habari Mpya


Waziri Jaffo- Apongeza Ushirikiano wa Wananchi Nyakanazi Biharamulo Katika Kutekeleza Miradi Ya Maendeleo.

Na: Sylvester Raphael.

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Seleman Jaffo awapongeza wananchi wa Kata ya Nyakanazi Wilayani Biharamulo Mkoani Kagera kwa ushirikiano wao wa kuchangia na kushiriki katika kutekeleza miradi ya maendeleo hasa ujenzi wa Kituo cha Afya Nyakanazi ambacho kimekamilika ujenzi wake baada ya Seriakli kutoa Shilingi milioni 500 ili kiweze kuboreshwa na kutoa huduma muhimu za afya kwa wananchi.

Waziri Jaffo aliyasema hayo Agosti 9, 2018 alipofanya ziara ya siku moja na kutembelea na kukagua ujenzi wa kituo hicho ambapo alisema kuwa amaeridhishwa na ujenzi ulivyofanyika kuwa ni kiwango kinachoridhisha na thamani ya fedha iliyotolewa inaonekana katika majengo yaliyojengwa na mengine kukarabaitiwa.

Nawapongeza wananchi wa Kata ya Nyakanazi kwa kujitoa kushirikiana na Serikali kuhakikisha kituo hiki cha Nyakanazi kinajengwa na kukamilika, nyinyi wananchi mmekuwa mstari wa mbele kutekeleza wajibu wenu pale mlipotakiwa kufanya hivyo na ndiyo maana kituo chenu kimekalika.” Alifafanua Waziri Jaffo.
Waziri Jaffo alizidi kusisitiza kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wake wananpata huduma bora hasa akinamama wajawazito katika suala la upasuaji wakati wa kujifungua sasa tatizo hilo limefika mwisho baada ya kituo hicho kukamilika.


 Aidha, Waziri Jaffo aliongeza kuwa Serikali baada ya kuridhishwa na ujenzi ulivyotekelezwa katika kituo hicho imetoa tena shilingi milioni 400 nyingine za kujenga kituo kingine katika Halmashauri ya Wilaya Hiyo ya Biharamulo.

Pamoja na kuupongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo Waziri Jaffo alitoa tahadhari kwa Halmashauri hiyo kusimamia mapato ambapo alisema Biharamulo haifanyi vizuri katika kukusanya mapato.

Pia aliagiza kuitishwa kwa Balaza Maalum la Madiwani ili kujadili ripoti ya Tume ya uchunguzi ilioundwa kuchunguza mapato yanavuja wapi na kama ikigundulika kuna watumishi waliohusika wachukuliwe hatua mara moja naye apewe taarifa.
 

Kituo cha Nyakanazi kimekamilika ujenzi wake kwa jumla ya shilingi milioni 700 ikiwa shilingi milioni 500 zilitolewa na Serikali kujenga majengo ya Wodi ya akinamama na watoto, Wodi ya watoto, chumba cha kuhifadhi maiti, Nyumbambili (Two in one) za watumishi na kukarabati chumba cha upasuaji. 

Pia shilingi milioni 200 zilitumika kununua vifaa katika kituo hicho.

Waziri Jaffo alimaliza kwa kusema kuwa Serikali itajenga vituo vyote vya afya Wilayani Biharamulo ili wananchi wote wapate huduma safi, pia alisema wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani mwaka 2015 kulikuwa na Vituo vya Afya 115 tu lakini hadi sasa vimejengwa vituo 210 na tayari vituo 97 vimepewa fedha kujengwa, hayo ni mafanikio na mapinduzi makubwa katika Sekta ya Afya.

Post a Comment

0 Comments