habari Mpya


Madaktari Bingwa Watoa Huduma ya Matibabu Mkoani Kagera.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti anapenda kuwataarifu Wananchi wa Mkoa wa Kagera na nje ya Mkoa kuwa Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wameandaa Kliniki tembezi ya Madaktari Bingwa wa fani mbalimbali itakayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa (Government) kuanzia tarehe 05 – 11 Novemba, 2018.

Ikiwa ni mara ya pili kutekeleza zoezi hilo la huduma za kibingwa katika Mkoa wa Kagera kutakuwa na Madaktari Bingwa kati ya 28 hadi 34 kutoka Hospitali za Kanda za Bugando, KCMC, Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na baadhi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa.

Madaktari hao Bingwa wanatarajia kutoa huduma katika magonjwa ya Uzazi na kizazi kwa wanawake, Magonjwa ya upasuaji kwa jumla, Magonjwa ya njia ya mikojo ikiwemo tezi Dume, Magonjwa ya pua, sikio na koromeo.

Magonjwa mengine yatakayoshughulikiwa na Madaktari Bingwa ni pamoja na Magonjwa ya mifupa, Magonjwa ya moyo, Magonjwa ya ndani ikiwemo sukari na figo, Magonjwa ya watoto, Magonjwa ya Afya ya kinywa na meno, Magonjwa ya macho, Magonjwa ya Ngozi, Magonjwa ya afya ya akili, na Saratani ya Mlango wa kizazi.
Mkuu wa Mkoa Gaguti anatoa rai kwa wananchi hasa wenye matatizo mbalimbali ya kiafya kuchangamkia fursa ya Madakitari Bingwa kwani gharama za kuwaona Madaktari hao zitakuwa nafuu sana ukilinganisha na gharama za kuwafuata Madaktari Bingwa Katika Vituo vyao vya kazi kama Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali ya Rufaa ya Bugando au KCMC Moshi ikiwa ni pamoja na gharama za kusafiri na kuishi huko wakati ukisubiri kumuona Daktari Bingwa.

Mkuu wa Mkoa Gaguti anasisitiza kuwa (Mwananchi) mgonjwa kumuona Daktari Bingwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera itakuwa ni shilingi 10,000/= (Elfu kumi tu) kwa magonjwa yote isipokuwa magonjwa ya moyo itakuwa ni shilingi 15,000/= (Elfu kumi na tano tu). Gharama hizi ni nafuu sana ukilinganisha na gaharama ya shilingi 25,000/= hadi 40,000/= kumuona Daktari Bingwa akiwa katika kituo chake cha kazi kwa magonjwa yote na magonjwa ya moyo shilingi 40,000/= hadi shilingi 50,000/=.

Aidha, gharama za upasuaji nazo zitakuwa nafuu sana, upasuaji katika magonjwa yote gaharama yake itakuwa katai ya shilingi 60,000/= hadi 100,000/= tu ambapo itakuwa nafuu sana ukilinganisha na gharama za upasuaji Madaktari Bingwa wakiwa katika vituo vyao vya kazi ambapo huanzia shilingi 300,000/= hadi shilingi 1,500,000/=.

Pia Mhe Gaguti anawakumbusha wananchi kuwa zoezi la kuwaleta Madaktari Bingwa Mkoani Kagera kwa kiasi kikubwa litagharamiwa na Serikali ili kuhakikisha wananchi wake wanasogezewa huduma za matibau karibu.

Katika zoezi tulilotekeleza Septemba 18 hadi 24, 2017 tuliweza kuwahudumia wananchi takribani 3,146 na mwaka huu 2018 tumelenga kuwahudumia wananchi 4,000 hadi 5,000 kwa kuwa tumeongeza wigo wa Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo na tunatarajia wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo nao watapata huduma za kibingwa.” Alifafanua Mkuu wa Mkoa Gaguti.

Mwisho Mkuu wa Mkoa Gaguti anatoa Wito kwa wananchi ambao wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali kuchangamkia fursa hiyo, na Serikali ya Mkoa wa Kagera imejipanga vizuri katika Dawa, vipimo, na katika utoaji wa huduma ili kuhakikisha Madaktari Bingwa wanawahudumia wananchi kwa uhakika na kikamilifu zaidi.

Wananchi wenye matatizo ya kiafya wajitokeze kwa wingi ili kupata huduma za kibingwa lakini pia kwa kuwa muda utakuwa mfupi wa siku saba tu kuanzia tarehe 5 hadi 11, Novemba, 2018 wananchi mnakumbushwa kuwahi kuanzia tarehe 5 Novemba, 2018.


Imetolewa na; Sylvester M. Rapahel (Afisa Habari)
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera
NOVEMBA 01, 2018.

Post a Comment

0 Comments