habari Mpya


Wananchi Kakonko waitikia Kampeni ya Damu Yako,Maisha Yangu ya Radio Kwizera FM.

Ni katika harakati za uhamasishaji wananchi kujitokeza kuchangia damu hii leo May 12, 2018 katika viunga vya uwanja wa mpira jirani kabisa na kanisa kuu la parokia ya MT.Therezia , Kakonko mkoani Kigoma.

 Kwa mujibu wa mganga mkuu wa wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma ,Dr.Joseph Tutuba amesema mahitaji ya damu katika wilaya hiyo ni lita 180 ambapo kwa wastani katika siku zinatakiwa kuwepo lita sita.

Amesema wilaya hiyo inahudumia vituo vya afya vinne kikiwemo kituo cha afya Nyakanazi kilicho umbali wa kilomita 42 badala ya kilomita 67 kwenda hospitali teule ya Biharamulo mkoani Kagera.


Amesema zipo pia zahanati 26 ambapo makadilio kwa mwaka wilaya hiyo hutibu wagonjwa 123,000 kati ya hao wenye mahitaji ya damu salama ni kati ya 18,000 mpaka 20,000.

Dr.Tutuba amebainisha kuwa miongoni mwa wagonjwa ni watoto chini ya miaka mitano, akina mama wajawazito, wenye kupata ajali mbalimbali, na wenye lishe duni wanaokabiliwa na utapiamlo.

Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma ina watoto chini ya miaka mitano wapatao 38, 700 ambapo asilimia 40 ya watoto hao wanakabiliwa na uzito pungufu (udumavu) na asilimia 4 wana utapiamlo mkali na sababu kubwa ni umaskini kwani wilaya ya Kakonko ndio ya kwanza kwa umakini nchini.

Hata hivyo amesema wananchi wakielimishwa umuhimu kutumia vyakula bora vyenye lishe sahihi kwa maana ya makundi ya vitamini, Protini, wanga na mafuta katika uwiano sahihi uwezekano wa kuhitaji damu katika jamii utapungua.


Picha/Habari Na Team Damu Salama/Radio Kwizera-Kakonko.

Post a Comment

0 Comments