habari Mpya


Vifo na Nyumba Kuungua Kimiujiza Vyazua Taharuki Kwa Wakazi wa Kumuzuza wilayani Ngara.

Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Kumuzuza Bw Marthon Christopher akionesha moto ulivyounguza Nyumba ya Mzee Petro huku baadhi ya Wananchi wakishuhudia.

Na -Shaaban Ndyamukama-Radio Kwizera –Ngara.

Nyumba saba zimeungua kwa nyakati tofauti katika kijiji cha Kumuzuza wilayani Ngara mkoani Kagera huku kukitokea vifo vya watoto wawili ndani ya familia moja katika Mazingira ya kutatanisha vikihusishwa kwa imani za kishirikina. 

Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Kumuzuza Bw Marthon Christopher amesema Mtoto wa kwanza amefariki mwezi mmoja uliopita na mwingine amefariki juzi na wote ni wajukuu wa mzee mmoja aitwaye Petro Sabimihana mwenye umri wa miaka 68.

 Bw Christopher amesema watoto waliofariki mmoja ana umri wa miaka minane mwingine miaka miwili na kukutwa chumbani ndani ya nyumba ya mzee huyo ikiwa imefungwa na kwamba nyumba saba zimeungua kuanzia Novemba mwaka jana (2017) na iliyoungua jana chanzo chake hakijafahamika.

 
 
Kwa upande wake Mzee Petro Sabimihana alikiri kuijiwa na miujiza na kuunguliwa na vitu mbalimbali ndani ya nyumba yake na kwamba hadi sasa hana nguo, chakula wala vyombo na moto huo huunguza majiko, vyoo bila kujua chanzo chake.

 Alisema alijitahidi kufanya maombi akisaidiwa na Padri Pamphilius Kitondo ikashindikana ambapo miujiza hiyo hupoteza wajukuu wake kupitia chumba anacholala hata kama kimefungwa hukuta wamefariki.

 
 
 
Baadhi ya Wananchi wa kijiji hicho wamekumbwa na taharuki kuhofia usalama wa maisha yao kwa matukio hayo ya vifo na nyumba kuungua wakiomba vyombo vya usalama kufika kuimarisha amani na utulivu.

 Jeshi la Polisi wilayani Ngara limethibitisha kutokea kwa matukio hayo ambapo mkuu wa wilaya ya Ngara Luteni Kanali Michael Mtenjele amewataka Wananchi kuishi kwa amani na utulivu na kwamba serikali haiamini kuwepo vitendo vya ushirikina.

Post a Comment

0 Comments