habari Mpya


Balozi wa Uholanzi Nchini Tanzania Akagua Miradi ya Maendeleo Inayofadhiliwa na Nchi yake Mkoani Kagera.

Na: Sylvester Raphael.

Balozi wa Uholanzi Nchini Tanzania Jeroen Verheul amefanya ziara ya siku mbili Mkoani Kagera kukagua miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na nchi ya Uholanzi katika kuinua uchumi na kipato cha wananchi ambao ni wakulima na wafugaji ili kuboresha maisha yao.

 Mara baada ya kuwasili ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Balozi Jeroem Verheul alisema kuwa lengo la ziara yake Mkoani Kagera ni kuja kuona fursa za uwekezaji katika biashara ya bidhaa za kilimo na mifugo kati ya nchi yake na Tanzania hasa bidhaa zinazoweza kupatikana ili zikauzwe nchini Uholanzi kutoka Mkoani Kagera.

 
Pia Balozi Jeroen alisema kuwa pamoja na kufadhili miradi ya Kilimo na Ufugaji katika Mkoa wa Kagera lakini pia nchi yake imefadhili na kujenga mradi wa kituo cha kufua umeme Wilayani Biharamulo pamoja na mradi wa kujenga barabara kwa teknolojia iliyotengenezwa nchini kwao yenye unafuu wa gaharama za matengenezo ya barabara za vijijini ukilinganisha na matengenezo ya kawaida.

Balozi Jeroen alisema teknolojia hiyo imetengenezwa nchini Uholanzi na Wilaya ya Biharamulo ilichaguliwa kama sehemu ya majaribio ambapo imetengenezwa barabara ya kilometa moja kwa teknolojia hiyo ya kuchanganya maji, udongo na vifaa vingine ambapo barabara hiyo inaweza kudumu kuanzia miaka kumi na kuendelea bila matengenezo makubwa.

 
Ziara ya Balozi Jeroen Verheul Mkoani Kagera na Wilayani Biharamulo ni pamoja na kutembelea na kukagua barabara iliyotengenezwa kwa teknolojia kutoka nchini Uholanzi ili kuona ufanisi wake, changamoto zilizopo na kuona namna bora ya kuboresha teknolojia hiyo ili itumike katika kutengeneza barabara nyingi katika Halmashauri za Wilaya nchini.

 
Aidha, akimkaribisha Mkoani Kagera Mkuu wa Mkoa Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu alimshukuru Balozi Jeroen kwa kuamua kuutembelea Mkoa wa Kageara pia na ufadhili wa nchi yake wa kufadhili miradi mablimbali katka Sekta za Kilimo, Ufugaji, Nishati na Miundombinu inayolenga kuinua uchumi wa Wananchi wa Mkoa wa Kagera. 

Mkuu wa Mkoa Kijuu aliitaja baadhi ya miradi ambayo nchi ya Uholanzi imekuwa ikiifadhi Mkoani Kagera kuwa ni Mradi wa Kuendeleza Wafugaji Kagera (Kagera Livestock Development Programme - KALIDEP) pamoja na mradi wa kuendeleza wafugaji wadogo wa ng’ombe wa maziwa vijijini.

Miradi mingine ikiwa ni pamoja na utoaji wa mbegu bora za ng’ombe wa kisasa wenye tija katika ufuaji wanaotoa maziwa kwa wingi pamoja na kutoa madawa mbalimbali ya kupambana na magonjwa ya mifugo ili ufugaji katika mkoa wa uwe wa tija.

Mkuu wa Mkoa Kijuu alisema kuwa ni matarajio ya Serikali ya Mkoa kuwa siku moja maendeleo ya wakulima na wafugaji katika Sekta za Kilimo na Mifugo Mkoani Kagera polepole yatafikia maendeleo ya Waholanzi katika sekta hizo kutokana na ufadhili wa nchi hiyo katika kuhakikisha Wananchi wa Kagera wanapiga hatua ya maendeleo.

Balozi Jeroen katika siku yake ya kwanza Julai 2, 2018 Mkoani Kagera alitembelea Manispaa ya Bukoba kuona ufugaji wa Samaki katika mabwawa mradi uliopo chini ya Cartas Tanzania pia alitembelea mradi wa Wafugaji wadogo wa Ng’ombe wa Maziwa Wilayani Missenyi. 

Katika Siku yake ya pili Julai 3, alitarajiwa kutembelea Wilaya ya Biharamulo kukagua mradi wa kituo cha kufua umeme na mradi wa utengenezaji wa barabara za vijijini kwa teknolojia kutoka Uholanzi.

 

Post a Comment

0 Comments