habari Mpya


Mtihani wa Darasa la Saba , Kagera Matarajio Ni Mkoa Kushika Nafasi Ya Kwanza Kitaifa – RC Gaguti

Mwanafunzi wa Darasa la Saba Shule ya Msingi Tumaini Manispaa ya Bukoba Akiendelea Kufanya Mtihani wa Somo la Kiingereza.
Mkuu wa Mkoa Kagera Mhe. Gaguti Akiangalia Ratiba ya Mtihani Wa Darasa la Saba Shule ya Msingi Mafumbo Manispaa ya Bukoba.
Wanafunzi wa Darasa la Saba Wakiendelea Mtuhani wa Kuhitimu Elimu ya Msingi .
Wanafunzi wa Darasa la Saba Wakiendelea Mtuhani wa Kuhitimu Elimu ya Msingi.
Mkuu wa Mkoa Kagera Mhe. Gaguti Akiongea na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Tumaini Augustina Daniel Kujua Kama Kuna Changamoto Yoyote Iliyojitokeza Katika Shule Yake.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Gaguti Mara Baada ya Kukagua na Kujiridhisha na Maendeleo ya Namna Mtihani unavyfanyika Anasaini Kitabu cha Wageni Shule ya Msingi Mafumbo.

Na: Sylvester Raphael.

Mkoa wa Kagera ukiwa mkoa mmoja wapo kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara ambapo  wanafunzi wake wa Darasa la Saba  Wavulana 22,129 na Wasichana 25,099 jumla 47,228 wanafanya mtihani wa kuhitimu Elimu ya Msingi maandalizi kuanzia kuwaandaa wanafunzi, Mapokezi ya Mtihani hadi siku ya kwanza ya kufanya mtihani Septemba 5, 2018 na mtihani huo kufanyika hali ni shwari na mtihani umefanyika kama ilivyopangwa. 

Kikiwa kipaumbele chake cha kwanza kuhakikisha Mkoa wa Kagera unaendelea kufanya vizuri na kushika nafasi za juu kabisa Kitaifa tangu kuripoti kwake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti alipata nafasi ya kutembelea baadhi ya shule katika Manispaa ya Bukoba ili kuona mitihani hiyo kama inaendelea kufanyika kama Mkoa ulivyojiandaa na kujipanga ifanyike.

Baada ya kutembelea shule za Msingi kadhaa katika Manispaa ya Bukoba ikiwemo Shule za Msingi Tumaini na Mafumbo na kuongea na wasimamizi wakuu wa vituo na Walimu Wakuu wa Shule hizo Mkuu wa Mkoa Gaguti aliridhika na maendeleo ya wanafunzi wanavyofanya mtihani pia na usimamizi unavyoendelea kuimarishwa kuhakikisha hakuna udanganyifu wowote.

Hadi sasa hakuna changamooto yoyote katika Mkoa wetu wa Kagera ambayo nimeipokea kuhusu kufanyika kwa Mitihani ya Darasa la Saba, aidha, na mimi mwenyewe nimepita katika shule kadhaa kuona namna zoezi hili linavyoendelea, naona wahusika wote pamoja na wanafunzi wanaendelea na majukumu yao bila wasiwasi.” Alifafanua Mkuu wa Mkoa Gaguti.

Pia Mkuu wa Mkoa Gaguti alitoa rai kwa watendaji wote waliokabidhiwa jukumu la kusimamia Mitihani ya Darasa la Saba kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa kusimamia Mitihani hiyo kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu hadi mitihani itakapokamilika na kukabidhiwa mahali panapohusika bila kujihusisha na vitendo vyovyote vya hujuma vinginevyo sheria itachukua mkondo wake.

Ufaulu wa Mitihani ya Darasa la Saba Mkoa wa Kagera: Kwa ujumla Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa Mikoa inayofanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba. 

Mwaka 2017 ulishika nafasi 3 kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara ikilinganishwa na nafasi ya 5 mwaka 2016 kati ya Mikoa 26 ya Tanzania Bara pia ikilinganishwa na nafasi ya 7 mwaka 2015 kati ya Mikoa 25 na nafasi ya 8 mwaka 2014 kati ya Mikoa 25

Mkuu wa Mkoa Gaguti amewatakia heri na ufaulu mzuri wanafunzi wote wanaofanya Mtihani wa Darasa la Saba Mkoani Kagera na kusema kuwa imani yake mwaka huu Mkoa wa Kagera utongoza Kitaifa kwa kushika nafasi ya kwanza Kitaifa.   

Jumla ya Shule 953 Katika Mkoa wa Kagera 890 zikiwa za Serikali na 63 Binafsi zenye watahiniwa jumla 47,228 zinafanya Mtihani wa Darasa la Saba.

Post a Comment

0 Comments