habari Mpya


Bodi ya Wakulima wa Kahawa Ngara Farmers yashindwa Kukabidhi Mali za Chama kwa Wajumbe Wapya.

Na Shaaban Ndyamukama-Radio Kwizera Ngara.

Bodi ya Wakulima Kahawa ya chama cha wakulima cha Ngara Farmers mkoani Kagera iliyomaliza muda wake imeshindwa kukabidhi mali za chama hicho kwa wajumbe  wa bodi  mpya ambayo imeundwa  mwaka huu (2018) baada ya kuwepo mgogoro wa nyaraka na mali inayokabidhiwa.

 Akitoa taarifa ya Mali za aina mbalimbali za Ngara Farmers aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi ya zamani Bw.Steven Runzanga amesema wajumbe  wa bodi mpya wapokee majengo, mitambo, na nyaraka yakiwemo madeni ya makarani, na deni la benki ya NMB la Shilingi milioni 50.7.

 
Bw.Runzanga amesema katika chama hicho kumeshindikana ulipaji wa madeni kutokana na kushindwa kuuza wala kununua kahawa kutoka kwa wakulima zaidi ya miaka mitatu iliyopita baada ya kukabidhiwa chama kisichokuwa na  fedha kama mtaji wa uzalishaji.

Aidha Bw.Runzanga amesema bodi  ijipange kuboresha miundombinu ya kiwanda cha kukoboa kahawa badala ya kupeleka kwenye viwanda vingine na kuongeza gharama za uendeshaji na lakini pia kumpunja mkulima pamoja na kupunguza uaminifu katika ushindani wa kibiashara.

Baadhi ya wajumbe wa bodi mpya  ya mpito kwa kipindi cha mwaka mmoja wamehoji mali iliyo halisi ya kuonekana au nyaraka mbalimbali ambazo hazifafanui  uhalisia na kuondoa wasiwasi katika kutekeleza majukumu.

Hata hivyo Mwenyekiti mpya wa bodi ya chama hicho Bw David Bukozo (Pichani ) amesema wajumbe wenzake hawawezi kukabidhiana mali za chama cha wakulima hadi kufanya marekebisho ya nyaraka na takwimu za mali baada ya kubainika baadhi kuwa na utata katika umiliki wake.

Bw.Bukozo  pia amekanusha bei ya kahawa inayotangazwa ya Shilingi 1000 na Shilingi 1200 kwa kilo sababu  serikali haijatangaza ispokuwa kiwango hicho ni sehemu ya mauzo kwenye chama cha ushirika hivyo wakulima wajipange kuuza kahawa yao mnadani katika soko la Moshi.

Amewataka wakulima wa zao hilo kuanza uvunaji na kulipeleka kwenye chama cha ushirika cha Ngara Farmers na mkulima hatapewa   fedha taslimu bali atafungua akaunti yake binafsi katika taasisi za kibenki  kwa watakaokuwa na a kiwango kikubwa cha mauzo.

Amesema kwa mkulima mwenye kuuza kahawa kuanzia zia kilo moja kufikia tani moja atafungua akauti kwa kutumia simu yake ya  mkononi akitumia mtandao wa mawasiliano na kuingiziwa malipo kwa lengo la kudhibiti matukio ya usalama .

Aidha Meneja wa Chama hicho Bw Hamphrey Kachecheba amesema baada ya kupata akaunti kutajazwa fomu maalum za usajili kutoka taasisi za kibenki kwa ajili ya kuwabaini wasiojua kusoma na kuandika kuchagua watu waaminifu wa kuwachukulia fedha za malipo ya mauzo.

Post a Comment

0 Comments