habari Mpya


Watumishi wa Umma Kagera watakiwa Kumpa Ushirikiano Katibu Tawala Mpya.

Na: Sylvester Raphael.

Katibu Tawala mpya wa Mkoa wa Kagera Profesa Faustine Kamuzora katika siku yake ya pili katika kituo chake kipya cha kazi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera akutana na Watumishi wa ofisi yake na kuzungumza nao ambapo alitoa mwelekeo wa kutimiza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kipaumbele chake katika Mkoa wa Kagera.
Katika kikao kifupi na watumishi wa ofisi yake Januari 11, 2019 Katibu Tawala mpya wa Mkoa wa Kagera Profesa Kamuzora aliwaomba watumishi atakaowaongoza katika utumishi wa umma kumpa ushirikiano wa kutosha ili kuweza kutekeleza majukumu yake ya kuwaletea wananchi maendeleo na kuinua uchumi wa Mkoa wa Kagera na kuurudisha katika enzi zake.

Profesa Kamuzora akitaja kipaumbele chake katika Mkoa wa Kagera alisema kuwa ni kuona namna bora ya kupambana na suala la utapiamlo hasa kwa watoto kwani takwimu zilizopo sasa Kagera inashika nafasi ya nne kwa asilimia 41.7%  kati ya mikoa 25 Tanzania Bara ambapo takwimu hizo zinatisha sana na kupelekea udumavu hasa udumavu wa akili hususani kwa watoto.

Kama hatutaangaika na suala hili la utapiamlo hatuwezi kusonga mbele kwasababu hata uwezo wa kufikiri hasa kwa watoto wetu ni mdogo sana utaendelea kuwa mdogo sana jambo ambalo ni hatari kubwa kwa  vizazi vya sasa na vijavyo.”  Alifafanua Profesa Kamuzora.

Profesa Kamuzora aliendelea kusisitiza kuwa anajua kuna sababu nyingi zilizochangia katika kuurudisha nyuma Mkoa wa Kaegera kimaendeleo ikiwa ni pamoja na VITA, TETETEMEKO, AJALI YA MV BUKOBA, UGONJWA WA UKIMWI lakini alisema kuwa watumishi na wananchi kwa ujumla wanatakiwa kushikamana na kupambana kama nchi ya Rwanda walivyofanya baada ya vita ya wenyewe kwa wenyewe na wakasonga mbele na Rwanda sasa ipo mbali kimaendeleo.
Katika upande mwingine Profesa Kamuzora alipongeza juhudi mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na uongozi wa Mkoa wa Kagera katika sekta mbalimbali mfano Elimu kuwa mkoa unaendelea kufanya vizuri na taratibu unarejea enzi zake za zamani. Pia aliwaomba watumishi kuendelea kushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali hata za kimaendeleo ili kuufikisha mkoa mahali pake.

Mkoa wa Kagera unakabiliwa na tatizo kubwa la utapiamlo ambapo unashika nafasi ya nne kutoka mwisho kwa asilimia 41.7% ya utapiamlo na Mkoa wa Njombe ukiongoza kwa asilimia 49.4% ya utapiamlo wakati mkoa ambao una asilimia ndogo ya utapiamlo ukiwa ni Dar es Salaam ambao una asilimia 14.6% (Takwmu za mwaka 2016).

Profesa Faustine Kamuzora ni Katibu Tawala wa 20 tangu uhuru. Aidha, Profesa Kamuzora aliteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Kagera na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli  Januari 8, 2019 na kuapishwa Ikulu Jijini Dar es Saalam Januari 9, 2019 na alilipoti Mkoani Kagera Januari 10, 2019 na kuanza kazi ya kutekeleza majukumu yake ya kazi mara moja.

Post a Comment

0 Comments