habari Mpya


Waleteni Watoto Kupata Chanjo Zahanati ya Bugarama wilaya ya Ngara.

Jumla ya watoto 100 wamejitokeza kupata chanjo ya aina mbalimbali katika zahanati ya kijiji cha Bugarama wilaya ya Ngara mkoani Kagera licha ya mganga wa kutoa chanjo hiyo kuwa mmoja katika Zahanati na kusababisha akina mama kusongamana wakati wakihitaji huduma.
Wakiongea na Radio Kwizera Hivi Karibuni katika Zahanati hiyo baadhi ya wazazi wenye watoto chini ya miaka mitano waliopeleka watoto wao kupata chanjo wamesema wanapata usumbufu mkubwa kwa sababu ya kuhudumiwa na mganga mmoja.

Aidha Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Bugarama, Yudosia Ntaramuka amesema kila siku anatoa huduma ya kuwatibu wagonjwa, wajawazito na chanjo kwa watoto na wastani wa wagonjwa ni kati ya 30 hadi 40 kwa siku na wanahitajika watumishi tisa kuweza kumudu wateja wanaojitokeza.
Baadhi ya wanawake waliokuwa katika Zahanati hiyo walisema wanahangaika sana kupata huduma kutokana na msululu au msongamano wa wanaohitaji huduma.

Hata hivyo Mwenyekiti wa kijiji cha Bugarama Jaafari Saidi amesema Serikali ya halmashauri ya wilaya hiyo ijaribu kuongeza watumishi kusaidia wananchi kupata huduma bora za afya kwani zahanati hiyo inahudumia vijiji vya Bugarama na Rwinyana.


Habari/Picha na Shaaban Ndyamukama.

Post a Comment

0 Comments