habari Mpya


Ziara ya RC Kagera Ngara, Itaka Kamati ya Ulinzi na Usalama Kufuatilia Uuzwaji wa Kahawa Vyama vya Ushirika.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Bw.Marco Gaguti ametembelea kiwanda cha Ngara Coffe akiongozwa na Mkurugenzi wa kiwanda hicho Bw.Abdallah Seif aliyetoa taarifa ya mikakati ya kiwanda hicho kuboresha huduma za kusaga na kukoboa kahawa wilayani Ngara.

Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya Bw.Michael Mtenjele na Katibu Tawala Wilaya Bw.Vedastus Tibaijuka.

Habari / Picha Na  Shaaban Ndyamukama –RK Ngara.

 Kamati ya ulinzi na Usalama ya wilaya ya Ngara mkani Kagera imetakiwa kufuatilia uuzwaji wa zao la kahawa katika vyama vya ushirika badala ya kuuzwa kwa magendo kuelekea nchi za jirani.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Bw. Marco Gaguti ameagiza kamati hiyo  Sept 9,2018  akitaka kuwekwa ulinzi kwenye vituo vya mipakani kudhibiti magendo ya kahawa kwa kuwa zao hilo limewekwa katika  mazao ya   kimkakati  kukuza uchumi wa Taifa.

Bw.Gaguti alisema katika uuzwaji wa zao hilo wanachama wa ushirika walipwe mapema fedha za awali wakati ukifanyika mchakato wa kuwalipa awamu ya pili baada ya kuuzwa kwenye mnada mkoani Kilimanjaro.
Akisoma taarifa ya hali ya uuzaji wa kahawa wilayani Ngara, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilayani hivyo Bw.Aidan Bahama amesema changamoto zilizopo ni uchakavu wa miundombinu katika chama cha wakulima cha Ngara Farmers.

Bw.Bahama alisema ghala la chama hicho limechakaa na hakuna machine ya kusaga wala kukoboa na kulazimika kusafirisha kahawa hadi kwenye kiwanda cha Ngara Coffee  kwa kukodi na kutumia gharama kubwa za uendeshaji. 

Alisema pia wazabuni waliosaini mkataba na chama hicho kuleta magunia ya kuhifadhi kahawa hawajaleta kwa wakati na kwamba vituo vya mauzo vingine viko mbali hivyo wakulima kutembea umbali mrefu kuzisafirisha mpaka vijiji jirani.

"Bajeti iliyopitishwa na mrajisi ni ndogo ukilinganisha na kahawa itakayopatikana  hadi sasa zimekusanywa tani 909.22 pia tuna  ukosefu wa magari ya kusafirisha kahawa kutoka kwenye vituo vya mauzo huko vijijini" Alisema Bw.Bahama.

Alisema kupitia wakala wa barabara za vijijini na mijini (Tarura) wameboresha barabara kwa kujenga madaraja na kuzipanua kurahisisha magari kupita  kupunguza usumbufu kwa wakulima wazee wanaohitaji kuuza kahawa yao.  
Kiwanda Ngara Coffee kimetenga Shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya uboreshaji miundombinu yake ambapo  kimenunua mashine ya kusaga na kukuboa  tani 18,000 kwa mwaka kutoa ajira za kudumu watu kuanzia 1,200 mpaka 1,800 na vibarua wa muda 500.

Mkuu wa mkoa anatembelea wilaya zote za mkoa wa Kagera akijitambulisha huku akikagua miradi ya maendeleo hususan Sekta ya Afya na  Kilimo pamoja na kuzungumza na Wafanyakazi wa Halmashauri hizo.

Post a Comment

0 Comments