habari Mpya


Upungufu wa Miundombinu ya Kujifunzia na Kufundishia Kikwazo cha Taaluma Bora,Biharamulo mkoani Kagera.

Shaaban Ndyamukama - RK NGARA.

Halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera inakabiliwa na upungufu wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi na kusababisha mipango  ya kuboresha taaluma kushindwa kutekelezwa kwa malengo kusudiwa.

Afisa elimu taaluma idara ya msingi wilayani Biharamulo Amosi Nyamtera amebainisha hayo jana  Juni 12 wakati wa kuadhimisha  wiki ya elimu  na kwamba changamoto ni  madawati ambapo yaliyopo ni 16,934 katika vyumba 617 kati ya 1.586  vyenye wavulana 43,927 na wasichana 43136 katika idara hiyo.
 
 
Nyamtera amesema pia wilaya hiyo inahitaji matundu ya vyoo 1,998 kati ya matundu 3,019 yanayohitajika na yaliyopo ni 1021 ambapo nyumba za walimu zinahitajika 1,139 lakini zilizopo ni nyumba 214 na kupungua 925.

Amesema  pia upungufu mwingine ni madawati 6,775 kati ya 23,710 yanayohitajika kwa ajili ya kukaliwa na wanafunzi 87,063 kuanzia elimu ya awali mpaka darasa la saba kukidhi kiwango cha taaluma  na kwamba walimu wanaohitaji nyumba ni  1,139 waliopo kati ya 2,086 wanaohitajika.

Amesema  vyumba vya madarasa vinahitajika 1,586 lakini yaliyopo ni 617 na kupungua vyumba 969 kutosheleza uwiano wa wanafunzi 45 katika chumba kimoja ambapo wilaya hiyo inamiliki shule 85 za serikali zikiwemo  nne za binafsi.

Amesema licha ya mapungufu hayo wilaya ya biharamulo imekuwa na ufaulu wa miaka mitatu kitaaluma mkoani kagera kuanzia mwaka 2015-2017 kwa wastani wa aslimia 85 mpaka asilimia 92 kwa darasa la saba na asilimia 99.5 darasa la nne.

“Ufaulu mzuri umechangiwa na juhudi za  wadau wa elimu, wataalamu,wazazi mashirika na taasisi mbalimbali wakiwemo viongozi wa kisiasa ambao huamasisha jamii kutambua umuhimu wa elimu kwa mtoto” Alisema Nyamtera.

Hata hivyo ametoa wito kwa jamii kuwasomesha watoto wa kike na walio na mahitaji maalum kwa kuwapatia haki ya elimu katika shule zilizobainishwa ambazo ni kabindi na Biharamulo mjini ambapo watapatiwa mahitaji husika.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Afsa Galiatano aliwataka wananchi wa wilaya hiyo pia wadau mbalimbali kuchangia miundombinu katika shule za msingi na sekondari kuboresha kiwango cha taaluma na kutimiza ndoto za watoto wao.
 
 
Aidha amesisitiza  viongozi kila kijiji kuhamasisha wazazi kutowatumikisha wanafunzi na kusababisha utoro wa reja reja unaosababisha wazidi kurudi  nyuma katika masomo yao lakini kuwashauri watoto wa kike kujihadhari na mapenzi ya kingono na kupata ujauzito  katika umri mdogo.

Ameongeza kuwa baadhi ya changamoto zijadiliwe kuanzia ngazi ya vitongoji mikutano ya kila baada ya miezi mitatu na kwenye vikao vya kamati ya maendeleo ya kata huku vikwazo vingine vikifikishwa kwenye baraza la madiwani ili serikali ifanye utekelezaji kwa kuunga nguvu kazi za wananchi.

Maadhimisho ya wiki ya elimu wilayani Biharamulo yamefanyika katika kata ya Nyantakara baada ya kufanya vizuri kitaaluma katika matokeo ya mtihani wa darasa la nne miaka miwili mfululizo 2016 na 2017 kati ya kata 17 wilayani humo.
 

Post a Comment

0 Comments