habari Mpya


Mkoa wa Kagera wagawa Vitambulisho 25,000 Kwa Wajasiriamali Wadogo.

Na: Sylvester Raphael-Kagera.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti ametekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli la kugawa vitambulisho kwa Wajasiriamli Wadogo ili waweze kufanya shughuli zao za ujasiriamali na kujiingizia kipato chao cha kila siku bila kusumbuliwa na mtu yeyote.

Mkuu wa Mkoa Gaguti ametekeleza agizo hilo la Rais Magufuli leo Desemba 20, 2018 katika Uwanja wa Uhuru (Maarufu kama Mayunga) Manispaa ya Bukoba ambapo alivigawa vitambulisho hivyo kwa Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Kagera na Halmashauri zake nane.
Mkoa wa Kagera ulipewa vitambulisho jumla 25,000 vilivyotolewa na Rais Magufuli na kusisitiza  kuwa vitambulisho hivyo vikigawiwa na kuisha uongozi wa mko utaomba vingine zaidi ili kuhakikisha kila Mjasiriamali Mdogo anapata kitambulisho hicho.

Mkuu wa Mkoa Gaguti alitoa angalizo kuwa vitambulisho hivyo vinawalenga Wajasiriamali au Wafanyabiashara Wadogo na  wanatakiwa kuwa walinzi wao wenyewe kujilinda ili waweze kujiingizia kipato chao bila kusumbuliwa lakini wasiwe mawakala wa wafanyabiashara wakubwa ili kuwafanyia biashara kwa kutumia vitambulisho hivyo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, aliwatahadharisha wafanyabiasha wadanganyifu kuwa tayari ofisi yake imepata taarifa kuwa kuna baadhi ya Wafanyabiashara wasio waaminifu kuwa wameanza kupunguza bidhaa kwenye chanja za maduka yao ili waweze kutambuliwa kama Wajasiriamali Wadogo wakilenga kupata vitambulisho. “Ukibainika umefanya mchezo huo hatua kali zitachukuliwa kwa kuzingatia sheria na katika zoezi hili Serikali itasimaia sheria ipasavyo.” Alitahadharisha Mkuu wa Mkoa Gaguti.

Hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na wafanyabiashara watakaogundulika kufanya mchezo wa udanganyifu ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzani kuwafutia moja kwa moja leseni za biashara. 

Aidha, Viongozi wa Serikali za Mitaa na Watendaji wa Kata walitakiwa kutenda haki katika utambuzi wa Wajasiliamali Wadogo katika maeneo yao. Pia wananchi walitakiwa kupaza sauti pale watakapoona zoezi hilo linaendeshwa bila kutenda haki.
Naye Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kagera Bw. Adam Ntoga alitoa ufafanuzi wa ni Mjasiriamali yupi Mdogo anatakiwa kupata kitambulisho ambapo alisema kuwa ni Wajasiriamali wadogo ambao hawajawahi kutambuliwa na mfumo wa kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania na mzunguko wao wa fedha haufikii kiasi cha shilingi milioni nne. Pia Bw. Ntoga alisema kuwa malipo ya kitambulisho hicho ni shilingi 20,000/- tu.
Katika Mkoa wa Kagera, Wilaya ya Bukoba ilipatiwa jumla ya vitambulisho 3,580 na Wilaya za Missenyi, Karagwe, Kyerwa, Ngara, Biharamulo na Muleba kila Wilaya kupitia Wakuu wa Wilaya zilipatiwa vitambulisho 3,570 na kukamilisha jumla ya Vitambulisho 25,000 vilivyotolewa katika Mkoa wa Kagera na Rais Magufuli Desemba 10, 2018

Ikumbukwe kuwa Desmba 10, 2018 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli  akiwa Ikulu Jijini Dar es Salaam alitoa vitambulisho vya wajasiriamali wadogo 670,000 kwa Wakuu wa Mikoa yote na kila Mkoa ulipatiwa vitambulisho 25,000 na Mkoa wa Kagera ukiwemo ambapo Rais Magufuli alisema kuwa kila Mkuu wa Mkoa atakusanya shilingi 500 milioni kupitia vitambulisho hivyo.

Post a Comment

0 Comments