habari Mpya


Wananchi Wafurahia Huduma za Kituo Cha Afya Nyakanazi.

Na: Sylvester Raphael.

Wananchi wa Nyakanazi Wilayani Biharamulo waanza kunufaika na Kituo cha Afya Nyakanazi baada ya Serikali kutoa Shilingi milioni 500 za kuboresha na kukarabati Kituo hicho kinachotoa huduma za afya kwa Wananchi 19,172 ambapo Uongozi wa Halmashauri kwa kushirikiana na Wananchi wameweza kujenga majengo mapya na kukarabati ya zamani ili kuboresha huduma za afya katika jamii hiyo.

 
Ushuhuda huo ulitolewa na akina mama wazazi katika wodi ya wazazi kituoni hapo mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti kufika kituoni hapo Septemba 7, 2018 kutembelea na kukagua ubora wa majengo yaliyojengwa  lakini pia thamani ya fedha za Serikali katika ujenzi huo.

Kwa niaba ya akina mama wazazi waliokuwa wamepumzishwa katika wodi ya wazazi mara baada ya kujifungua vichanga vyao  Bi Schola Elias (30) alimweleza Mkuu wa Mkoa wa Kagera, kuwa wanafurahia huduma za kituo hicho kwa kuboreka baada ya Serikali  kuleta fedha za kujenga majengo mapya hasa chumba cha kujifungulia akina mama wajawazito na wodi ya wazazi pamoja  na ukarabati majengo ya zamani.

Kipindi cha nyuma chumba cha kujifungulia kilikuwa na vitanda vya wazazi viwili tu jambo liloleta usumbufu mkubwa sana lakini baada ya ujenzi mpya kuna vitanada vitano jambo ambalo linapelekea hata sisi akina mama wajawazito watano tunaweza kujifungua kwa wakati mmoja. Aidha, wodi yetu ya zamani ilikuwa ina vitanda vinane tu lakini sasa kama unavyoona kuna vitanda vya kupumzikia baada ya kujifungua 25 na tunapuzishwa baada ya kujifungua hakuna mama anakosa kitanda.” Alieleza Bi Schola.
Ziara ya Mkuu huyo wa Mkoa wa Kagera katika kituo hicho cha Nyakanazi wilayani Biharamulo imefanyika Septemba 7, 2018 na hadi Mkuu wa Mkoa Gaguti alipowasili katika Kituo hicho majira ya saa 8:00 mchana walikuwa wamejifungua akina mama tisa watoto wa kike wakiwa sita na wa kiume wakiwa watatu. 

Katika hatua nyingine Bi Pili Ndamulo, Afisa Muuguzi Msaidizi ambaye ni Msimamizi wa wodi ya wazazi katika Kituo hicho alisema kuwa wastani kwa wiki wanajifungua akina mama 30 hadi 40 na kwa mwezi ni akina mama 100 hadi 120.

Naye Mkuu wa Mkoa Gaguti akiongea na wananchi katika Kituo cha Nyakanazi mara baada ya kukikagua aliwataka wananchi hao kukitunza Kituo hicho, Pili aliwataka watumishi katika kutoa huduma zinazoendana na ubora wa majengo ya Kituo, Tatu wananchi kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa EBOLA kwani Nyakanazi inazo njia kuu mbili zinazoelekea nchi jirani za Burundi, Rwanda na Kongo DRC, Mwisho aliwataka wananchi wote kujiunga na bima ya afya kwajili ya matibabu yao.

Majengo yaliyojengwa katika Kituo cha Afya Nyakanazi ni pamoja na Wodi ya Watoto, Wodi ya Akina Mama Wazazi, Nyumba ya Watumishi wawili, Chumba cha kuhifdhia maiti, Jengo la kujifungulia,  Njia za kutembelea na Kichomea taka. 

Aidha, majengo yaliyokarabaitiwa ni pamoja na Jengo la wagojwa wa nje, Jengo la upasuaji na Mahabara. 

Ujenzi huo umefanyika kwa jumla ya zaidi ya shilingi milioni 566 fedha hizo zikijumuisha fedha za Serikali Kuu, Halmashauri ya Wilaya pamoja na Wananchi wa Nyakanazi.

Post a Comment

0 Comments