habari Mpya


Mbunge akabidhi Vifaa Tiba Vya Milioni 36.5 Kuboresha Sekta ya Afya Kahama.

Na Simon Dioniz -RK Kahama 97.3 Fm.

Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga Mhe. Azza Hilal Hamad (CCM) amekabidhi msaada wa Vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 36.5 kwa ajili ya vituo vya afya na zahanati sita zilizopo katika halmashauri ya wilaya ya Ushetu,Msalala na Kahama Mji wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

 Mhe. Azza amekabidhi vifaa tiba hivyo Jana Jumanne Oktoba 16,2018 kwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama,Bw.Anamringi Macha wakati wa Kikao cha Baraza la UWT wilaya ya Kahama uliofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Kahama.

Vifaa tiba hivyo ni pamoja na SHUKA 100,MASHINE ZA KUPIMA DAMU,WINGI WA DAMU,SUKARI,JOTO,MAPIGO YA MOYO NA VIFAA VYA KUSAIDIA KUJIFUNGUA KWA AKINA MAMA ambavyo kupatikana kwake kumetokana na jitihada za Mbunge huyo kuhakikisha vifo vya mama na mtoto vinapungua mkoani Shinyanga.

Awali akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa tiba hivyo,Mhe. Azza Hilal amesema kupitia Kampeni yake ya ‘AFYA YANGU MTAJI WANGU’ na kuwajali akina mama aliamua kutafuta wadau kwa ajili ya kusaidia kumaliza changamoto ya uhaba wa vifaa tiba katika vituo vya afya na zahanati.

“Nawashukuru sana Bahari Pharmacy Ltd na Brett &Beileys kwa kunishika mkono na kuchangia kupatikana kwa vifaa hivi ambavyo leo navikabidhi ili vikatumike kwenye zahanati na vituo vya afya kwani hatutaki kuona vifo vya mama na mtoto”,alieleza Azza.

Alivitaja vituo vya afya vitakavyonufaika na msaada huo kuwa ni Mwendakulima,Mbika na Lunguya na zanahati ambazo ni Ngogwe,Kisuke na Bulige.
Akipokea vifaa tiba,Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha alimshukuru Mbunge huyo kwa msaada huo na kubainisha kuwa ameunga mkono kwa vitendo ilani ya CCM na juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli katika kuboresha sekta ya afya.

Kwa Upande wake Mbunge wa Jimbo la Ushetu,Mhe.Elias Kwandikwa ambaye ni Naibu Waziri wa Ujenzi aliahidi kumuunga mkono Mhe. Azza kwa kutoa msaada wa vifaa tiba katika vituo vitatu vya afya wilayani Kahama.
Vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 36.5 kwa ajili ya zanahati na vituo vya afya wilayani Kahama vilivyotolewa na Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Azza Hilal Hamad (CCM) kwa kushirikiana na wadau wake Bahari Pharmacy Ltd na Brett &Beileys.
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Azza Hilal Hamad akikabidhi shuka ikiwa ni sehemu ya shuka 100 alizotoa kwa ajili ya vituo vya afya na zahanati wilayani Kahama. 
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Azza Hilal Hamad akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa UWT Wilaya ya Kahama mkoani Shinyang'a.

Post a Comment

0 Comments