habari Mpya


Waziri Mpina Aagiza Wakurugenzi,Wenyeviti na Madiwani 11 waliokamatwa Kwa Uvuvi Haramu Kufika Dodoma Kujieleza.

Waziri wa Mifugo na Uvivu Luhaga Mpina akiteketeza nyavu 352 haramu za uvuvi katika eneo la Businde nje kidogo ya Manispaa ya Kigoma Ujiji zilizokamatwa kwenye oparesheni maalum ya kuzuia uvuvi haramu zenye zaidi ya shilingi bilioni 3 zilizokuwa zikitumika ndani ya  ziwa Tanganyika.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina akiongea na wavuvi pamoja na wafanyabiashara wa mazao ya dagaa na samaki katika mwalo wa Kibirizi kabla ya kuteketeza zana haramu za Uvuvi zilizopatikana kufuatia oparesheni ya kuzuia uvuvi haramu inayoendelea katika Ziwa Tanganyika.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameagiza madiwani 11 waliokamatwa wakijihusisha na uvuvi usiozingatia sheria amoja na wenyeviti na wakurugenzi wa halmashauri zao kufika ofisini kwake Dodoma Leo Desemba 5,2018 Jumatano kwa mahojiano zaidi huku wakiwa na nyaraka zote walizosaini walipokamatwa na kulipa faini kutokana na makosa hayo.

Akizungumza katika kikao cha tathmini ya Operesheni Sangara awamu ya tatu inayoendeshwa katika Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Bwawa la Nyumba ya Mungu na Mtera, kilichofanyika jana mkoanin Kigoma, Waziri Mpina amesema kitendo cha madiwani hao kukamatwa na kulipa faini kinawaondolea sifa ya kuwa wasimamizi wa rasimali za uvuvi katika maeneo yao.

Kufuatia hali hiyo, Waziri Mpina ameamua kuanzisha Kanda Kuu ya Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi, Ziwa Tanganyika na kumteua West Mbembati kuongoza kanda hiyo na kuanzisha kanda zingine ikiwemo Kanda ya Rorya, Ziwa Rukwa, Nyumba ya Mungu, Mtera ili kuongeza ulinzi na usimamizi wa rasilimali hizo za uvuvi.

Hivi karibuni, baadhi ya Madiwani walikamatwa wakijihusisha na uvuvi usiokubalika katika Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika na kutozwa faini katika Operesheni Sangara.

Pia katika operesheni hiyo wamefanikiwa kuwakamata raia wa kigeni 242 wakijishughulisha na uvuvi huo katika Ziwa Victoria na Tanganyika na kuwaomba mawaziri wenzake wa uvuvi katika nchi jirani kuwaelimisha wananchi wao juu ya ulinzi wa rasilimali za uvuvi pamoja na umuhimu wa kutii sheria za nchi husika.

Post a Comment

0 Comments