habari


Shirika la Nyumba la Taifa NHC Kupima Viwanja 5,000 Chato mkoani Geita.

Na Gibson Mika RK –Geita.

Shirika la Nyumba la Taifa  NHC limesaini Mkataba wa makubaliano na halmashauri ya wilaya ya Chato Mkoani Geita katika  kupima viwanja vya makazi ya watu 5000 kwa lengo la kutengeneza mpango mji nzuri utakaosaidia halmashauri hiyo kukusanya mapato makubwa ya ndani.

Akizungumza na Radio Kwizera Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa Bw.Felix Maagi amesema kuwa kwa awamu ya kwanza Shirika hilo linatarajia kuanza kupima viwanja 1,200 katika eneo la Rubabangwe wilayani humo.

Hata hivyo, Bw. Maagi amesema NHC kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekusudia kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa wakati ili kutimiza mahitaji ya halmashauri hiyo.
 
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Chato Bw.Joel Hali amesema kukamilika kwa upimaji wa viwanja utasaidia kuboresha mazingira na  kuongeza mapato ya ndani yatakayotokana upimaji pamoja na  kodi ya majengo.

Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Bw.Bathoromeo Christian amesema kupitia upimaji wa viwanja hivyo utawasaidia wananchi wa maeneo hayo kuwa na hati itakayo wasaidia katika maendeleo yao na kwamba katika nyumba hizo zitakazojengwa  zitakuwa na mahitaji yote ya  kijamii.  
 

Post a Comment

0 Comments