habari Mpya


Ulevi waponza Fedha za Mpango wa TASAF Kata ya Buhororo,Ngara kutotolewa kwa Walengwa.

Mkutano wa Hadhara ukiendelea Kata ya Buhororo wilayani Ngara mkoani Kagera.Na Shaaban Ndyamukama-Radio Kwizera Ngara.

Jumla ya Shilingi 70,000 zilizotolewa na Mpango wa kusaidia kaya maskini katika kijiji cha buhororo wilaya ya Ngara mkoani Kagera, zinashikiliwa na uongozi wa kijiji hicho kwa ajili ya kuwajengea nyumba walengwa wa fedha hizo baada ya kuonekana kaya husika zinajihusisha na ulevi  na kuendekeza umaskini wao.

Mwenyekiti wa kijiji cha Buhororo Bw Staford  Simon amesema hayo hii May 31,2018 wakati wa mkutano wa hadhara ulioitishwa kwa ajili ya Diwani wa Kata ya Kibimba John Shimimana kusikiliza kero za wananchi na kueleza mikakati ya kuwaletea maendeleo.

Bw Simon amesema katika kijiji hicho kaya tisa zinazonufaika na TASAF zimeonekana kutokuwa na matumizi bora ya fedha hizo hivyo uongozi wa kijiji umeamua kupokea fedha zao na kuwanunulia vifaa vya ujenzi wa makazi yao ambayo ni hayako katika ubora.

 
Awali mmoja wa wakazi wa kijiji hicho Evelina Prosper aliutaka uongozi wa kijiji kuwapatia elimu wanufaika wa tasaf kuanzisha miradi ya kiuchumi kuepuka kuendelea kuitwa watu maskini.

Pia Mwenyekiti huyo amemuomba Diwani kufuatilia serikalini kupata vibao ya usalama barabarani kuwekwa katika kijiji hicho kutokana na kukithiri matukio ya ajali ambapo juzi mwanafunzi wa pili amefariki shule ya msingi buhororo kwa kugongwa na gari.
 
Diwani wa Kata ya Kibimba.

Hata hivyo Diwani wa Kata ya  Kibimba John Shimimana amewataka wakazi wa kijiji katani humo kufanya kazi badala ya wizi na ulevi kujiongezea umaskini.

Amesema kila mmoja afanye kazi halali ambapo amekemea tabia ya kutorosha wanafunzi kwenda kufanya kazi za ndani wilayani kahama ambapo wanafunzi wa buhororo shule ya msingi na sekondari ya Kibimba waetoroshwa na baadhi kurudi baada ya kufanyiwa vitendo vya ukatili huko kahama.

Aidha amesema wananchi wajitahidi kuchangia ujenzi wa zahanati ya kijiji na halmashauri ya wilaya iko katika mpango wa kusambaza maji mpaka kitongoji cha Mubabwile mpakani na kijiji cha Kanazi.

Diwani wa kata ya Kibimba yuko katika ziara ya kutembelea vijiji  kusikiliza maoni na kero za wananchi lakini kuwapatia utekelezaji wa mipango ya halmashauri ya wilaya hiyo.
 
Afisa Ugani wa Kata ya Kibimba.

Kwa upande wake Afisa Ugani wa Kata ya Kibimba Juster Julius amewataka wakulima wa kahawa kusubiria msimu wa mauzo ya zao hilo katika vyama vya ushirika badala ya kuuzwa kwa walanguzi kuepuka faini au kifungo.

Amesema atakaye kamatwa akiuza kahawa kimagendo faini yake Shilingi milioni 8  au kifungo cha miaka sita gerezani na watakaokaidi kutokomeza ugonjwa wa mnyauko watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.
 

Post a Comment

0 Comments