habari Mpya


Ujenzi Barabara Bariadi Hadi Maswa Mkoani Simiyu.

Moja ya mitambo ya Kampuni ya CHICO kutoka China, inayotumika kujenga barabara Bariadi hadi Maswa mkoani Simiyu kwa kiwango cha lami, yenye urefu wa km 50, ikiwa kazini, huku ujenzi wa kipande hicho cha barabara utakao gharimu sh. bilioni 88, ukiwa umekamilika kwa asilimia 34. 

Na Benny Mwaipaja, WFM, Simiyu
Ujenzi wa daraja kubwa la Simiyu linalounganisha wilaya za Bariadi na Maswa ukiendelea kwa kasi ikiwa ni sehemu ya ujenzi wa miundombinu ya barabara yenye urefu wa kilometa 50 (Bariadi-Maswa), mkoani Simiyu.
Ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 50 kati ya mji wa Bariadi na Maswa mkoani Simiyu kwa kiwango cha lami, inayojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 88, unaendelea kwa kasi ambapo hivi sasa umefikia asilimia 34.

Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini-TANROADS, mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mohamedi Athumani, ameiambia timu ya maafisa wa Serikali inayoongozwa na Wizara ya Fedha na Mipango, inayofuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani humo kwamba mradi huo utakapo kamilika  mwezi Oktoba mwakani, utafungua fursa za kibiashara na kiuchumi kwenye mkoa huo na mikoa jirani ya Mwanza, Shinyanga, Singida na nchi jirani ya Kenya.

Amesema kuwa kazi zilizofanywa na mkandarasi anayejenga barabara hiyo, Kampuni ya CHICO ya China, ni kuanza kwa ujenzi wa madaraja makubwa mawili ya Simiyu na Banhya na uinuaji wa tuta la barabara maeneo mbalimbli ya mradi.

"Kuna madaraja mengine madogo madogo (Pipe culverts 57) pamoja na makalvati madogo (Box culverts 12), kwenye kipande hiki cha Barabara chenye urefu wa kilometa 50 na mkandarasi, Kampuni ya CHICO inafanyakazi vizuri na tuna imani kwamba ujenzi wa barabara hii utakamilika ifikapo mwezi Oktoba, 2019 kama mkataba unavyoonesha" alifafanua Mhandisi Athumani.

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri Mkazi wa mradi huo, Mhandisi Swalihi Kazuvi amesema kuwa barabara ya Mwigumbi-Maswa-Bariadi na Lamadi, inayojengwa kwa kiwango cha lami, yenye urefu wa kilometa 172, itakapokamilika, italeta chachu ya maendeleo yanayopitiwa na barabara hiyo.

"Kipande cha barabara ya lami kutoka Mwigumbi mpaka Maswa na kile cha Bariadi hadi Lamadi vimekamilika kwa hiyo kipande kilichobaki ni hiki (Bariadi-Maswa), ndio maana unaona magari yanayopita barabara hii ni mengi licha ya kwamba kipande hiki cha kilometa 50 hakijakamilika, madereva wanaona afadhali wapite huku kwenda Musoma kuliko kupitia njia ya Mwanza" aliongeza Mhandisi Swalihi Kazuvi

Lengo la ziara hiyo ya maafisa wa Serikali ni kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezawa katika  Mkoa huo ili kujua mafanikio, changamoto na mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo.
Maafisa wa Serikali wakiongozwa na Wizara ya Fedha na Mipango, wakikagua ujenzi wa Daraja la Mto Simiyu, kwenye ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, ya Bariadi hadi Maswa, (km50), wakati wa ziara ya kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Simiyu.

Post a Comment

0 Comments