habari Mpya


Mkuu wa Mkoa wa Kagera Aipongeza Serikali ya Rwanda kwa Kusaidia Kuudhibiti Moto Rusumo.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigadia Jenerali Marco Gaguti, amewapongeza wananchi na serikali ya Rwanda, kwa kuudhibiti moto uliosababisha kifo cha mtu mmoja, na kuteketeza magari sita mpakani Rusumo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara Agosti 19, 2018.

Brigadia Jenerali Gaguti, ametoa pongezi hizo jana mpakani Rusumo wakati akiongea na waandishi wa habari, kwamba anaipongeza serikali ya Rwanda, iliyotoa magari mawili ya zimamoto na helkopta moja, kwa ajili ya kuzima moto huo.

Moto ulionza majira ya saa moja asubuhi umesababishwa na gari la kampuni ya Lake Oil lenye namba za usajili T 578 CPM, lililofali breki na kuyagonga magari yaliyokuwa katika yadi ya Rusumo, na kusababisha moto uliopelekea magari sita kuungua pamoja na trekita moja.” alisema Brigadia Jenerali Gaguti.

Aidha, ametoa pole kwa familia ya aliyekuwa dereva wa gari la Lake Oil aliyepoteza maisha, kwamba anawatakia wawe na moya wa vumilivu na wananchi wa Rusumo waliofadhaishwa na tukio hilo.

Amekiri kwamba kulikuwa na mapungufu ya kukosa nyenzo za kukabiliana na majanga kama moto; huku akiahidi kwamba atakaa na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya na ya Mkoa, ili kwa pamoja watafute suluhisho la kudumu.

Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Magharibi wa Rwanda Ndugu Mufulukye Fred, Mkuu wa Wilaya ya Kirehe Bw.Mzungu Gerald amesema tukio hilo ni somo kwa Wananchi wa nchi za Rwanda na Tanzania.

Kuna haja sasa ya nchi zetu mbili kukaa pamoja na kutafuta suluhisho la majango haya, ili siku nyingine yasisababishe hasara kama hii, nashukuru kwamba jitihada zetu, zimezaa matunda chanya kwani moto umedhibitiwa” Alisema Bw. Muzungu.

Viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Ngara walihudhuria tukio hilo akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Afisa Tawala, Afisa Usalama (W) pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Magharibi wa Rwanda, na Mkuu wa Wilaya ya Kirehe.

Post a Comment

0 Comments