habari Mpya


Muhimu Bodaboda Kagera Kuwajibishana Wao Bila Jeshi la Polisi na Kuwa Kivutio cha Utali– RC Gaguti.

Na: Sylvester Raphael

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti aweka wazi mikakati yake ya kuwafanya  Waedesha Pikipiki maarufu kama Bodaboda Mkoani Kagera hasa katika Manispaa ya Bukoba kuwa mojawapo ya Utalii katika Mji wa Bukoba na bodaboda hao kufanya kazi zao kiueledi na kwa kuinua vipato vyao huku wakijishughulisha na ujasiliamali katika vikundi vyao.

Ni baada ya  Mkuu wa Mkoa Gaguti kukutana na Bodaboda katika Ukumbi wa Linas Night Club Manispaa ya Bukoba Januari 17, 2019 na kuongea nao ambapo aliweka  wazi ni jinsi gani atahakikisha anasimamia mikakati yake ili wasafirshaji hao wafanye kazi zao kama yeye anavyotamani wafanye lakini wakizingatia taratibu na sheria za Usalama Barabarani.

Nimewaiteni katika mkutano huu nia ikiwa ni kukutana nanyi na kuweka mazingira mazuri ya kufanya kazi zenu kwani najua kuwa kwa kipindi cha nyuma mmekuwa mkifanya kazi katika mazingira yasiyokuwa mazuri na mkiwa na mivutano na Vyombo vya Ulinzi na Usalama hasa Jeshi la Polisi pale wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao ya Usalama Bararani.” Alitaja Lengo la Mkutano Mkuu wa Mkoa Gaguti
Mkuu wa Mkoa Gaguti aliyataja mambo makuu matatu muhimu ambayo Bodaboda wanatakiwa kuyatekeleza haraka kwanza, Kuunda vikundi na kuvisajili vikundi hivyo katika maeneo yao ya kazi ili Bodaboda watambulike na kupitia vikundi hivyo wapate mikopo na elimu ya ujasilamali nje ya kuendesha Bodaboda ili kuingiza kipato zaidi.

Pili, Kupitia vikundi vitakavyoundwa Bodaboda wote wapatiwe elimu ya Usalama Barabarani lakini pia kupitia vikundi vyao washiriki katika Ulinzi na Usalama wa Mkoa wa Kagera kwani kumekuwa na tabai ya majambazi kujificha katika kazi ya kuendesha Bodaboda huku wakifanya uhalifu. Aidha, Mkoa wa Kagera unapakana na nchi tatu za Burundi, Rwanda na Uganda na ni muhimu kila mwananchi kuwa mzalendo.

Tatu, Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kuwa anataka Bodaboda wapate elimu ya ujasiliamali mbali na kuendesha Bodaboda ili vijana watarajike kupitia ujasiliamali pia.  “Hivi utafanya kazi hii ya Bodaboda mpaka uzee wako? Ni lazima tuwaandae nyinyi vijana kuanza ujasiliamali ambao hata ukizeeka au kupata ajali hutapata shida na familia yako itaendelea kupata huduma kwani hutotegemea tena Bodaboda.” Alifafanua Mkuu wa Mkoa Gaguti.

Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kuanzia sasa hataki kuona au kusikia tena mivutano ya Bodaboda na Jeshi la Polisi bali wawe na mahusianao mazuri na alisema kuwa kama mfumo anaoulenga utafanya kazi kutakuwa hakuna haja ya Jeshi la Polisi kuwakamata Bodaboda bali wao wenyewe wachukuliane hatua mmoja wao anapovunja sheria katika vikundi vyao ambavyo vitakuwa imara kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

Hivi karibuni katika Mkoa wa Kagera utalii unaanza na katika mji wetu wa Bukoba Bodaboda bado wapo hovyo lakini natamani Bodaboda nyinyi muwe wa mfano kwa kuvaa sare na kutoa huduma bora za usafiri ili mikoa mingine ije kujifunza hapa na watalii wakija liwe eneo mojawapo la utalii waone jinsi vijana wanvyofanya kazi ya Bodaboda kwa weledi na kufuata sheria lakini wakiwa katika vikundi vyao vilivyosajiliwa.” Alisisitiza Mkuu wa Mkoa Gaguti.

Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kuongea na Bodaboda Mdau wa Usalama Barabarani Mkoani Kagera Bw. Winston Kabantega alimweleza Mkuu wa Mkoa Gaguti kuwa biashara ya Bodaboda ilianzia mjini Bukoba na kuenea nchi nzima lakini sasa Mkoa wa Kagera haumo katika mikoa mitatu bora inayofanya vizuri katika biashara ya Bodaboda nchini.

Bw. Kabantega alisema suala hilo lilitokana na Bodaboda wengi kutokuwa na Elimu ya Usalama Barabarani, kuwa na mivutano na Jeshi la Polisi jambo lililokuwa linapelekea kufukuzana mjini na kusababisha ajali nyingi. 

Pia Bw. Kabantega alisema kuwa kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2018 zaidi ya ajali 800 za Bodaboda zilitokea nchini na Mkoa wa Kagera ukichangia katika ajali hizo.
Maazimio.

Katika Mkutano huo Mkuu wa Mkoa Gaguti alikubaliana na Bodaboda na kuazimia kama ifuatavyo: Kwanza, Mkuu wa Mkoa Gaguti awe Mlezi wa Bodaboda Mkoani Kagera na kuanzia sasa Bodaboda waliopo mjini Bukoba wakiwakilisha wenzao maeneo mengine wawe tayari kuufanya usafiri wa Bodaboda kuwa wa kuaminika kwa kufuata sheria na kuvaa sare ili kuufanya mji wa Bukoba kuwa Mji wa kitalii katika suala la bodaboda kwani  Bukoba ndiye mhasisi wa usafiri wa Bodaboda.

Pili, Bodaboda wavae viaksi mwanga (Reflectors) zenye namba na eneo Bodaboda anakofanyia kazi ambapo kwa Bodaboda wote walioudhuria mkutano huo Mkuu wa Mkoa Gaguti aliwahaidi kuwapatia bure viaksi mwanga hivyo.

Tatu, kila Bodaboda kukubali kujiunga katika kikundi na kupewa elimu ya ujasiliamali ili atajirike nje ya kuendesha Bodaboda kwa kupata mikopo mbalimbali kupitia vikundi ambapo Mkuu wa Mkoa Gaguti alihaidi kuchangia Pikipiki tatu kwa kuanzia katika vikundi vitakavyofanya vizuri ili zawadi hizo za pikipiki ziwasaidie wanakikundi kukuza uchumi wa kikundi husika.

Naye Bw. Abdusalum Mashankara Dereva Bodaboda katika Manispaa ya Bukoba akimshukuru Mkuu wa Mkoa kwaniaba ya wenzake alisema kuwa Mkuu wa Mkoa Gaguti kaweka historia kuamua kuwaita na kukaa nao kuwapa mikakati yake ya kuona usafiri wa Bodaboda katika Mkoa wa Kagera unafanya vizuri na Vijana wanatajirika kupitia ajira hiyo.

Bw. Mashankara alisema kuwa Mkuu wa Mkoa amewafungua macho Bodaboda kwani kila Taasisi ina chombo chake mahala pa kupeleka kero lakini Bodaboda hawakuwa nacho hicho chombo na kwa mwongozo wa Mkuu wa Mkoa chombo hicho sasa  kitaundwa na akamshukuru Mkuu wa Mkoa Gaguti kukubali kuwa mlezi wa Bodaboda katika Mkoa wa Kagera.

Mwisho Bw. Mashankara alitoa ombi kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Gaguti kuwa iundwe Kamati ya Mkoa ambayo itawajumuisha baadhi ya  Bodaboda katika Kamati hiyo ili kuweka taratibu na kanuni za kusimamia usafiri na usafirishaji wa Bodaboda kuwa mzuri zaidi katika Mkoa wa Kagera.

Post a Comment

0 Comments