habari Mpya


Askofu Ruwa’ichi: Nimepokea kwa mshtuko mkubwa uteuzi wangu kutoka kwa Papa

MWANZA, NA AULERIA GABRIEL
Askofu mkuu mteule mwandamizi ambaye ni Askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Mwanza muhashamu Yuda Thadeus Ruwa’ichi, amewaomba wakristo wakatoliki wa jimbo hilo kuwa wavumilivu na kumtazama Kristo ambaye ndiye mchungaji mwema katika kipindi hiki anapojiandaa kwenda jimbo kuu la Dar es salaam.

Askofu mkuu Ruwa’ichi amesema hayo baada ya kuhojiwa na Redio Kwizera juu ya namna alivyopokea uteuzi wake kutoka kwa Papa Francis wa kuwa askofu mkuu mwandamizi wa jimbo kuu katoliki la Dar es salaam.
Amesema alipopata taarifa za kuteuliwa kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisco alipatwa na mshtuko kwani hakutarajia kupewa majukumu kama hayo katika kipindi hiki cha maisha yake.
“Nilipozipata taarifa hizi, nilipata mahangaiko na mshtuko hasa ukizingatia kwamba nilishapata vihamo vingine, kwahiyo sikutegemea tena kukutwa na kihamo katika awamu hii ya maisha” amesema Askofu mkuu Ruwa’ichi.

Amewaomba waumini wa jimbo kuu katoliki la Dar-es salaam kumpa ushirikiano na umoja kwa ajili ya utukufu wa Mungu na ustawi wa kanisa
Ikumbukwe kuwa Juni 21 mwaka huu, Baba Mtakatifu Francisco alimteuwa Askofu  mkuu Yuda Thadeus Ruwa’ichi kuwa askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo Kuu katoliki la Dar es Salaam na anatarajiwa kupokelewa na jimbo hilo Septemba 7 mwaka huu.


Post a Comment

0 Comments