubwa katika kuboresha huduma
mbalimbali za kijamii na kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Kwa
mujibu wa Rais Magufuli alisema malengo ya Serikali ni kuhakikisha kuwa
huduma muhimu na za msingi kwa Maendeleo ya wananchi zinapewa
kipaumbele ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na Zahanati, kwa kuwa
kukamilika kwake kutasaidia kupunguza vifo vya akina mama na watoto
ambavyo katika miaka ya nyuma vimekuwa vikisababisha vifo vya makundi
hayo ya kijamii.
Akizumgumzia
kuhusu Sekta ya Maji, Rais Magufuli alimtaka Waziri wa Maji, Prof.
Makame Mbarawa kuwasimamia wakandarasi wa miradi ya maji nchini, kwani
Serikali imekuwa ikitenga kiasi kikubwa cha cha fedha katika miradi ya
Maendeleo pasipo na kupata matokeo yaliyotarajiwa, na hivyo
kuisababishia hasara Serikali.
“Kwa
mujibu wa ripoti ya Wizara ya Fedha na Mipango, miradi mingi ya maji
imekuwa ikitumia fedha nyingi pasipo na kupata matokeo yoyote na
wataalamu wetu hasa wakandarasi wamekuwa wazito kutoa tafsiri za
nadharia za utaalamu na kuzileta katika nadharia halisi, na mataifa ya
nje yanashangwa tunaposhindwa kuvitumia vyanzo tulivyonazo ili kuweza
kuzalisha maji ya kutosha’ alisema Rais Magufuli.
Awali
akizungumzia kuhusu ujenzi wa barabara hiyo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema kujengwa kwa barabara hiyo
kutaimarisha mawasiliano katika ukanda wa kusini unaojumuisha Mtwara,
Mingoyo, Masasi, Mangaka, Tunduru hadi Mbamba Bay na hivyo kuzidi
kufungua fursa za kiuchumi nanchi jirani za Malawi na Msumbiji.
Alisema
hadi kukamilika kwake barabara hiyo imegharimu kiasi cha Tsh Bilioni
173, ambapo Shirika la Misaada la Japan limetoa asilima 23.24, Benki ya
Maendeleo ya Afrika asilimia63.32 na Serikali ya Tanzania asilimia 13.35
ikiwemo kodi na kulipa fidia kwa wananchi wanaostahili kwa mujibu wa
sheria ya barabara ya mwaka 2007.
Naye
Balozi wa Japan nchini Tanzania, Shinichi Goto alisema Serikali ya
Japan imekuwa mstari wa mbele kuisaidia Tanzania kutekeleza miradi ya
maendeleo ikiwemo barabara ya Namtumbo-Kilimasera-Matemanga-Tunduru na
itaendelea kusaidia miradi mingine ili kuhakikisha kuwa malengo ya
Serikali ya Awamu ya Tano ya kuondoa umaskini kwa wananchi wake
yanafikiwa.
0 Comments