habari Mpya


Majengo Mapya ya Shule ya Sekondari Ihungo mkoani Kagera.

Muonekano wa Majengo kwa sasa ya  Shule ya Sekondari Ihungo na hapa ukamilishwa wa baadhi ya miundombinu midogomidogo katika majengo hayo baada ya Serikali kuamua na kuijenga upya shule hiyo iliyoharibiwa vibaya na Tetemeko la Ardhi lililotokea Mkoani Kagera Septemba 10, 2016.

Shule hiyo ya Ihungo sasa imejenga upya na kukarabati baadhi ya majengo  kwa gharama ya shilingi bilioni 10.45 na kuifanya shule hiyo iwe shule bora na ya kisasa nchini inayovutia elimu bora kwa wanafunzi.
Mara baada ya Shule ya Sekondari Ihungo kukamilika ujenzi wake kwa asilimia zaidi ya 90% Serikali tayari imewarudisha Wanafunzi walikokuwa wamehamishiwa katika Shule ya Sekondari Omumwani  katika Manispaa ya Bukoba na Chuo cha Ruhija Halmashauri ya Wilaya Bukoba ili wakaendelee na masomo yao katika shule yao ya Ihungo Sekondari.

Katika kukamilisha ujenzi wa miundombinu midogo midogo iliyobakia katika katika shule hiyo Mkuu wa Mkoa wa Kagera , Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti alipotembelea Shule hiyo August 25, 2018 , alisema kuwa yeye jukumu lake ni kufuatilia na kuhakikisha kila kilichopangwa kujengwa katika shule hiyo lazima kijengwe na kukamilshwa na Kampuni ya Tanzania Building Agency (TBA).

Tetemeko la Ardhi Mkoani Kagera lilisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu yote ya Shule ya Sekondari Ihungo  ikiwemo Madarasa, Mabweni, Maabara, Bwalo, Jiko, Vyoo na Mabafu, Nyumba za Walimu, Jengo la Utawala, Kanisa, Msikiti, Maktaba na Mifumo ya maji na umeme. 
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejenga majengo matatu ya madarasa yenye ghorofa moja kila moja, kila jengo lina vyumba 8 vya madarasa na ofisi 4 na kufanya jumla ya vyumba vya madarasa 24 yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 960 na jumla ya ofisi 12.

Serikali pia imejenga majengo 3 ya mabweni yenye ghorofa 2 kila moja, kila jengo lina uwezo wa kuchukua wanafunzi 384; hivyo majengo yote 3 ya mabweni yatachukua wanafunzi 1,152, vikiwemo vyoo na mabafu. Serikali pia inajenga nyumba mpya za wafanyakazi kwa matumizi ya familia 30.

Aidha, Serikali imefanya ukarabati wa Maktaba ya Shule, Jengo la Utawala, Maabara ya Kompyuta, Jengo la Kilimo, Bwalo, Jiko na Maabara za Fizikia, Kemia na Baologia.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti atembelea Shule ya Sekondari Ihungo na kuona maendeleo ya ukamilishwa wa baadhi ya miundombinu midogomidogo katika majengo baada ya Serikali kuamua na kuijenga upya shule hiyo iliyoharibiwa vibaya na Tetemeko la Ardhi lililotokea Mkoani Kagera Septemba 10, 2016.
Tayari Shule ya Sekondari Ihungo imepangiwa wanafunzi 679 wa Kidato cha Tano na tayari wanafunzi  556 wameripoti shuleni hapo tangu tarehe 16/7/2018 na wanafunzi hao ni wa michepuo ya PCB, PCM, CBG, EGM na HGE  na wanaendelea na masomo kadri ratiba ya shule ilivyopangwa.

Ikumbukwe kuwa Shule Sekondari Ihungo awali kabla ya Tetemeko kutokea ilikuwa ina uwezo wa kubeba wanafunzi 801 na kwasasa baada ya kujengwa upya inao uwezo wa kubeba wanafunzi 1,152.

Post a Comment

0 Comments