habari Mpya


Vinara kwa Utoro Shuleni -Bukiriro, Shunga, Kibogora, Muganza na Rusumo.

Wakuu wa Shule za Sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara mkoani Kagera wametakiwa kuweka mikakati ya kupunguza Utoro wa Wanafunzi ili kuinua kiwango cha kufaulu wilayani humo.

Afisa Elimu Takwimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara Bw. Zacharia Mkumbo,ameyasema hayo  wakati wa kikao kazi cha Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari, kilichoandaliwa na Idara ya Elimu Sekondari kilichofanyika Shule ya Sekondari Ngara Julai 12, 2018.

Kama Wakuu wa Shule tujiwekee mkakati wa kukomesha utoro ili takwimu za kufikia Machi mwaka kesho,2019 zishuke, kwa sababu hadi sasa kila mmoja wetu anajua yuko wapi na anatakiwa kufanya nini ili kutimiza azma hiyo.” Alisema Bw. Mkumbo.

Shule zinazoongoza kwa utoro ni Bukiriro yenye watoro 112, Shunga wanafunzi 80, Kibogora wanafunzi 58, Muganza wanafunzi 57,Shule nyingine ni Rusumo yenye wanafunzi 52.

Amewataka Wakuu hao wa Shule kuwahimiza Walimu wa Madarasa, kuripoti na kuwafuatilia Wanafunzi watoro na kuwarejesha shuleni, ili wasipoteze na kukosa haki yao ya msingi ambayo ni elimu.

Bw. Mkumbo amesema walimu wa madarasda ni zaidi ya wazazi kwani wana muda mrefu wa kukaa na wanafunzi; hivyo wanawajibika kuhakikisha wanafunzi wote wanahudhuria shuleni hadi watakapohitimu masomo yao.

Naye Kaimu Afisa Elimu Sekondari Bw. Marton James amewakumbusha Walimu Wakuu wakomeshe tabia ya baadhi ya walimu shuleni kwao, wenye tabia ya kuwatukana watoto kwa madai kwamba tabia hiyo inawakatisha tamaa Wanafunzi ,kwani hadi Machi 2018, wanafunzi wapatao 674 wameacha Shuleni na kutokomea kusikojulikana.

Nao Walimu Wakuu wameishukuru ofisi ya elimu sekondari kwa kuandaa kikao hicho ambacho kwao kimekuwa cha manufaa kwani wameweza kushirikishana kimawazo; huku wakikemea pale pasiponyooka.

Post a Comment

0 Comments