habari Mpya


Mh. Ndugulile- Simamieni Ubora wa Huduma Katika Hospitali Zetu.

Wasimamizi wa vituo vya afya na hospitali katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, wametakiwa kusimamia utoaji wa huduma bora ya afya, na kwamba vituo ambavyo havitakidhi vigezo, vitashushwa au kufungwa kabisa.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Faustine Ndugulile (MB), ameyasema hayo wakati akiongea kwa wakati tofauti na wafanyakazi wa hospitali za Nyamiaga na Murugwanza Julai 29, 2018.

Amesema lengo la ziara yake iliyoanza Julai 16, 2018, katika mikoa Sita ya Mara, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Geta na kuhitimishwa mkoani Kagera, kuangalia shughuli mbalimbali, na kutunuku vyeti kwa vituo vya afya na watu waliofanyakazi vizuri.

“Tutaweka vigezo vya kuainisha ubora wa kituo cha afya; tukikuta kituo cha afya kimeshuka yaani hakina viwango, kama kilikuwa kituo cha afya kinakuwa zahanati; pia hospitali ya wilaya tunaweza tukaishusha au kuifunga kabisa ikiwa haina vigezo stahiki.” Alisema Mh. Nduglile.

Amesema Wizara ina mpago wa kusajili na kuvipatia leseni vituo vya afya na hospitali zote za serikali na za binafsi, ikionekana kituo hakina vigezo, kitafungwa  na msimamizi itabidi aeleze ni kwa nini wananchi hawapati huduma.

Amefafanua kwamba kinachotakiwa ni uwajibikaji na usimamizi mzuri, na kuongeza kwamba ikiwa usimamizi utakuwa mzuri, mapungufu yataisha, na wananchi watapata huduma bora ya afya.

Wizara inalenga kuweka vigezo vya ubora wa utoaji huduma ya afya; kwa hiyo ni jukumu la kila msimamizi katika eneo lake, kuhakikisha kwamba anatimiza wajibu wake, ikishindikana itabidi kituo kifungwe.

Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Ngara bado haijapiga hatua stahiki, kwani tathimini inaonesha kwamba mwaka 2016, ni asilimia 2% tu ya vituo vya afya ndivyo vilikuwa na nyota tatu, na kwamba katika tathimini nyingine Halmashauri imepata 26% ambapo kiwango cha chini cha serikali ni 80%.

Amewataka watendaji kuongeza kasi katika kuwahamasisha akina mama wajawazito, kuhudhuria kliniki, pia wasisitize suala la lishe, kwa madai kwamba kiwango cha ubora wa huduma katika maeneo hayo bado ni cha chini ikilinganishwa na kile cha taifa.

Aidha, amewapongeza wafanyakazi wa hospitali teule ya Murugwanza, kwani hospitali hiyo kadili ya tathimini ya Julai 2018 wilayani Muleba ina nyota nne, na imeibuka ya kwanza katika mkoa wa Kagera.

Katika ziara hiyo Mh. Ndugulile aliambatana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Dr. Marco Mbata, aliyewasisitiza Wafanyakazi katika vituo vyote vya afya na hospitali wilayani Ngara, kuondoa mapungufu aliyoyaona waziri, ili vituo vyote mwakani viwe na nyota tatu na kuendelea. 

Post a Comment

0 Comments