habari Mpya


Wauguzi wilayani Ngara, tumieni Lugha rafiki na Upendo kutibu Wagonjwa''.

Picha/Habari Na Laurent Gervas /Shaaban Ndyamukama -Radio Kwizera Ngara.

Idara ya afya wilayani Ngara Mkoani Kagera inakabiliwa na upungufu wa Wauguzi na Waganga Wafawidhi katika Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali kwa ajili ya kutoa huduma bora za matibabu kupunguza changamoto za vifo vinavyojitokeza ndani ya Jamii wilayani humo.

Taarifa hiyo imetolewa na mmoja wa Wauguzi ,Bw. Richard Alphonce wakati akisoma risala ya siku ya wauguzi iliyoadhimishwa Jana May 30, 2018  badala ya May 12, mwaka huu kutokana na sababu zisizozuilika .

Bw. Alphonce amesema pamoja na utoaji huduma, Wauguzi wanaohitajika wilayani Ngara ni 388 kati ya hao waliopo ni 242 na upungufu uliopo ni Wauguzi 146 na kwamba upungufu huo unachangia Wananchi kuchelewa kupata huduma za afya.


Pichani wauguzi wakiwa katika Maandamano ya pamoja kuadhimisha siku ya Wauguzi.


Aidha Muuguzi mkuu wa wilaya hiyo Triphonia Rusilibana aliwataka Wauguzi Vijana kuwa na kauli nzuri kwa Wagonjwa kwa kutanguliza upendo, kufanya kazi wakizingatia misingi ya kitaaluma ambazo ni taratibu, kanuni na sheria za kazi.

Pia aliwataka kutanguliza uvumilivu katika kutekeleza na kutimiza wajibu wa kiutendaji lakini watumie nafasi zao kujiendeleza kitaaluma badala ya kuridhika na elimu ya ngazi ya cheti ili waweze kupata daraja kubwa kulitumikia taifa.


Pichani wakwanza kutoka kushoto ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Murgwanza Dr.Remmy wapili ni Dr.David Mapunda na watatu ni Muuguzi mkuu wa wilaya ya Ngara Bi.Triphonia Rusilibana.


Hata hivyo Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo ya Ngara mkoani Kagera ambaye ni Mratibu wa Afya ya Kinywa na Meno Dkt. David Mapunda amewasihi kufanya kazi kwa nidhamu , upendo na huruma ili husaidia kufariji mgonjwa hata kama mwili wake unakaliwa na maumivu hivyo kumuongezea matumaini na siku za kuishi bila kukata tamaa au kulazimika kutumia dawa zisizo na vipimo.


Wauguzi wakila kiapo kujikumbusha maneno ya utumishi bora katika utendaji kazi hasa wakimuenzi mwanzilishi wao Frolence Night Ngare.

Post a Comment

0 Comments