habari Mpya


Halmashauri za Wilaya Nchini zatakiwa Kujenga Nyumba za Watumishi wa Jeshi la Polisi.

Wananchi wakimsikiliza kwa umakini Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, KANGI LUGOLA Januari 8, 2019 kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika uwanja wa Fatuma mjini Muleba.
 
Na Shaban Ndyamukama & Shafiru Yusuf –RK Muleba.

Halmashauri za wilaya kote nchini zimeagizwa  kutenga fedha kutoka vyanzo vya  mapato ya ndani, kwa kushirikisha wananchi kujenga nyumba za watumishi wa Jeshi la polisi wanaolinda usalama wa raia na mali zao.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, KANGI LUGOLA ametoa agizo hilo januari 8, 2019 kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika uwanja wa Fatuma  mjini Muleba  mkoani Kagera na kwamba nyumba hizo zijengwe  palipo na kituo cha Polisi.

Amesema askari wanatakiwa kuishi kambini kwenye makazi ya pamoja na kulinda maadiliyao ya kiutendaji wakiwa na familia zao badala ya kuishi mitaani na kukiuka misingi ya  utumishi wa umma na wengine kushawishiwa na  rushwa.

Waziri LUGOLA Amesema halmashauri nyingi nchini kwa kutumia kamati za ulinzi na usalama zikijipanga zitaweza kuanzisha maboma ya nyumba za polisi kama zinazvyojengwa nyumba za walimu, wahudumu katika sekta ya afya na idara nyingine.
Waziri LUGOLA .

Aidha amesema iwapo halmashauri zitaonesha juhudi za kujenga nyumba za askari kwa kushirikisha wananchi serikali itajitahidi kutoa mahitaji ya viwandani kama mabati saruji na mengineyo kuwamotisha wafanye kazi kwa uadilifu zaidi.

Pia  Waziri LUGOLA ameagiza Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Kagera Revocatus Malimi  ndani ya siku saba, kusaka  wanume  wanaotuhumiwa kuwasababishia ujauzito wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na kuwafikisha mahakamani.
Mkuu wa wilaya ya Muleba RICHARD RUYANGO akitoa taarifa ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, amesema Polisi wameisaidia wilaya kukabiliana na vitendo vya uvuvi haramu, ujangili wa wanyama  hifadhi za Burigi na ranchi za Taifa mkoani Kagera.

RUYANGO amesema  wilaya ya Muleba inahitaji ZAIDI VITUO VYA POLISI NA ASKARI kutokana na jiografia kuwa kubwa ikiwa na kata 43, vijiji 166 na vitongoji 754 ambapo mazingira yote ya majini na nchi kavu yanahifadhi wahalifu.

Mkuu huyo wa wilaya  amesema pamoja na kupongeza Askari Polisi, bado wanaishi mazingira magumu kiutendaji kwa kuishi nyumba za kupanga  na raia lakini wanateseka hasa  walioko vituo  vya polisi vya visiwani ndani ya ziwa viktoria.

Katika mkutano wa Waziri LUGOLA, Wananchi wamelalamikia askari polisi kwa kuwabambikizia kesi  huku madereva wa magari wakilalamikia tabia ya askari wa usalama barabarani kuwapiga tochi wakiwa wamejificha vichakani.

Post a Comment

0 Comments