habari Mpya


Asilimia 0.4% ya Ulipaji Kodi Kagera yamshitua RC Gaguti na Kutoa Maagizo Yafuatayo.

Na: Sylvester Raphael

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti awaagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoa wa Kagera (TRA) kuanzia Januari 11, 2019 kuacha tabia za kufunga biashara za wananchi kwasababu ya kodi badala yake wajikite katika kutoa elimu na kuwaelimisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa utashi bila kushurutishwa sambamba na kuweke mkakati wa kuwapata walipakodi wapya.

Maagizo hayo yalitolewa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Gaguti katika kikao cha Baraza la Wafanyabiashara kilichofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Bukoba Januari 11, 2019 ambapo aliwaita wafanyabiashara hao kuwasikikiliza kero zao ili kuboresha ulipaji wa kodi katika Mkoa wa Kagera ikiwa ni pamoja na kufikia malengo ya ukusanyaji wa kodi kwa mwaka 2018/2019 kwa asilimia 100%.
Kabla ya Mkuu wa Mkoa kutoa maagizo hayo ,Wafanyabiashara waliopata nafasi ya kuchangia katika kikao hicho walilalamika juu ya utendaji kazi wa  Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwa wanakusanyatu kodi bila kutoa elimu na hawajengi mazingira mazuri yakuwasikiliza wafanyabiashara ili walipe kodi kwa utashi hasa katika Mkoa wa Kagera jambo ambalo limepelekea wafanayabisahara wengi kufunga biashara zao.

Mara baada ya kuwasikiliza Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kuwa anataka katika Mkoa wa Kagera kuwe na mazingira mazuri ya wafanyabiashara kufanya biashara zao  na kulipa kodi bila kushurutishwa na kila mfanyabiashara atambuliwe ili kuwa na takwimu sahihi za wananchi wote wanaojishughulisha na biashara.

Mkuu wa Mkoa Gaguti alitoa siku kumi na nne kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwatumia Viongozi na Watendaji katika ngazi za Kata hadi Vijiji kuwatambua wafanyabiashara wote wawe wakubwa au wadogo ili kuwe na takwimu sahihi ya mkoa kuhusu wananchi wanaojishughulisha na biashara kwani  katika Mkoa wa Kagera ulipaji kodi ni asilimia 0.4% tu.
Mara baadaya kikao cha Baraza la Biashara la Mkoa wa Kagera kumalizika Mkuu wa Mkoa na Ktibu Tawala wa Mkoa pamoja na viongozi wengine walitemblea baadhi ya Wafanyabiashara katika Mtaa wa One Way na Soko Kuu Manispaa ya Bukoba kusikiliza Changamoto wanazokumbana nazo ili kuzitafutia ufumbuzi na kuweka mazingira rafiki ya kufanya biashara na kulipa kodi stahiki kwa utashi.

Aidha, Mkuu wa Mkoa Gaguti aliitaka TRA Mkoa wa Kagera kutanua wigo katika kukusanya kodi hasa kodi za majengo na ardhi. Pia aliwataka wafanyabiashara kuwa wakweli katika kutoa takwimu zao za biashara ili wasikwepe kodi na wala wasionewe. 

Mwisho Mhe. Gaguti aliitangaza tarehe 25 hadi 30 Machi, 2019 kuwa itakuwa wiki ya Kagera na kuwaomba wananchi katika Sekta zote kushiriki kuutangaza Mkoa wa Kagera katika wiki hiyo.

Katika hatua nyingine Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Prof. Faustine Kamuzora aliyehudhuria kikao hicho aliwahakikishia Wafanyabiashara kuwa sasa uongozi wa mkoa umejipanga kuondoa vikwazo vyote vinavyorudisha juhudi za wafanyabiashara kusonga mbele ambapo alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inataka kuona kila mwananchi anatajirika katika nchi yake mahali popote alipo.

Profesa Kamuzora alisema kuwa atahakikisha anaimarisha Mabaraza ya Wfananyabiashara ya Wilaya na Mkoa ili kuhakikisha Sekta binafsi inashirikiana na Serikali kikamilifu katika kuchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments