habari Mpya


Watumishi Wawili Halmashuri ya Wilaya ya Karagwe Wasimamishwa Kazi kwa Upotevu Shilingi Milioni 500.

Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya  Karagwe, Wajumbe wa Kamati ya Fedha (Madiwani) na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wakisikiliza Maagizo ya Mhe. Kijuu.

Na: Sylvester Raphael

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu leo Mei 31, 2018 awasimamisha kazi watendaji wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kufuatia utendaji usioridhisha wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kieletroniki na kusababisha upotevu wa kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 500 katika Halmashauri hiyo.

Hatua hiyo imechukuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera baada ya Katibu Tawala wa Mkoa CP Diwani Athuman kuunda tume ya uchunguzi wa upotevu wa fedha hizo kutokana na ripoti ya Mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe ambapo tume hiyo ilifanya kazi ya uchunguzi kwa siku nne tu na kubaini upotevu fedha cha shilingi 500,000,000/=
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu (Aliyesimama) Akitoa Maagizo ya Kuwasimamisha Kazi  Watumishi Wawili Wilayani Karagwe.

Uamuazi wa kuwasimamisha kazi watumishi wawili Afisa TEHAMA Bw. Beatus Nyarugenda na Mhasibu wa Mapato Bw. Innocent Kakulima ulitolewa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu katika kikao cha Kamati ya Fedha cha Halmashauri hiyo ambapo alitoa maagizo kama ifutavyo;
 
MOJA, Uchunguzi wa kina ufanyike kwa kila Maafisa walioomba na kuidhinisha marekebisho au miamala ya mapato ya ndani katika mfumo bila kuwa na kibali cha Afisa Masuuli na kiasi cha fedha kinachohusika katika eneo hilo ni Shilingi 427,027,430.49/=
 
PILI, Watumishi waliokusanya mapato na hawajapeleka benki fedha walizokusanya jumla ya Shilingi 127,094,900/= hadi tarehe 14 Aprili, 2018 waziwasilishe katika akaunti ya mapato ya Halmashauri ndani ya siku 7, na vielelezo vihakikiwe na Katibu Tawala wa Wilaya ya Karagwe na watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo sheria ichukue mkondo wake.
 
TATU, Afisa TEHAMA Bw.Beatus Nyarugenda tume ilimbaini kuwa hakuwa makini kwa kukiuka usalama wa mtandao kwa kutoa haki kwa Afisa mmoja kukamilisha muamala mzima wa kufuta ama kubadili tarakimu za fedha katika mtandao. Mkuu wa Mkoa aliagiza utaratibu huo uachwe mara moja na Mkuu wa TEHAMA wa Mkoa kuhakikisha usalama wa mfumo unawekwa vizuri mara moja.
 
NNE, Mhasibu wa Mapato Bw. Innocent Kakulima tume ilimbaini kutokuwa na uthibitisho wa kupeleka benki shilingi 23,216,400/= fedha ambazo alizichukua kutoka kwa wakusanyaji. Aidha katika ufuatiliaji ilibainika kuwa katika Halmashauri ya Karagwe kuna vituo vya ukusanyaji (POS) 39, hivyo inahitajika uchunguzi zaidi ili kuwa na uhakika katika vituo vyote kama Mhasibu huyo hakukusanya fedha.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Karagwe Wamkimsikiliza Mkuu wa Mkoa kwa Makini.

Baada ya maagizo hayo Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu alimwagiza Kamanda wa TAKUKURU Mkoa kupokea taarifa hiyo kwa ajili ya kuifanyia uchunguzi ambao utatoa majibu sahihi ya kushuka kwa mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.

 Aidha, wakati uchunguzi unafanyika Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu aliagiza Afisa TEHAMA Bw. Beatus Nyarugenda na aliyekuwa Mhasibu wa Mapato Bw. Innocent Kakulima wasimame kazi kupisha uchunguzi huo. 

Pia aliagiza kuwa wakati uchunguzi unaendelea watuhumiwa wengine watakaobainika kuwa wanaweza kuingilia uchunguzi wawapo maeneo yao ya kazi ajulishwe haraka ili nao wahusishwe kupisha uchunguzi.

Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu alihitimisha kwa kurudia kumuagiza Kamanda wa TAKUKURU Mkoa kufanya Uchunguzi na kuukamilisha haraka pia na kuzitahadharisha Halmashauri nyingine za Wilaya za Mkoa wa Kagera hususani Wakurugenzi Watendaji na Watumishi wengine kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu mkubwa bila kujihusisha na vitendo vya kuyahujumu mapoto hasa mapato ya ndani ya Serikali.

Post a Comment

0 Comments