habari Mpya


MBUNGE NGARA ATEMBELEA SEHEMU ZA KUWEKWA VIVUKO WILAYANI HUMO

Shaaban Ndyamukama, RK-Ngara 
Ngara. Serikali  imeanza mchakato wa kutafuta kivuko cha kuwasafirisha wakazi wa vijiji vya Mayenzi kata ya Kibimba na Kanyinya  kata ya Mbuba wilayani Ngara  mkoani Kagera walioko jirani na mto Ruvubu kuharakisha usafiri  wa kwenda kutafuta huduma za kijamii na kufanya shughuli za kiuchumi

Mbunge wa jimbo la Ngara (CCM) Alex Gashaza amebainisha hayo  leo Julai 21, wakati alipoambatana na wataalamu wa miundombinu ya majini na nchi kavu katika mpaka wa vijiji hivyo kubaini njia za kupitisha kivuko kwenye mto huo

Gashaza amesema wananchi wa vijiji vya kata za kibimba na Mbuba wamekuwa wakihangaika kuvuka mto Ruvubu kwenda sehemu nyingine  na kupoteza maisha kwa kutumia mitumbwi ambayo sio salama kwenye mto huo.

Amesema kufuatia kuvuka kwa kutumia mitumbwi iliyochakaa  imesababisha kuwepo kwa vifo vya watu 13 katika miaka tofauti kwa vijiji hivyo waliokuwa wakivuka kwenda kila ng’ambo ya mto kutafuta huduma za kijamii

 “Wanaopita ni wanafunzi wa  shule za msingi pia  wajawazito  wanaokwenda kutafuta huduma za matibabu ambapo  kipindi cha masika watoto hawaendi shule zikitumika gharama kubwa kupita nchi kavu kutafuta huduma”Amesema Gashaza

Aidha mhandisi Lukombe King’ombe ambaye ni Kaimu mkurugenzi wa huduma za vivuko vya serikali na ukodishaji mitambo kutoka wizara ya ujenzi  wakala wa ufundi na umemeTEMESA amesema kivuko kitakacholetwa ni kile kilichopo Kijiji cha Rusumo ambacho kitafanyiwa ukarabati ili kitumike kwenye eneo hilo

Amesema baada ya kujiridhisha wataalam wanakwenda kufanya tathimini ya gharama zitatakazotumika na kuweka  utaratibu wa kuchimba barabara kutoka makao makuu ya kijiji kwenye kwenye eneo la mto ulio na upana na mita 50 

Amesema mto huo unajaa maji kwa umbali wa mita 37 kila upande na kukiongeza upana wa mto huo maadalizi ni kuwa na kivuko kitakachosafiri umbali wa mita 124 badala ya kutumia mitumbwi ambayo ni hatari katika kusafirisha abiria majini

“Kivuko kitakachowekwa hapa kitafungwa mashine ya kutumia mafuta badala ya kukivuta kwa kamba wakitumia mikono kiweze kuharakisha ussafirishaji wa abiria na mizigo waweze  kufanya shughuli za kiuchumi” Alisema King’ombe

Pia amesema serikali itatafuta njia mbadala za kuweka boti kwenye kivuko cha mto Ruvubu katika mradi wa uzalishaji umeme wa maporomoko yam to Rusumo baada ya kilichokuwepo kushindwa kufanya kazi ambapo maji yejaa nchi kavu
Kivuko hicho kimeshindwa kuhudumia wananchi baada ya kuziba mifereji ya kusafirisha maji kwenda maporomoko ya Rusumo, panapojengwa bwawa la kuzalisha umeme wa megawati 80 kwa nchi za Rwanda, Burundi na Tanzania.

Awali diwani wa kata ya Kibimba John Shimimana amesema wananchi wakipata kivuko  kitapunguza gharama za usafirishaji abiria na mazao  kwenda hospitali ya Nyamiaga  umbali wa kilomita 12 badala ya kuzunguka kilomita50

Alisema njia hiyo itarahisisha wananchi wanaojihusisha na kilimo cha mazao ya chakula na biashara kupita kwa urahisi wakitumia hata pikipiki na magari kwenda sokoni katika magulio ya Ngara mjini Rulenge na kanazi kujiongezea mapato.

Hata hivyo Mwenyekiti wa kijiji cha Mayenzi Philipo Rutumbanya na mhandisi Masunzu Christopher kutoka wakala wa  barabara za vijijini na mijini TARURA wilayani Ngara  wamesema wananchi wanaandaa barabara ya kupitisha kivuko kitakachotolewa Rusumo kwenda kwenye mto unaounganisha vijiji vya kata hizo.  

Post a Comment

0 Comments