habari Mpya


Taarifa ya habari ya saa mbili usiku february 14,2019

SHINYANGA
Viongozi wa wachimbaji wadogo mkoani Shinyanga wameweka mkakati wa kuwakamata na kuwataja watu wanaojihusisha na ununuzi na utoroshaji wa madini yanayochimbwa katika migodi midogo mkoani humo

Akizungumza na waandishi wa habari, mwenyekiti wa wachimbaji wadogo Mkoani Shinyanga Bw. Hamza Tandiko amesema kuwa kumekuwepo na watu wanaowachafua wachimbaji wadogo kuwa wanatorosha madini hivyo uongozi hauko tayari kuvumilia na ikiwa watabainika watachukuliwa hatua za kisheria
Kwa upande wake Makamu mwenyekiti wa wachimbaji wadogo Mkoani Shinyanga Bi. Hilda Juliasi amepongeza hatua ya kupunguza kodi ya uchimbaji madini kwa wachimbaji wadogo na kwamba hatua hiyo inakwenda kuwainua hasa wanawake ambao wanajihusisha na uchimbaji mdogo


BIHARAMULO
Kijana mwenye umri wa miaka 22 mkazi wa Kanywamaizi wilayani Biharamulo mkoani Kagera amefikishwa mahakamani kwa tuhuma ya kukatisha masomo ya mwanafunzi wa darasa la pili kisha kumtorosha kwa lengo la kumtafutia

Mbele ya hakimu wa mahakama ya wilaya ya Biharamulo Bi. Frola Ndale, mwendesha mashitaka wa polisi Bw.  Sud Lugana amemtaja mshtakiwa kuwa ni Yohana Samsoni 

Amesema mnamo Februari 7 mwaka huu mshtakiwa alimtorosha wananfunzi huyo aliyekuwa anasoma shule ya msingi maendeleo na kumpeleka mkoani Dodoma kumfanyisha kazi za ndani 

Mshitakiwa amekana shitaka linalomkabili na amepelekwa rumande hadi shauri hilo litakapotajwa tena mahakamani hapo Februari 28 mwaka huu


KAKONKO
Jumla ya miti mia 9 na 7 imepandwa katika shule ya msingi Tumaini iliyopo kata ya Kasanda wilayani Kakonko mkoani Kigoma

Akizungumza na Radio kwizera Afisa maliasili wilayani Kakonko Bw. Saimon Mando ameeleza kuwa wilaya ya Kakonko imeotesha jumla ya miti laki 2 na 50 itakayo gawiwa kwa taasisi mbalimbali na kwa wananchi
Aidha nao baadhi ya wanafunzi na wanajamii walioshiriki kupanda miti katika kata ya Kasanda wameeleza kuwa miti hiyo iliyo pandwa itasaidia kutunza mazingira na jamii itanufaika maana miongoni wa miti iliyopandwa ni pamoja na ya matunda


NGARA
Kijiji cha Bugarama kilichopo wilayani Ngara Mkoani Kagera huenda kikakumbwa na mapigano kati ya wakulima na wafugaji kutokana na kile kinachotajwa kuwa ni rushwa iliyokithiri kwa viongozi

Baadhi ya wananchi wakiongozwa na mabalozi wa nyumba kumi wameeleza kuwa uongozi ngazi ya kijiji hasa mwenyekiti na wajumbe wake ndiowamekuwa vinara wa kupokea rushwa na kupitisha ruhusa kwa wafugaji kutoka nje ya kijiji

Mmoja wa mabalozi anayeongoza eneo la Nyaruguma Bw. Emanuel Bernard amesema eneo lake lina zaidi ya Ng’ombe 400 wakati nyaraka za kijiji zikithibitisha uwepo wa ng’ombe 8

Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa kijiji cha Bugarama Bw. Jaffar Said amewaomba wananchi kuwa wavumilivu huku akiahidi kuyatolea ufafanuzi matatizo yaliyotajwa


KAHAMA
Zaidi ya ekari elfu 1 na 500 za Mahindi na Mpunga katika halmashauri ya Mji wa Kahama Mkoani Shinyanga vimeharibiwa na panya wakati yakiwa yameanza kuota

Hayo ni kwa mujibu wa Afisa kilimo halmashauri ya mji wa Kahama Bw. Samson Sumuni

Amesema idara ya kilimo ilitoa taarifa wizara ya kilimo na watalaamu walileta dawa kilo 150 ya kuangamiza panya hao ambapo kilo 9 pekee ndizo zilitumika na ekari 540 hazikudhibitiwa kutokana na wakulima kutojitokeza kuchukua dawa hiyo

Kutokana na hali hiyo amewataka wananchi kujitokeza kuchukua dawa kwa ajili ya kuwatega ili wakulima waweze kuvuna na kujiepusha na njaa


Post a Comment

0 Comments