Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amefanya ziara ya kushtukiza katika Kituo
cha Polisi Katoro mkoani Geita na kuwahoji watuhumiwa wa makosa
mbalimbali waliokuwepo katika mahabusu kituoni hapo.
Waziri Lugola
ambaye alikua safarini kuelekea Mkoani Kigoma kwa ziara yake ya kikazi, ghafla
aliibukia katika kituo hicho akitaka kujua utendaji kazi wa polisi pamoja na
makosa mbalimbali wanayowakabili watuhumiwa waliopo katika mahabusu hiyo na pia
kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili askari wa kituo hicho.
Waziri Lugola
aliowasili kituoni hapo jana mchana na akaelekea moja kwa moja mahabusu na
akaomba kitabu cha taarifa ya makosa mbalimbali yaliyoripotiwa kituoni hapo, na
akamuelekeza askari wa zamu awapange foleni watuhumiwa hao ili aweze kuwahoji
makosa yao na pia Mkuu wa Kituo cha polisi hicho, aweze kufafanua makosa yao.
Baada ya
watuhumiwa hao, Waziri Lugola licha ya kuwapongeza polisi wa kituo hicho kwa kufanya
kazi vizuri, pia alimtaka Mkuu wa Kituo hicho, Steven Kimaro kua makini na utendaji
wake na kuwafuatilia kwa umakini utendaji kazi wa askari wake kwasababu yeye
ndio kiongozi wa kituo hicho.
“Sipendi
wananchi waonewe, haki itendeke na si kila kosa lazima mtuhumiwa awekwe
mahabusu, tumieni busara umakini ili tuweze kutenda haki na pia nataka jeshi
hili liwe na picha nzuri zaidi kwa jamii,” alisema Lugola.
Pia
alifafanua kua, hataki kusikia askari polisi anatuhumiwa kwa rushwa au
kunyanyasa wananchi, na endapo taarifa hizo zitamfikia basi atahakikisha askari
huyo anachukulia hatua za kisheria.
Aidha,
Waziri Lugola alitaka polisi wa usalama barabarani kufuata sheria na pia si
kila kosa lazima mwenye gari kuandikiwa risiti ya malipo, makosa mengine watoe
elimu zaidi kwa madereva hao ili taifa liweze kusonga mbele.
Waziri Lugola, leo Septemba 25 anatarajia kuanza ziara yake ya kutembelea mikoa yote nchini,
ambapo ataanza ziara katika Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma ambapo atazungumza
na askari na maafisa polisi, watumishi wa taasisi zilizopo katika wizara yake
na baadaye atafanya mkutano wa hadhara kwa kuzungumza na wananchi pamoja na
kusikiliza kero zao mjini humo.
|
0 Comments