habari Mpya


Maafisa wa Vyombo Vya Ulinzi na Usalama Kutoka Nchi Kumi na Moja Wanafunzi wa Chuo Cha Ulinzi Cha Taifa Waja Kagera Kupata Somo

Na: Sylvester Raphael

Ujumbe wa Kitaifa wa Maafisa wa Vyombo Mbalimbali vya  Ulinzi na Usalama kutoka Chuo cha Ulinzi cha Taifa (National Defence Collage) ukiwakilisha nchi 11 tofauti wautembelea Mkoa wa Kagera Januari 7, 2019 kujifunza na kubadilishana ujuzi na Uongozi wa Mkoa hasa katika masuala ya Ulinzi na Usalama na kutumia fursa hiyo kushauriana namna bora ya kukuza uchumi wa Mkoa wa Kagera.

 Ujumbe huo wa Maafisa 16 kutoka Chuo cha Ulinzi cha Taifa ukiwa na Maafisa kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Nigeria na China mara baada ya kuwasili Mkoani Kagera ulipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti ofisini kwake na Kiongozi wa Ujumbe huo Balozi Peter Kallage alisema lengo kubwa ni kuja Kagera Kujifunza na kubadilisha mawazo hasa katika Nyanja za Ulinzi Kimataifa na kuona namna bora ya kuendeleza fursa mbalimbali za kukuza uchumi.

Chuo cha Ulinzi cha Tanifa (NDC) ni chuo ambacho kipo chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na kinaendesha kozi mbali mbali za Kimataifa kama unavyoona hapa tuna Maafisa kutoka nchi nne kama nilivyozitaja hapo awali lakini kwa kozi hii ambayo imetuleta hapa Kagera ina Maafisa kutoka nchi 11 tofauti na tumewagawanyika katika makundi 4 na Maafisa wengine wamekwenda katika mikoa mingine sisi tumechagua kuja Kagera .” Alifafanua Balozi PETER KALLAGE
Aidha, Ujumbe huo kutoka Chuo cha Ulinzi cha Taifa  ulipitishwa kwenye Wasifu wa Mkoa wa Kagera wa Kiuchumi na Kijamii ili kuonesha maendeleo ya Mkoa, Fursa mbalimbali za uwekezaji na changamoto ambazo mkoa unazipitia katika kuendelea kukuza uchumi wake na uchumi wa wananchi kwa ujumla. Katika wasilisho hilo Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kuwa pamoja na Mkoa wa Kagera kufanya vizuri kiuchumi lakini chamoto kubwa ni Wahamaiaji Haramu, na Biashara ya magendo ya Mazao.

“Pamoja na Mkoa wetu kuwa na fursa nzuri za kiuchumi kwa kupakana na nchi tatu za Rwanda, Burundi na Uganda na kuwa kitovu cha biashara cha Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini bado tunakabiliwa na Changamoto ya Wahamiaji haramu na Bishara ya Magendo ya mazao. Tunaendelea kushirikiana na Viongozi wenzetu wa nchi jirani kukomesha uhamiaji haramu, pia uongozi wa Mkoa umeanzisha Mkakati wa Nyumba Kumi bora kuhakikisha biashara hiyo inakoma.” Alieleza Mkuu wa Mkoa Gaguti. 
Maafisa hao mara baada ya kupitishwa kwenye Wasifu wa Mkoa walishauri namna mbalimbali za kuimarisha Ulinzi na Usalaama katika Mkoa, namna bora za kufanyia kazi fursa za kiuchumi zilizopo katika Mkoa wa Kagera ili kuinua uchumi wa mkoa pamoja na uchumi wa wananchi na kuchangia pato la Taifa kwa ujumla.

Mara baada ya kupitishwa katika Wasifu wa Kiuchumi na Kijamii wa Mkoa wa Kagera Kiongozi wa ujumbe huo wa Maafisa kutoka Chuo cha Ulinzi cha Taifa aliushukuru Uongozi wa Mkoa wa Kagera kwa kukubali ombi la chuo hicho kuualeta ujumbe wa Maafisa hao kuja Mkoani Kagera kujifunza hasa katika fursa mbalimbali za Kiuchumi, Ulinzi na Usalama pia na kuona fursa za uwekezaeji zilizopo Mkoani humo.

Pamoja na kupitishwa katika wasifu wa Kiuchumi na Kijamii wa Mkoa wa Kagera Ujumbe wa Maafisa hao 16 kutoka Chuo cha Ulinzi cha Taifa pia utakuwepo Mkoani Kagera kwa ziara ya siku saba ili kutembelea maeneo mbalimbali ya uwekezaji, maeneo ya utalii, viwanda pia na kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji mali kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera.

Post a Comment

0 Comments