habari


Benki ya wakulima yatoa bilioni 1 na milioni 226 kununua kahawa ya wakulima wilayani Ngara.


NGARA:NA SHAABAN NDYAMUKAMA RK
Benki ya wakulima imetoa mkopo wa  shilingi bilioni moja na milioni 226 kwa ajili ya manunuzi ya zao la kahawa kupitia chama cha wakulima cha Ngara farmers wilaya ya Ngara mkoani Kagera kinachotegemea kununua tani 2000   msimu huu.

 Afisa kilimo wilayani Ngara Costantine Mudende amesema fedha hizo zimetolewa ambapo chama hicho kililenga kutenga shilingi milioni 300 na kwamba mkulima akipeleka zao hilo kwenye chama cha ushirika atalipwa kianzio cha shilingi 1000
Bw Mudende amesema baada ya kahawa kupelekwa kwenye chama cha ushirika na kupewa fedha za kianzio itapelekwa  mnadani  wilaya ya Moshi  na nyongeza ya malipo ya pili yatapatikana ikitangazwa bei katika soko la dunia.

Pia  Afisa mtendaji wa kijiji cha Mukikomero wilayani Ngara  Dauson Bwoba amewataka wananchi kuzingatia ushauri  wa serikali unaohimiza kila mkulima wa kahawa kuanika zao hilo kwenye chanja juu ya  matulubai kulinda ubora unaotakiwa kwenye soko la dunia

Hata hivyo mkuu wa wilaya ya Ngara Luteni Kanali Michael Mntenjele amesema ni marufuku mtu yeyote au kampuni kununua kahawa ya wakulima kinyemela kwa njia ya magendo  kwa kahawa iliyokomaa au mbichi kutoka shambani na kwamba atakayekamatwa atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Hivi karibuni waziri wa kilimo Charles Tizeba akiwa katika ziara ya kiutendaji mkoani Kagera aliagiza  uvunaji wa kahawa ufanyike kwa kuzingatia usafi yaani kuvuna zilizokomaa na kuiva zikionesha rangi nyekundu na kuanikwa kwenye chanja


Pamoja na hayo mmoja wa wakazi wa kijiji cha Mikikomero Alfred Bishundu amesema wakulima wameanza kutekeleza zoezi hilo la uvunaji na uanikaji kwa kutumia chanja na kwamba  wanatumia gharama kubwa ya kununua matulubai, miti na nyasi wakati kiwango cha bei ya zao la kahawa kwa msimu huu hakijajulikana.

Post a Comment

0 Comments