habari Mpya


Kikundi cha TUFASHANYWE Chawezeshwa Mashine ya Kuchakata Mihogo Kibondo.

Na James Jovin -RK Kibondo.

Kikundi cha Ujasiriamali cha TUFASHANYWE kilichoko kijiji cha Kisogwe kata ya Busunzu wilayani Kibondo Mkoani Kigoma kimewezeshwa mashine ya kuchakata zao la Muhogo yenye thamani ya shilingi milioni 3.6  kupitia mradi wa SAKIP chini  ya Shirika la ENABEL la nchini Uberigiji kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.

Kikundi hicho kimepatiwa mashine hiyo ya kisasa yenye uwezo wa kuchakata zaidi ya kilo 300 za Muhogo  kwa saa baada ya kukidhi vigezo na masharti na kuonekana kuwa ni kikundi imara kinachoweza kuendeleza mradi huo na hatimaye kuwa kiwanda kikubwa.
Mshauri wa maswala ya Jinsia na Mafunzo katika mradi huo  Bw. Paschal Tekwi amevitaka vikundi vya Ujarisiamali kuongeza jitihada zaidi katika kuzalisha zao la muhogo ili vikundi hivyo viweze kupatiwa mashine za kuchakata zao la muhogo na kutafutiwa masoko ya bidhaa hiyo ili waweze kujiinuka kiuchumi.

Kwa upande wake mshauri wa maswala ya kilimo katika mkoa wa Kigoma Bw.Joseph Rubuye amewataka wanakikundi hao kuitangaza mashine hiyo ya kuchakata muhogo kwa wananchi ili waweze kuitumia katika kuchakata mazao hayo ya muhogo na kupata bidhaa bora na si kuuza malighafi ambazo hupewa fedha kidogo na walanguzi na hivyo kubaki katika umasikini.
Katika kuendeleza  kikundi hicho kinayo mikakati mbali mbali kinayotarajia kufanya katika msimu ujao ikiwemo kulima kwa kutumia pembejeo za kilimo ili kupata tija na faida kwa kuongeza thamani ya mazao na wingi wa mazao hali itakayosaidia upatikanaji wa malighafi za kutosha.

Kwa upande wake katibu tawala wa wilaya ya Kibondo Bw. Ayubu Sebabili akimwakilisha mkuu wa wilaya ya Kibondo Bw.Luis Bura wakati wa kukabidhi mashine hiyo kwa wanakikundi amewataka wananchi kote wilayani Kibondo kujikita katika kulima zao la muhogo kwa kuwa ni zao lenye tija na tayari limepewa kipaumbele na Serikali.
Iwapo kikundi hicho kitaona kuwa mradi huo wa mashine ya kuchakata zao la muhogo unafaida basi watalipia asilimia 15 za gharama ya mashine hiyo na fedha inayobaki watalipia ndani ya miezi 24 baada ya kukabidhiwa ili waweze kuendeleza viwanda vidogo vidogo na hatimae kukuza uchumi wa kikundi chao na wana kikundi kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments