habari Mpya


Ukaaji huu wa Wanafunzi wa Darasa la tano na la Saba Shule ya msingi Ruhuba wilayani Ngara ,Kagera.

Muonekano wa  Wanafunzi wa darasa la tano na la saba wa Shule ya Msingi Ruhuba iliyopo Kata ya Mbuba Wilayani Ngara mkoani Kagera wakiwa wanasoma katika chumba kimoja kilichotenganishwa na Jamvi. 


Habari/Picha Na Shaaban Ndyamukama –RK Ngara.
 
Wanafunzi hao 200 wa darasa la tano na la saba katika Shule ya Msingi Ruhuba  wakizungumza na waandaaji wa kipindi cha SAUTI YA JAMII hivi karibuni  wakiwa darasani ,wamesema msongamano  huo unawapa wakati mgumu wakati wa kujifunza.

Baadhi ya wanafunzi wamesema “Tunakosa uelewa zaidi unaweza kuwa makini unamsikiliza mwalimu wa Hisabati lakini baadaye kelele zikatoka nyuma yetu kutoka kwa wenzetu wanaojifunza somo la Kingereza au jingine, hivyo tunakuwa hatumuelewi vizuri mwalimu,” . 
Mwalimu INNOCENT SOSPETER anayefundisha somo la Hisabati  darasa la saba na BARAKA SABUKA anayefundisha Kiingereza darasa la tano wamesema ufundishaji katika chumba hicho ni ngumu kufikia malengo ya utoaji elimu bora shuleni hapo.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, YUSTAS BENEDICTO  amesema madarasa hayo yametenganishwa kwa wanafunzi kupeana migongo ili wote waweze kupata maarifa, kwamba ni vyema wakafanya hivyo kuliko kutofanya kabisa.

Amesema katika kuhakikisha shule hiyo inaondokana na changamoto hiyo wameitisha mkutano wa wanakijiji kuwahamasisha kujenga  madarasa.

Diwani wa Kata ya Mbuba,  DAVID BUZUTU amesema wananchi wamebweteka na kuacha kuchangia elimu kwa maelezo kuwa Serikali inatoa elimu bure jambo ambalo linawatesa wanafunzi na walimu.

Amewashauri wananchi kushirikiana na watendaji wa halmashauri ya wilaya kufanya  mkutano wa hadhara wa kijiji cha Mbuba chenye shule mbili ya msingi za Mbuba na Ruhuba, kuhamasisha ujenzi wa madarasa.

Hata hivyo, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Ngara, AIDAN BAHAMA amesema wananchi wanaweza kushiriki katika ujenzi na Serikali ikatoa vifaa.

Post a Comment

0 Comments