habari Mpya


Biharamulo yaongoza Kwa Kupata Nyota Nne Utoaji wa Huduma Bora za Afya Mkoani Kagera.

Na: Sylvester Raphael.
     
Halmashauri za Wilaya nne Mkoani Kagera zikiongozwa na Halmashauri ya Biharamulo zapata vyeti vya utoaji huduma bora za afya kwa wananchi katika Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati kwa kupata nyota kuanzia tatu na kuendelea baada ya tathimini iliyofanywa na  Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mwaka 2017.

 Vyeti hivyo vya huduma bora ya afya  vilitolewa na Naibu Waziri Dkt. Faustine Ndugulie Julai 28, 2018 Wilayani Muleba ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo iliongoza kwa kuwa na nyota nne Katika Hospitali Teule ya Wilaya na Zahanati ya Katoke kwa kupata asilimia 69% pamoja na cheti walipewa ngao ya mshindi wa kwanza.

Wilaya ya  Ngara  ilishika nafasi ya tatu kwa Hospitali ya Murugwanza kupata nyota nne na kupata asilimia 51%.

 Karagwe ilishika nafasi  ya nne kwa Hospitali Teule ya Wilaya Nyakahanga kupata nyota nne na kupata asilimia 51%. Halmashauri ya Wilaya ya Muleba ilishika nafasi ya tano kwa Zahanati ya Buganguzi kupata nyota tatu na kupata asilimia 17%
Katika tathmini ya mwaka 2017, wilaya ya Biharamulo imeendelea kushika nafasi ya kwanza, Muleba ilikuwa ya mwisho kwa tathmini ya mwaka 2016 kwa kutokuwa na kituo chochote kilichokuwa na nyota tatu lakini kwa mwaka 2017 imeshika nafasi ya pili kimkoa. 

Aidha, Muleba, Kyerwa, Halmashauri ya Bukoba  na Missenyi kwa tathmini ya mwaka 2016 zilikuwa nafasi ya mwisho ambapo hazikuwa na kituo hata kimoja chenye nyota tatu.
Akitoa vyeti hivyo Naibu Waziri Dkt. Ndugulile alizipongeza Halmashauri zilizopata ushindi na kuzisisitiza kuendelea kufanya vizuri ili zifikie nyota tano. 

Aidha, Dkt. Ndugulile alisema kuwa pamoja na ushindi huo lakini hakuna Halmashauri iliyofikia asilimia 80% kwa hiyo mkoa bado una kazi ya kufanya ili kuhakikisha kila Halmashauri inafikia kiwango cha kitaifa cha asilimia 80%.

Katika hautua nyingne Naibu Waziri Dkt. Ndugulile aliagiza Waganga Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanasimamia Madaktari na Watumishi wa idara ya Afya wanapotoa huduma kwa mgonjwa katika vituo kila mmoja kwa nafasi yake aandike muda aliomhudumia mgonjwa ili kuhakikisha mgonjwa anapata huduma kwa wakati na likitokea tatizo ajulikane ni yupi kafanya uzembe.

Naibu Waziri Dk. Ndugulile alimalizia hotuba yake fupi kwa kuzitaka Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya kuhakikisha zinasimamia dawa za Serikali zenye nembo ya “MSD” na “GOT” haziuzwi kwenye maduka binafsi na zikipatikana katika maduka binafsi wahusika wachukuliwe hatua za kisheria
Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhandisi  Richard Luyango kwa Niaba ya Serikali alishukuru Wizara ya Afya kwa kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi na kusisitiza kuwa viongozi wote Mkoani Kagera wataendelea kusimamia ili upatikanaji wa huduma bora zinapatikane na wananchi wapate huduma bora na kwa wakati.

Mwisho Mkuu wa Wilaya Luyango aliipongeza Halmashuri ya Wilaya ya Biharamulo kwa kupata ushindi wa kwanza katika mkoa na kuitaka Halmashauri hiyo kuendelea na uboreshaji wa huduma ili kuendelea kushika nafasi ya kwanza pia alizitaka Halmashauri zilizofanya vibaya kwenda kujifunza katika Halmashauri ya Biharamulo ili nazo ziweze kufanya vizuri.

Post a Comment

0 Comments